杏MAP导航

Tafuta

Viaggio Apostolico in Lituania Lettonia Estonia 2018.09.22

Ujumbe wa Papa wa Siku ya 33 ya Wagonjwa Duniani 2025:Mungu anapitia kukutana,zawadi na kushiriki!

Papa Francisko ametoa Ujumbe wa Siku ya 33 ya Wagonjwa Ulimwenguni itakayofanyika tarehe 11 Februari,sambamba na kumbukizi ya Bikira Maria wa Lourdes.Katika Ujumbe huo unaongozwa na kuuli mbiu:“Matumaini hayakatishi tamaa(Rm5,5),lakini yanatutia nguvu wakati wa majaribu."Katika ujumbe huo Papa anaelezea wanaoteseka na wanaotoa huduma kuwa Mungu anapitia kwa njia tatu maalum:kupitia kukutana,zawadi na kushirikiTunatambue kwamba sisi ni “malaika” wa matumaini na wajumbe wa Mungu.

Na Angela Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ametoa ujumbe wake wa Siku ya 33 ya Wagonjwa duniani sanjari na kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, iadhimishwayo kila ifikapo tarehe 11 Februari ya kila Mwaka. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko unaongozw ana kauli mbiu:"Tumaini halitahayarishi"(Rm 5:5), lakini hutuimarisha wakati wa majaribu". Papa Francisko katika ujumbe anabainisha kwamba: “Tunaadhimisha Siku ya 33 ya Wagonjwa Duniani katika Mwaka wa Jubilei 2025, ambapo Kanisa linatualika kuwa “mahujaji wa matumaini.” Neno la Mungu linatusindikiza na kutupatia, kwa maneno ya Mtakatifu Paulo, ujumbe wa kutia moyo: “Tumaini halitahayarishi”(Rm 5:5); hakika, linatutia nguvu wakati wa majaribu.” Hayo ni maneno ya kufariji, lakini yanaweza pia kutatanisha, hasa kwa wale wanaoteseka. Tunawezaje kuwa na nguvu, kwa mfano, wakati miili yetu inaathiriwa na magonjwa mazito, yenye kudhoofisha ambayo yanahitaji matibabu ya gharama ambayo hatuwezi kumudu? Je tunawezaje kuonesha nguvu wakati, zaidi ya mateso yetu wenyewe, tunaona wapendwa wetu wanaotuunga mkono bado wanahisi kutokuwa na uwezo wa kutusaidia? Katika hali hizi, tunahisi hitaji letu la nguvu kubwa kuliko zetu. Tunatambua kwamba tunahitaji msaada wa Mungu, neema yake, Utoaji wake, na nguvu ambayo ni zawadi ya Roho wake (taz. Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 1808).

Kukutana:kuwasaidia wagonjwa kuona udhaifu wao

Katika hili Papa Francisko anakazia kusema,  hebu tutafakari jinsi Mungu anavyoendelea kuwa karibu na wale wanaoteseka kwa njia tatu maalum: kupitia kukutana, zawadi na kushiriki. Papa alianza na kipengele cha “kukutana.” Wakati Yesu alipowatuma wanafunzi sabini na wawili kwenda kwenye utume (rej. Lk 10:1-9), aliwaambia wawatangazie wagonjwa: “Ufalme wa Mungu umekaribia kwenu” (Lk 10, 9). Aliwaomba, kwa maneno mengine, kuwasaidia wagonjwa kuona udhaifu wao, hata jinsi uchungu na usioweza kueleweka unavyoweza kuwa, kama fursa ya kukutana na Bwana. Wakati wa ugonjwa, tunahisi udhaifu wetu wa kibinadamu katika viwango vya kimwili, kisaikolojia na kiroho. Lakini pia tunapitia ukaribu na huruma ya Mungu, ambaye, katika Yesu, alishiriki katika mateso yetu ya kibinadamu. Mungu hatutupi na mara nyingi hutushangaza kwa kutupa nguvu ambayo hatukutarajia kamwe, na tusingeipata peke yetu. Ugonjwa, basi, unakuwa tukio la kukutana kwa mabadiliko, ugunduzi wa mwamba imara ambao tunaweza kushikilia sana katikati ya dhoruba za maisha, uzoefu ambao, hata kwa gharama kubwa, hutufanya sisi sote kuwa na nguvu zaidi kwa sababu unatufundisha kwamba hatuko peke yetu.. Mateso  huja pamoja  daima na  ahadi ya ajabu ya wokovu, kwa kuwa hutufanya tupate uzoefu wa ukaribu na ukweli wa uwepo wa kufariji wa Mungu. Kwa njia hiyo, tunapata kujua “utimilifu wa Injili pamoja na ahadi na uzima wake wote” (MTAKATIFU ??Yohane Paulo II , Hotuba kwa Vijana, New Orleans, 12 Septemba 1987).

Zawadi: Mateso hutufanya tutambue kuwa tumaini linatoka kwa Bwana

Papa Francisko alikazia kusema kuwa na hiyo inatuleta katika njia ya pili ya kwamba Mungu yuko karibu na mateso na kwa hyo  kama zawadi. Zaidi ya kitu kingine chochote, mateso hutufanya tujue kwamba tumaini hutoka kwa Bwana. Kwa hivyo, kwanza kabisa, ni zawadi inayopaswa kupokelewa na kukuzwa, kwa kubaki “mwaminifu katika uaminifu wa Mungu”, katika usemi mzuri wa Madeleine Delbrêl (taz. La speranza è una luce nella note, Mji wa Vatican 2024, Dibaji.)Hakika, ni katika ufufuko wa Kristo pekee ambapo maisha na hatima yetu hupata nafasi yake ndani ya upeo usio na kikomo wa umilele. Katika fumbo  pekee la Pasaka ya Yesu tunapata uhakika kwamba “wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho cho chote; utaweza kututenganisha  na upendo wa Mungu” (Rm 8:38-39). “Tumaini hili kuu” ndilo chanzo cha miale yote hiyo midogo ya nuru inayotusaidia kuona njia yetu kupitia majaribu na vizuizi vya maisha (taz.Benedikto XVI, Spe Salvi, 27, 31). Bwana mfufuka anakwenda mbali zaidi na kutembea kando yetu kama msindikizaji njiani, kama alivyofanya na wanafunzi katika njia ya kwenda Emau (taz. Lk 24:13-53). Kama wao, tunaweza kumweleza mahangaiko, masumbuko na masikitiko yetu, na kusikiliza neno lake, ambalo hutuelimisha na kuchangamsha mioyo yetu. Kama wao pia, tunaweza kumtambua akiwapo katika kuumega mkate na hivyo, hata katika hali ya sasa, kuwa na maana ya “ukweli mkuu” ambao, kwa kutukaribia, huturudishia ujasiri na uhakika wetu.

Kushiriki: maeneo ya mateso mara nyingi ni sehemu ya kugawana na kutajirishana

Baba Mtakatifu Francisko amefikiria njia ya tatu ya Mungu ya kuwa karibu nasi: kupitia kushiriki. Maeneo ya mateso mara nyingi pia ni sehemu za kugawana na kutajirishana. Ni mara ngapi, kando ya kitanda cha wagonjwa, tunajifunza kutumaini! Ni mara ngapi, kwa ukaribu wetu na wale wanaoteseka, tunajifunza kuwa na imani! Ni mara ngapi, tunapowajali wale wanaohitaji, tunagundua upendo! Tunatambua kwamba sisi ni “malaika” wa matumaini na wajumbe wa Mungu sisi kwa sisi, sisi sote kwa pamoja: iwe wagonjwa, waganga, wauguzi, wanafamilia, marafiki, makuhani, wanaume na wanawake watawa, haijalishi tulipo, iwe katika familia au zahanati, nyumba za wazee, hospitali au vituo vya matibabu. Tunahitaji kujifunza jinsi ya kuthamini uzuri na umuhimu wa mikutano hii iliyojaa neema. Tunahitaji kujifunza jinsi ya kuthamini tabasamu nyororo la muuguzi, shukrani na uaminifu wa mgonjwa, uso unaojali wa daktari au mfanyakazi wa kujitolea, au sura ya wasiwasi na ya kutarajia ya mwenzi, mtoto, mjukuu au rafiki mpendwa. Yote hii ni miale ya nuru ya kuhifadhiwa; hata katikati ya usiku wa giza wa shida, hutupatia nguvu, wakati huo huo hutufundisha maana ya ndani zaidi ya maisha, katika upendo na ukaribu (rej. Lk 10:25-37).

Wagonjwa/ wanaowasaidia wanatimiza sehemu muhimu ya matumaini

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huo, anakazia kuwalekeza kaka na dada   ambao ni wagonjwa au wanaowasaidia wanaoteseka, katika Jubilei hii kwamba “mnatimiza sehemu muhimu sana. Safari yenu pamoja ni ishara kwa kila mtu ya : “wimbo kwa utu wa binadamu, wimbo wa matumaini” (Spes Non Confundit, 11). Matatizo yao yanasikika mbali zaidi ya vyumba na vitanda vya vituo vya afya, na kusaidia katika kutoa misaada “ushiriki wa kwaya wa jamii kwa ujumla” katika maelewano ambayo nyakati fulani ni magumu kufikiwa, lakini kwa sababu hiyohiyo inafariji sana na ina nguvu, inayoweza kuleta mwanga na joto popote inapohitajika zaidi. “Kanisa zima linakushukuru kwa hili! Mimi pia hufanya hivyo, na ninawakumbuka daima katika sala zangu. Ninawakabidhi kwa Mama Yetu, Afya ya Wagonjwa, kwa maneno ambayo kaka na dada zetu wengi wamemwambia wakati wa shida:

Tunakimbilia ulinzi wako, ee mzazi Mtakatifu wa Mungu. Usitunyime tukiokumba katika shida zetu, lakini utuokoe daima na hatari zote, ee Bikira mtukufu na mwenye baraka.

Papa Francisko anahitimisha ujube huu kwa kuwabariki  pamoja na familia zao na wapendwa wao, na anawaomba, tafadhali, wasisahau kumuombea.

Ujumbe wa Papa wa SIKU ya XXXIII ya Wagonjwa Duniani
27 Januari 2025, 12:57