Majadiliano ya Kiekumene Yakoleze Amani, Umoja Na Ushirika
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu na mbegu ya Ukristo sehemu mbalimbali za dunia. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 20 Januari 2025 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa kiekumene kutoka nchini Finland wanaohiji mjini Roma kama sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Henric, Msimamizi na Mwombezi wa Finland. Ujumbe wa kiekumene kutoka Finland umeongozwa na Askofu mkuu Elia wa Helsink wa Kanisa la Kiorthodox aliyechaguliwa hivi karibuni kuwa ni kiongozi mkuu wa Helsinki na Finland nzima. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amegusia kuhusu: Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu: “Mahujaji wa matumaini”, Umuhimu wa muziki mtakatifu na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1,700 ya Mtaguso wa Nicea na kwamba, Wakristo wanao wito wa kutangaza na kushuhudia umoja wa Wakristo.
Baba Mtakatifu Francisko ameushukuru ujumbe wa kiekumene kutoka Finland, unaofanya hija yao kama “Mahujaji wa matumaini” kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, huku wakihamasishwa kushika sana ungamo la tumaini lao, lisigeuke: maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu. Rej Ebr 10:23. Mtakatifu Enric, Msimamizi na Mwombezi wa Finland ni mjumbe na chombo cha amani, aliyekazia umuhimu wa kuombea amani duniani; ni kielelezo cha ushirika, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, maadhimisho ya sikukuu yake, yawe ni kikolezo cha umoja na ushirika wa Wakristo wote, ili kwa pamoja waweze kumtukuza Mwenyezi Mungu.
Muziki Mtakatifu ni chombo cha ibada na uinjilishaji; ni amana na utajiri wa Kanisa; dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa ibada, uchaji, unyenyekevu na unyoofu wa moyo! Hii inatokana na ukweli kwamba, nyimbo na muziki mtakatifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa zinawasaidia waamini kuzamisha Neno la Mungu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Muziki ni chombo cha imani, amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa! Muziki mtakatifu unasaidia sana maboresho na ushiriki wa waamini katika Liturujia na maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa, changamoto kwa wanakwaya ni kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha waamini wengine furaha ya Injili kwa njia ya muziki mtakatifu. Ikumbukwe kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayowakirimia waamini matumaini ya kuimba huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, hadi pale atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu amewapongeza wanakwaya wa “Cappella Sanctae Mariae” wanaolitukuza Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa njia ya nyimbo zao, huduma makini sana kwa watu wa Mungu.
Kanuni ya Imani ya Nicea ni kielelezo cha imani na ukweli ambao ni Kristo Yesu mwenyewe. Huu ni ukweli uliofanyika mwili. Ni Mungu kweli na mtu kweli, Bwana na Mkombozi wa Ulimwengu, anayepaswa kusikilizwa kwa moyo, ili hatimaye, msikilizaji aweze kuguswa na Fumbo la Mungu, linalosheheni upendo wa Kristo Yesu. Huu upendo aminifu unasimikwa katika matumaini ambayo kamwe hayawezi kudanganya kama ambavyo Mtakatifu Paulo Mtume anavyosimulia katika utenzi kwa upendo wa Mungu akisema, “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Rum 8:38-39. Baba Mtakatifu Francisko anasema kutangaza na kushuhudia upendo huu ni wito na wajibu wa kiekumene kwa wabatizwa wote.