杏MAP导航

Tafuta

Papa afunga Juma la kuombea Umoja wa Kristo:Tuvumbue tena mizizi ya imani kuelekea umoja

Kanisa Katoliki liko tayari kukubali tarehe yoyote ya pamoja ya maadhimisho ya Pasaka na wakristo wengine ambayo katika kalenda ya Julian na Gregorian ni sawa na kuadhimisha miaka 1,700 ya Baraza la kwanza la Kiekumene la Nikea.Injili inatuambia kuwa pamoja na Yesu tumaini daima huzaliwa upya,kwa sababu kutoka katika majivu ya kifo,Yeye hutufufua,hutuinua,hutupatia nguvu ya kuendelea na safari yetu na kuanza tena.Ni tafakari ya Papa katika kufunga Juma la kuombea Umoja wa Kikristo.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Jumamosi jioni tarehe 25 Januari 2025, Mama Kanisa akiwa anaadhimisha siku kuu ya Uongofu wa Mtakatifu Paulo Mtume wa Watu, sanjari na kuhitimisha Juma la Maombi kwa ajili ya Umoja wa Wakristo, lililoanza tangu tarehe 18 Januari, Baba Mtakatifu Francisko aliongoza Masifu ya Jioni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo , Nje ya Ukuta Roma. Mara baada ya zaburi na Injili,  Baba Mtakatifu Francisko alianza tafakari yake kwa kusema kuwa, Yesu alifika katika nyumba ya marafiki zake Marta na Maria wakati kaka yao  Lazaro alikuwa amekwisha kufa, siku nne kabla. Kila tumaini utafiriki lilikuwa limepotea hadi kufikia maneno ya kwanza ya Marta anaelezea uchungu wake pamoja na kulalamika kwa sababu Yesu alifika amechelewa kuwa: “Bwana kama ungekuwa hapa, kaka yangu hasingekufa (Yh 11,21). Na wakati huo huo, lakini alifika Yesu akawasha nuru ya tumaIni katika moyo wa Martha na kumpelekea kukiri imani kwamba: “Hata sasa ninajua kuwa chochote ukiombacho kwa Mungu, Mungu atakupatia”(rej. Yh 11, 22). Na ndiyo tabia ambayo inaacha mlango wazi daima na haufungwi kamwe, Papa alisisitiza. Kutokana na hilo, Papa Francisko alipenda kujikita na neno hilo  la “Je unaamini hilo? (Yh 11,26) na kuongeza kusema kuwa hili ndili swali ambalo hata sisi sote na yeye pia, tunapaswa kujiuliza iwapo tunaamini.

Maadhimisho ya masifu ya jioni 25 Januari
Maadhimisho ya masifu ya jioni 25 Januari   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Wakati mwingine tunaelemewa na ushirikiano wa kiekume

Papa aliendelea kusema kuwa Mkutano huu wa huruma kati ya Yesu na Martha, ambao tulisikia katika Injili, unatufundisha kwamba, hata katika nyakati za ukiwa, hatuko peke yetu na tunaweza kuendelea kutumaini. Yesu anatoa uzima, hata inapoonekana kwamba tumaini lote limetoweka. Baada ya hasara yenye uchungu, ugonjwa, kukatishwa tamaa kwa uchungu, usaliti, au mambo mengine magumu, tumaini linaweza kudhoofika; lakini ikiwa kila mmoja wetu anaweza kupata nyakati za kukata tamaa au kukutana na watu ambao wamepoteza matumaini, Injili inatuambia kwamba pamoja na Yesu tumaini daima huzaliwa upya, kwa sababu kutoka katika majivu ya kifo, Yeye hutufufua daima.

Yesu hutuinua daima, hutupatia nguvu ya kuendelea na safari yetu na kuanza tena. Papa Francisko alisisitiza kuwa, “tusisahau kamwe kuwa tumaini halikatishi tamaa; matumaini kamwe hayakatishi tamaa. Tumaini ni kamba  ambayo tunashikilia katika nanga kwenye pwani. Na hiyo hakatishi tamaa kamwe! Hili pia ni muhimu kwa maisha ya Jumuiya za Kikristo, Makanisa yetu na mahusiano yetu ya kiekumene. Wakati mwingine tunaelemewa na uchovu, tunakatishwa tamaa na matokeo ya juhudi zetu, inaonekana kwetu kwamba hata mazungumzo na ushirikiano kati yetu hauna matumaini na karibu kufa na haya yote yanatufanya tupate uchungu sawa na Martha; lakini Bwana anakuja na kuuliza kuwa:  Je, tunaamini katika hili? Je, tunaamini kwamba Yeye ni ufufuo na uzima? Ni nani  anayekusanya juhudi zetu na daima kutupatia neema ya kuanza tena safari pamoja? Je, tunaamini hili? Papa aliuliza maswali hayo.

Mafifu ya jioni
Mafifu ya jioni   (Vatican Media)

Ujumbe wa matumaini ni kiini cha Jubilei: Roho ndiye anayetuongoza

Ujumbe huu wa matumaini ndiyo kiini cha Jubilei tuliyoianza, Baba Mtakatifu alisema. Mtume Paulo, ambaye tunamkumbuka kuongoka kwake kwa Kristo leo hii, aliwatangazia Wakristo wa Roma kwamba: “Tumaini halitahayarishi, wala halikatishi tamaa, kwa maana upendo wa Mungu umekwisha kumiminwa mioyoni mwetu na Roho Mtakatifu ambaye tulipewa”(Warumi 5:5). Kwa njia hiyo wote  tumepokea Roho yule yule, na huu ndio msingi wa safari yetu ya kiekumene. Kuna Roho anayetuongoza katika safari hii. Haya si mambo ya vitendo ili kuelewana vizuri zaidi. Hapana, kuna Roho; kuna Roho na lazima twende chini ya uongozi wa huyu Roho, Papa alishauri.

Miaka 1700 ya Mtaguso Mkuu wa Nikea

Na Mwaka huu wa Jubilei ya Matumaini, unaoadhimishwa na Kanisa Katoliki, unaenda sanjari na kumbukumbu ya muhimu sana  kwa Wakristo wote yaani ya mwaka wa 1700 wa Mtaguso mkuu wa kwanza wa Kiekumene, wa Nikea. Mtaguso huo ulijitolea kuhifadhi umoja wa Kanisa katika wakati mgumu sana na Mababa wa Mtaguso kwa kauli moja waliidhinisha kanuni ya Imani ambayo Wakristo wengi bado wanaisali leo hii  kila Dominika wakati wa maadhimisho ya Misa. Kanuni ya Imani hii ni kukiri kwa kawaida imani, ambayo inapita zaidi ya migawanyiko yote ambayo imejeruhi Mwili wa Kristo kwa karne nyingi. Maadhimisho ya Mtaguso wa Nikea kwa hiyo yanawakilisha mwaka wa neema, pia yanawakilisha fursa kwa Wakristo wote wanaokiri Imani moja na kumwamini Mungu mmoja: kwamba tuvumbue upya mizizi ya pamoja ya imani na tuhifadhi umoja! "Daima tusonge mbele! Umoja huo ambao sote tunautaka, kwamba hutokee. Je, hiyo ya Mtaalimungu  wa Kiorthodox, Zizioulas kama sikosei  aliyesema: "Ninajua wakati tarehe ya umoja kamili itakuwa: siku baada ya hukumu ya mwisho"? Lakini wakati huo huo ni lazima tutembee pamoja, tufanye kazi pamoja, tuombe pamoja, tupendane." Na hiyo ni nzuri sana," Papa aliongeza. Akiendelea alisisitiza kuwa  imani hii tunayoshiriki ni zawadi ya thamani, lakini pia ni changamoto. Maadhimisho hayo, kiukweli, hayapaswi kuadhimishwa kama "kumbukumbu ya kihistoria tu, hapana bali pia kama dhamira ya kushuhudia ushirika unaokua kati yetu. Ni lazima tuhakikishe haupotei, tujenge vifungo imara, tusitawishe urafiki wa pande zote, tuwe wafumaji wa ushirika na udugu.

Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuhamaisha Umoja wa Kikristo na Papa
Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuhamaisha Umoja wa Kikristo na Papa   (Vatican Media)

Juma la kuombea Umoja wa Kikristo 18-25 Januari

Katika Juma hili la Kuombea Umoja wa Kikristo tunaweza pia kupata uzoefu wa ukumbusho wa Baraza la Nikea kama wito wa kudumu katika njia ya kuelekea umoja. Kwa kawaida, mwaka huu, Pasaka itaadhimishwa siku hiyo hiyo katika kalenda ya Gregorian na Julian, hasa wakati wa ukumbusho huu wa kiekumene. Kwa njia hiyo Papa Francisko alisema “Ninarudia wito wangu kwamba tukio hili la pamoja linaweza kuwa ukumbusho kwa Wakristo wote kuchukua hatua madhubuti kuelekea umoja, ukaribu na tarehe ya pamoja, tarehe ya Pasaka (rej. Tamko la Spes non confundit, 17) na Kanisa Katoliki liko tayari kukubali tarehe ambayo kila mmoja anataka iwe tarehe ya umoja wa maadhimisho ya Pasaka.

Salamu kwa wageni mbali mbali waliofika

Papa aliendelea kumshukuru Polycarp, aliyewakilisha Upatriaki wa Kiekumene, Askofu Mkuu Ian Ernest, anayewakilisha Usharika wa Kianglikani na ambaye anahitimisha huduma yake adhimu ambapo amemshukuru sana pia na kumtakia kila la kheri atakaporudi katika ardhi yake, na pia kuwashukuru wawakilishi wa Makanisa mengine walioshiriki katika sadaka hiyo jioni ya masifu. Ni muhimu kusali pamoja, na uwepo wao  jioni hiyo kwamba “ ni chanzo cha furaha kwa wote. Papa alitoa  salamu kwa  wanafunzi wanaoungwa mkono na Kamati ya Ushirikiano wa Kiutamaduni na Makanisa ya Kiorthodox na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikristo, washiriki katika ziara ya mafunzo ya Taasisi ya Kiekumene ya Bossey ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni,(WCC)na wengine wengi, kama vile vikundi vya kiekumene na mahujaji waliofika Roma kwa ajili ya maadhimisho hayo. Papa hakusahau kuwashukuru Kwaya, ambao walifanikisha kusali vizuri.

Kwaya iliyoimba
Kwaya iliyoimba   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Je tunaamini kuwa Tumaini halikatishi tamaa?

Kwa kila mmoja kama Mtakatifu Paulo, Papa alisema kuwa: “apate tumaini letu katika Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili na kuwapelekea wengine, popote ambapo tumaini limetoweka, maisha yamevunjika au mioyo imezidiwa na dhiki (taz. Mahubiri ya Mkesha wa Noeli, Desemba 24, 2024). Katika Yesu, tumaini inawezekana kila wakati. Papa ameunga mkono tumaini la safari yetu ya pamoja kuelekea kwake na  swali aliloulizwa Martha na kuelekezwa kwetu jioni hiyo  limerejea kwamba: “ Je, tunaamini katika ushirika sisi kwa sisi? Je, tunaamini kwamba tumaini halikatishi tamaa? Huu ndio wakati wa kuthibitisha ungamo letu la imani kwa Mungu mmoja na kutafuta njia ya umoja katika Kristo Yesu. Tunapomngoja Bwana “arudi katika utukufu kwa kuwahukumu walio hai na waliokufa” (rej. Imani ya Nikea), tusichoke kamwe kutoa ushuhuda mbele ya watu wote, kwa ajili ya  Mwana wa pekee wa Mungu, chanzo cha matumaini yetu yote.

Papa na Umoja wa Kikristo
25 Januari 2025, 18:10