杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Pietro Parolin kuwa mwakilishi wake katika kutabaruku Kanisa la Ubatizo wa Bwana nchini Yordani. Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Pietro Parolin kuwa mwakilishi wake katika kutabaruku Kanisa la Ubatizo wa Bwana nchini Yordani. 

Kutabarukiwa Kwa Kanisa la Ubatizo wa Bwana: Maana na Umuhimu Wake

Katika maadhimisho ya Kutabaruku Kanisa la Ubatizo wa Bwana, lililoko nchini Yordani, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinaliu Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican, kuwa ni mwakilishi wake katika Sherehe za Kutabaruku Kanisa la Ubatizo wa Bwana, Ijumaa tarehe 10 Januari 2025. Hapa ni mahali panaposadikiwa kwamba, ndipo Yohane Mbatizaji alimpombatizia Kristo Yesu. Yohane Mbatizaji katika maisha na utume wake, alitangaza na kushuhudia Ubatizo wa toba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kutabarukiwa kwa Kanisa maana yake ni kutenga Kanisa kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu ya Kanisa, kwa ajili ya sifa, utukufu na ukuu wa Mungu. Na ni katika mantiki hii, Kanisa linaitwa Nyumba ya Mungu, Makao ya watu wa Mungu, mahali ambapo watu wa Mungu wanakutanika kusali, kuabudu, kumtukuza, kumwomba na kumshukuru Mungu kwa wema, huruma na ukarimu wake wa daima. Hapa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anasubiri kukutana na waje wake, lakini inasikitisha kuona kwamba, kuna Kanisa lililojengwa vizuri na la kupendeza, lakini hakuna waamini wanaokwenda kusali ndani mwake. Hivyo basi, Liturujia inayoadhimishwa kila siku, iwajenge waamini waliomo katika Kanisa ili wawe ni Hekalu Takatifu la Bwana, Makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo Yesu. Maadhimisho ya Liturujia yawaimarishe waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya maisha adili na matakatifu. Rej. SC, 2. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwenda Kanisani ili kuchuma, neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kumbe, uwepo wa waamini Kanisani humo, itakuwa ni baraka na neema tosha kabisa. Ujenzi wa jengo kama Kanisa unakamilika kwa haraka, lakini inachukua muda mrefu kujenga na kuimarisha Jumuiya ya waamini, wenye tabia, ari na mielekeo tofauti. Kumbe, huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha Jumuiya ya waamini inayoimarishwa kwa Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume.”

Kutabarukiwa kwa Kanisa la Ubatizo wa Yesu nchini Yordani
Kutabarukiwa kwa Kanisa la Ubatizo wa Yesu nchini Yordani

Altare inaonesha: sadaka na meza ya Bwana. Mababa wa Kanisa wanasema, Altare ni alama ya Kristo mwenyewe aliye kati ya kusanyiko la waamini wake, papo hapo akiwa kafara inayotolewa kwa ajili ya upatanisho kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Altare ni sura ya mwili wa Kristo Yesu anasema Mtakatifu Ambrosi na kwamba, mwili wa Kristo uko juu ya Altare. Kumbe, Kanisa linafundisha kuhusu umoja kamili kati ya Sadaka na Altare. Altare hai ni Kristo Yesu mwenyewe, hivyo, wanapoiangalia Altare wamwone Kristo aliyejitoa sadaka Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Vivyo hivyo kama mwamini ni kiungo cha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, anapaswa kutambua kuwa yeye ni sehemu ya Altare ambacho kimsingi ni kielelezo makini cha Kristo Yesu katika hali yake yote. Ni Kristo Yesu: anayeganga na kuponya, anayesamehe na kutakasa; Kristo anayefundisha, kuonya na kuongoza. Ni katika maadhimisho ya Kutabaruku Kanisa la Ubatizo wa Bwana, lililoko nchini Yordani, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican, kuwa ni mwakilishi wake katika Sherehe za Kutabaruku Kanisa la Ubatizo wa Bwana, Ijumaa tarehe 10 Januari 2025. Hapa ni mahali panaposadikiwa kwamba, ndipo Yohane Mbatizaji alimpombatizia Kristo Yesu. Yohane Mbatizaji katika maisha na utume wake, alitangaza na kushuhudia Ubatizo wa toba na maondoleo ya dhambi. Akawataka watu kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu na hivyo, kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya, kama njia makini ya kuweza kumpokea Masiha wa Bwana, atakayetambulika kwa uwepo wa Roho Mtakatifu juu yake na huyu ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu. Wakati ulipotimia Yesu akajitokeza hadharani kando ya Mto Yordani, baada ya kukaa nyumbani kwao mjini Nazareti kwa muda wa miaka thelathini, ili aweze kubatizwa.

Kardinali Parolin, Mwakilishi wa Papa: Kutabaruku Kanisa la Ubatizo wa Bwana
Kardinali Parolin, Mwakilishi wa Papa: Kutabaruku Kanisa la Ubatizo wa Bwana   (Vatican Media)

Baada ya kubatizwa, Roho Mtakatifu akamshukia Yesu na mara sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”, alama ambayo Yohane Mbatizaji alikuwa akiisubiria na kwamba, Kristo Yesu ni Masiha wa Bwana. Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso, Balozi wa Vatican nchini Yordani anasema, Kanisa la Ubatizo wa Bwana, liliwekewa jiwe la msingi na Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI wakati wa hija yake ya kitume kunako mwaka 2009 na limejengwa kwa takribani miaka 15. Mtakatifu Yohane Paulo II na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko wote wametembelea eneo la Ubatizo wa Bwana. Kanisa hili linatabarukiwa wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo inayonogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini.” Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake ya uteuzi wa Kardinali Pietro Parolin, kuwa Mwakilishi wake, anasema, uwakilishi huu ni kielelezo cha upendo wake kwa watu wa Mungu nchini Yordani. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yawatie nguvu, ili waweze kumwiga Kristo Yesu kwa nguvu na bidii mpya; waoneshe upendo wa pekee kwa Kristo Yesu, Injili na Kanisa lake. Maadhimisho haya yawashe moto wa: imani, matumaini na mapendo thabiti kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu anamwomba Kardinali Pietro Parolin aweze kumfikishia salam na matashi mema kwa watu wa Mungu nchini Yordani. Anawahimiza wajenge utamaduni wa majadiliano ya kidini na kiekumene; wakuze na kudumisha uhuru wa kuabudu na kidini; amani na upendo wa dhati.

Kanisa la Ubatizo wa Bwana
08 Januari 2025, 14:35