Papa ataadhimisha Dominika ya Neno la Mungu katika Kanisa la Mtakatifu Petro Januari 26
Vatican News
Tarehe 26 Januari 2025 itakuwa ni Dominika ya VI ya Neno la Mungu, siku iliyoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako tarehe 30 Septemba 2019 ili kukumbusha umuhimu wa Maandiko Matakatifu. Kauli mbiu ya toleo hili imechukuliwa kutoka katika kufungucha Zaburi 119: "Natumaini neno lako". Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu anatarajia kuongoza Maadhimisho ya Misa Takatifu katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican saa 3:30 asubuhi, majira ya Ulaya. Mwishoni mwa liturujia atawapatia wale watakaohudhuria Injili ya Mtakatifu Luka, kulingana na mapokeo sasa kwa lengo la kueneza Neno la Mungu kwa njia inayoonekana.
Kusaidia waamini katika ukuaji wao wa kiroho
Wakati wa maadhimisho hayo Papa Francisko aidha anaratajia kuwapatia huduma ya Usomaji(Lector), kwa waamini walei arobaini, ambao ni wanaume na wanawake, kutoka mataifa mbalimbali: 4 kutoka Albania, 3 kutoka Argentina, 5 kutoka Austria, 1 kutoka Bolivia, 4 kutoka Brazil, 5 kutoka Ufilipino, 1 kutoka Iceland, 6 kutoka Italia, 5 kutoka Mexico, 1 kutoka Poland, 5 kutoka Slovenia. Kila mmoja wao, kulingana na ibada hiyo, atapewa nakala ya Biblia ya Nova Vulgata kwa jina kamili ni: Bibliorum Sacrorum Nova Vulgata Editio ambayo ina marekebisho ya sasa ya Vulgate, tafsiri ya Biblia katika Kilatini inayotazamwa kuwa rasmi na Kanisa Katoliki.
Ili kusaidia waamini katika ukuaji wao wa kiroho na katika kulikuza Neno la Mungu kwa kina, Kitengo cha Masuala Msingi ya Uinjilishaji katika Ulimwengu cha Baraza la Kipapa la Uinjilishaji limetoa mtandaoni, katika lugha sita, msaada wa bure wa kiliturujia-kichungaji, unaoweza kupakuliwa kutoka katika tovuti rasmi ya Baraza hilo ni: "evangelizatio.va". Hiki ni chombo kinachotoa mapendekezo ya kukuza kukutana kwa kina na Neno la Mungu katika jamii, katika familia, katika maisha ya kila siku, na pia inajumuisha makala, tafakari, maandiko ya Kuabudu na mapendekezo ya kichungaji.
Jinsi ya kuhudhuria Misa: chukua tiketi ya bure ya kuingilia
Dominika ya Neno la Mungu ambayo sasa iko katika toleo lake la sita, ni tukio muhimu kwa Wakristo kufanya upya ahadi yao ya kusoma na kutafakari Biblia, kama nyenzo msingi ya ukuaji wa imani na maisha ya kiroho na pia chombo cha matumaini kwa waamini kutoka sehemu zote za dunia. Tiketi za bure za kuhudhuria Misa Takatifu zinaweza kuchukuliwa katika eneo la maulizo ya Jubilei 2025(Infopoint of Jubilee 2025) iliyoko Njia ya Conciliazione n. 7, kuanzia Alhamisi, tarehe 23 Januari 2025. Tafadhali kumbuka kuwa tiketi ni chache kwa idadi, kwa hivyo uchukuaji utaruhusiwa hadi zitakapoisha.