Papa kwa wakuu wa usalama Vatican:Kuishi na kutenda kwa manufaa na wengine!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Alhamisi tarehe 23 Januari 2025, Baba Mtakatifu Francisko alikutana na kuzungumza wasimamizi na wafanyakazi wa Ukaguzi wa Usalama wa Umma wa “Vatican.” Katika hotuba yake, ameonesha furaha ya kukutana nao katika mwanzo wa mwaka na kama ilivyo desturi yak ila mwaka ya kukutana nao. Papa alibainisha kuwa hii ni nafasi nzuri ya kuwatakia wao bara tele familia zao kwa mwaka wa 2025, mwaka wa Jubilei, ambao tumealikwa kuelekeza mitazamo yetu kwa Yesu Kristo, tumaini letu, anayejifanya kuwa msafiri pamoja nasi na anayetaka kujitoayeye mwenyewe kuwa baraka zake na msamaha wake. Papa Francisko aidha aliwaalika wachukue fursa ya Mlango Mtakatifu uliofunguliwa usiku wa Noeli katika Basilika ya Mtakatifu Petro, pamoja na yale yaliyofunguliwa baadaye katika Basilika zingine za Kipapa za Roma. Kuvuka Mlango Mtakatifu sio kitendo cha kiinnimacho, hapana,- ni ishara ya Kikristo - Yesu mwenyewe anasema: "Mimi ndimi mlango (Yh 10: 7), ishara inayoonesha hamu ya kuanza tena na hii ni hekima nzuri, kuanza tena, kila siku. Na daima kwenda hatua moja mbele. Shauku ya kujipyaisha na kujiruhusu kupatikana na Mungu.
Baba Mtakatifu alibainisha tena kwamba “Na yeyote asiyetambua kwamba ana karama ya imani, bado anafaa kuchukua fursa ya Mwaka huu wa Jubilei ili kusonga mbele. Baba Mtakatifu aliendelea kuwashukuru kwa kazi zote wanazozifanya, kwa kujitolea, weledi na ukarimu, ili kuhakikishia usalama wa Papa, washiriki wake, mahujaji na watalii wote katika eneo la Vatican na vile vile wakati wa ziara yake ya kichungaji nchini Italia. 'Asante sana!' Hii ni kazi yao, ambayo ni ya lazima kila wakati Papa aliitambua na kwamba “inahitaji utayari na ujasiri na ambayo mara nyingi hufanywa kwa busara, bila kutambuliwa, lakini ambayo inaonesha kujikana, kuzingatia kila undani, uvumilivu na ustadi kupatikana kwa kujitoa sadaka. Usalama kiukweli ni mali isiyoonekana ambayo umuhimu wake tunafahamu kwa usahihi wakati, kwa sababu fulani, unapokosekana, na ambao hujengwa kupitia juhudi za ufuatiliaji wa mara kwa mara na wa akili, usiku na mchana, kila siku ya mwaka. Wanadamu waliojeruhiwa na dhambi hufanya kazi ya nguvu za umma kuwa ya lazima, iliyowekwa katika huduma ya manufaa ya wote ya jumuiya nzima, ambayo ina zana zinazofaa za kulinganisha na kuwazuia wale ambao wanakaribia kufanya uhalifu na makosa.”
Papa Francisko alisema kuwa wao “wanaweza kujivunia sana kuishi na kutenda kwa manufaa ya wote na wakati huo huo kubaki wanyenyekevu, kwa sababu hiyo inawawezesha kujitambua kuwa wanahitaji msaada, wa baraka, wa ukombozi, na kuweka moyo wao wazi kwa neema ya Mungu.” Papa Francisko kwa Mawakala na Viongozi hawa amewasihi wafahamu kwamba Papa huwafikiria wao mara kwa mara na kwa shukrani,na anawaombea wao na familia zao. Na wakati makatibu wake wanapokwenda kuwatembelea kila Dominika ili kuwapelekea chokoleti au kitu kama hicho, Papa ameongeza kusema kuwa "ni ishara, lakini ishara inayoonesha ukaribu" wake Papa. Amewashukuru tena na kwamba “Mama Yetu na awasindikize na Mtakatifu Malaika Mkuu Mikaeli, Msimamizi wao, awalinde. Papa hatimaye amewabariki kutoka moyoni mwake. Na amewaomba, tafadhali, wamwombee na siyo dhidi yake.