Papa azindua mwaka wa Mahakama ya Rota Romana
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu akukutana na wajumbe wa Mahakama ya Vatican Rota Roma katika uzinduzi wa mwaka wa Kimahakama, Ijumaa tarehe 31 Januari 2025 alisisitiza umuhimu wa kurahisisha michakato ya kubatilisha ndoa na kuzifanya zipatikane kwa urahisi zaidi huku akishikilia mafundisho ya Kanisa juu ya kuvunjika kwa ndoa. "Tunaitwa kwa uchungu na matumaini ya waamini wengi wanaotafuta ufafanuzi kuhusu ukweli wa hali yao binafsi na, hivyo basi, uwezekano wao wa kushiriki kikamilifu katika maisha ya kisakramenti," Utekelezaji wa mageuzi kwa hati mbili: Mitis Iudex Dominus Iesus na Mitis et Misericors Iesus. Mwaka huu ni kumbukumbu ya miaka kumi ya hati zake mbili binafsi za Moti Proprio: 'Mitis Iudex Dominus Iesus' na 'Mitis et Misericors Iesus', ambavyo vilirekebisha mchakato wa kubatilishwa ndoa, na kuwapa uwezo maaskofu wa Majimbo kufanya kazi kama majaji ili kubatilisha ndoa, na kuondoa hitaji la Mahakama ya Rota Romana kutia saini na sentensi yake mwenyewe. Hatua hiyo pia ilisukuma kufanya utaratibu wa kuwa huru zaidi.
Hatua za michakato ya mahakama baada ya Sinodi ya 2024
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake aliwakumbusha kwamba, “hatua yake hiyo imechangiwa na mijadala ya Mababa wa Sinodi wa Mwaka 2014, ambao walikazia hitaji la dharura la kuwepo kwa taratibu zaidi zinazoweza kufikiwa na kusawazishwa, huku wakiongozwa na mahangaiko ya kichungaji ili kuhakikisha kwamba, miundo ya Kanisa inabaki kuwa karibu na Kanisa, waamini na kuhudumia mahitaji yao ya kiroho ipasavyo. Kumpa askofu uwezo wa kutoa ubatilishaji kupitia mchakato mfupi zaidi (processus brevior) katika hali ambapo ubatili unadhihirika, Papa Francisko alieleza kuwa ni kielelezo cha kujali kwa Kanisa kwa ajili ya wokovu wa roho (salus animarum). Kadhalika Papa alibainisha kwamba mara nyingi waamini wengi hawajui uwezekano huu, Papa alisisitiza haja ya kuwafahamisha na akasisitiza tena kwamba taratibu zinapaswa kuwa za bure ili kuakisi upendo wa bure wa Kristo.
Kuwekeza malezi ya wafanyakazi
Papa Francisko pia alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kwamba mabaraza ya majimbo yana muundo mzuri, yakiwa na mapadre na watu wa kawaida waliofunzwa vya kutosha ili "waweze kufanya kazi yao kwa haki na bidii." Ubora wa malezi ya kiakili na kiroho kwa hiyo ni muhimu katika kuhakikisha kwamba waamini wanapata uchunguzi wa haki na makini wa kesi zao, alisema, huku akisisitiza kwamba mageuzi lazima yaendelee kuongozwa na kujali kwa wokovu wa roho kama ilivyoelezwa katika barua yake ya Motu Proprio ‘Mitis Iudex.’ Kuwekeza katika malezi ya wafanyakazi hawa, kisayansi, kibinadamu, na kiroho, huwanufaisha waamini, ambao wana haki ya kufikiria kwa uangalifu maombi yao, hata wanapopokea jibu lisilofaa, Papa alisititiza. Papa katika hotuba yake iliyoongoza na Mada kuu ya “usawa kati ya haki na usikivu wa kichungaji”alisisitiza kuwa Marekebisho hayo, hayakusudiwa kuongeza idadi ya ubatilishaji bali kuzuia mashaka ya muda mrefu ambayo yangeweza kuwaelemea waamini kulingana na mageuzi ya awali yaliyoanzishwa na Papa Mtakatifu Paulo VI mwaka 1975.
Kutumia busara haki na mapendo
Kwa kukomesha hitaji la kuzingatia hukumu maradufu, mageuzi ya 2015 yalilenga kuzuia utata wa kisheria usiohitajika kuzuia upatikanaji wa ukweli na haki. "Mageuzi hayalengi kuongeza ubatili wa ndoa bali kuharakisha michakato, kuhakikisha urahisi wa haki ili, kwa sababu ya kucheleweshwa kwa maamuzi, mioyo ya waumini inayongojea uwazi juu ya hali yao isikandamizwe kwa muda mrefu na giza la mashaka." Kwa hiyo, akionya dhidi ya hatari ya mtazamo wa kuegemea sheria kupita kiasi, Baba Mtakatifu Francisko, aliwataka majaji kutumia busara, haki, na mapendo, kuhakikisha kwamba kazi yao inakidhi mahitaji halisi ya watu badala ya kuwa zoezi la kisheria la kufikirika. "Kuna uhusiano wa karibu kati ya busara na haki, kwani zoezi la busara ‘iuris’ linalenga kujua ni nini kilicho katika kesi halisi," alisema Papa Francisko.
Kazi ya waamuzi katika kutambua uhalali wa ndoa, kwa hiyo, si tu wajibu wa kisheria bali ni huduma ya kichungaji kwa wokovu wa roho, kama inavyowawezesha waamini kujua na kukubali ukweli wa uhalisi wao binafsi hivyo kuchangia katika kuimarisha utamaduni wa kutotengana, unaothibitishwa na mafundisho ya Kanisa juu ya utakatifu wa ndoa. Baba Mtakatifu Francisko alihitimisha akiwahimiza wajumbe wa Mahakama ya Kipapa ya Rota Romana kuendelea katika utume wao, huku akiwakumbusha kwamba kazi yao ni ya matumaini katika kusaidia watu binafsi kujitakasa na kurejesha uhusiano kati ya watu.