杏MAP导航

Tafuta

Vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto wadogo ni suala zito la haki msingi za binadamu, jamii na afya ya jamii. Vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto wadogo ni suala zito la haki msingi za binadamu, jamii na afya ya jamii.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Katekesi Kuhusu: Dhuluma, Nyanyaso na Unyonyaji Wa Watoto Wadogo

Papa katika Kipindi cha Oktava ya Noeli, Jumatano tarehe 8 Januari 2025 amekita Katekesi yake juu ya Ukatili wa Watoto Wadogo hususan kazi za suluba wanazofanyishwa watoto wadogo. Vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto wadogo ni suala zito la haki msingi za binadamu, jamii na afya ya jamii. Vitendo hivi vinamomonyoa msingi imara ambao watoto wanahitaji ili wawe na afya bora na maisha yenye tija, na vinasigana na haki ya msingi ya watoto ya kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea na mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu.” Roho Mtakatifu ndiye aliyemwongoza Kristo Yesu jangwani na kwamba, Roho Mtakatifu ni mwenza wa waamini katika mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi. Mwenyezi Mungu ndiye aliyemtuma Kristo Yesu kwenda Jangwani na baada ya kushinda majaribu yote ya Shetani, Ibilisi “Yesu akarudi kwa nguvu za Roho Mtakatifu.” Lk 4:14. Kristo Yesu akarudi akiwa ni mshindi, tayari kuwakomboa wale wote wanaoteswa kwa nguvu za Shetani, Ibilisi, kielelezo cha uwepo wa Ufalme wa Mungu kati ya waja wake. Shetani, Ibilisi yupo na anaishi na kwamba, dunia imesheheni matendo ya Shetani, Ibilisi, licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Roho Mtakatifu amejidhihirisha katika matendo ya Mitume. Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, Roho Mtakatifu ni Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Katika Liturujia Roho Mtakatifu ndiye Mwalimu wa imani ya Taifa la Mungu na fundi wa kazi bora za Mungu ambazo ni Sakramenti za Agano Jipya. Tamaa na kazi ya Roho Mtakatifu katika moyo wa Kanisa ni hii kwamba waamini waweze kuishi kutokana na uzima wa Kristo Mfufuka. Kumbe, kwa njia ya Roho Mtakatifu liturujia huwa ni kazi ya wote, yaani ya Roho Mtakatifu na Kanisa. Rej KKK 1091- 1134. Kanisa limepambanua katika mwenendo wake wa karne, kwamba kati ya maadhimisho yake ya Kiliturujia, kadiri ya namna halisi ya neno, kuna Sakramenti saba zilizowekwa na Kristo Yesu. Kumbe, Roho Mtakatifu anatenda kazi katika Sakramenti ya Ndoa Takatifu. Kwa kweli kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara muungano wa Wabatizwa na Kanisa hufanywa kuwa mkamilifu zaidi, kwani wanatajirishwa kwa nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu na hivi hulazimika kwa nguvu zaidi kuineza na kuitetea imani kwa maneno na matendo, kama mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu. Rej. KKK 1285.

Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa uinjilishaji
Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa uinjilishaji

Karama na mapaji ya Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu. “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.” Gal 5:22-26. Habari Njema ya Wokovu inatangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya matendo adili na matakatifu na wala si wongofu wa shuruti kama alivyokaza kusema, Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI. Huu ndio ushuhuda wa furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa, lengo na hatima ya jicho la huruma na upendo kutoka kwa Kristo Yesu, kazi ambayo inaendelezwa kwa sasa na Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kristo Yesu Mfufuka aliwatuma wanafunzi wake akisema “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mt 28: 19-30. Uinjilishaji unatoa fursa kwa waamini kukutana na Kristo Yesu na hivyo kumfahamu na hatimaye: kumpenda na kumtumikia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Msalaba kwa Mitume wa Yesu, ulionekana kuwa ni hatima ya mambo yote, yaani kielelezo cha hali ya juu kabisa cha mateso, lakini Msalaba ukageuka kuwa ni chemchemi ya matumaini, huruma, upendo na msamaha. Msalaba ambao ulikuwa ni mti wa kifo, ukageuka kuwa ni mti wa uhai, chemchemi ya matumaini yanayoganga na kuponya magonjwa ya mwanadamu ambayo yanaendelea kulichafua na kulinajisi Kanisa la Kristo Yesu na Ulimwengu katika ujumla wake. Juu Msalabani, Mitume walimwona Yesu aliyesulubishwa, huku akiwa amevuliwa mavazi, Mungu katika unyenyekevu wake, anakuwa ni chemchemi ya wokovu, changamoto na mwaliko kwa waamini kusimamia na kuutangaza ukweli; sanjari na kuendelea kuwa ni vyombo vya huruma, upendo na upatanisho.

Uinjilishaji mpya unakita mizizi yake katika ushuhuda
Uinjilishaji mpya unakita mizizi yake katika ushuhuda   (Vatican Media)

Huu ni wakati wa kuvua na kutupilia mbali mambo yasiokuwa na msingi katika maisha, ili kutoa nafasi ya matumaini kuweza kuchipuka na kuchanua kama “mtende wa Lebanoni.” Baba Mtakatifu anasema, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, kuna mabadiliko makubwa, lakini, waamini wajifunze kujivika fadhila ya unyenyekevu na kujitahidi kuwa na kiasi na kamwe wasielemewe na tamaa za malimwengu kiasi cha kukosa furaha, amani na utulivu wa ndani. Ni vyema, kila mwamini akachunguza undani wa maisha yake na kuamua kung’oa na kutupilia mbali mambo ambayo si muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu alihitimisha katekesi yake kwa kuangalia kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Oktava ya Noeli, kwenye Katekesi yake Jumatano tarehe 8 Januari 2025 amekita Katekesi yake juu ya Ukatili wa Watoto Wadogo hususan kazi za suluba wanazofanyishwa watoto wadogo. Vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto wadogo ni suala zito la haki msingi za binadamu, jamii na afya ya jamii. Vitendo hivi vinamomonyoa msingi imara ambao watoto wanahitaji ili wawe na afya bora na maisha yenye tija, na vinasigana na haki ya msingi ya watoto ya kuishi salama utotoni. Tatizo la ukatili wa kijinsia, linaainisha aina zote za vitendo vya ukatili: kijinsia, kimwili na kiakili na sababu zake ni hatua muhimu kuelekea kwenye kubuni mikakati na sera za kitaifa na kimataifa zinazohusisha sekta mbalimbali, za kuzuia na kukabiliana na tatizo hili na kuwalinda watoto vizuri zaidi. Ulinzi wa utu na heshima ya binadamu ni dhamana na wajibu wa kisiasa na kijamii na Kanisa linatambua haki hizi msingi katika maisha na utume wake. Hizi ni haki ambazo zimebainishwa kwenye “Tamko la Haki ya Mtoto la Mwaka 1959” na kama haki hizi zinavyofafanuliwa kwenye Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuwawezesha watoto kukua na kukomaa katika mazingira salama katika maisha na utu wao.

Dhuluma na nyanyaso ni kinyume cha utu, heshima na haki msingi
Dhuluma na nyanyaso ni kinyume cha utu, heshima na haki msingi   (Copyright Marlon Lopez MMG1design. All rights reserved.)

Hawa ni watoto walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, walipewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Unyenyekevu wa watoto ni mfano bora wa kuigwa kwa wale wanaotaka kuingia kwenye Ufalme wa Mungu. Lakini, Kristo Yesu anaonya kwamba, Ole wake atakayemkwaza mtoto mdogo, itabidi afungiwe jiwe la kusagia shingoni na kuzamishwa baharini! Utumwa mamboleo ni mambo ambayo yanafumbatwa katika: Kazi za suluba, ukahaba, biashara ya binadamu na viungo vyake. Kuna masuala ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu wa magenge. Matendo yote haya ni uhalifu mkubwa dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu na yanapaswa kutambulika hivi na viongozi wa kidini, kisiasa na kijamii kama yanavyobainishwa na sheria za kitaifa na kimataifa bila kupindishwa pindishwa au kufumbiwa macho! Katekesi ya Baba Mtakatifu imeongozwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu isemayo: “Wakamletea na watoto wachanga ili awaguse; lakini wanafunzi walipoona waliwakemea. Bali Yesu akawaita waje kwake, akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa kuwa watu kama hao ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambia, Mtu ye yote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hauingii kamwe.” Lk 18:15-17. Licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia; karne inayokita maendeleo yake makubwa katika teknolojia ya akili mnemba lakini bado kuna watoto wanaodhulumiwa na kunyanyaswa utu, heshima na haki zake msingi; watoto wananyonywa, wanahumizwa na hatimaye wengine wanapoteza maisha. Neno la Mungu linatoa kipaumbele cha pekee kwa watoto wanaozaliwa, kwani hawa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu, licha ya kuwa ni chemchemi ya furaha, watoto kwa upande mwingine wamekuwa ni chanzo cha kinzani na migogoro sanjari na kilio. “Ulimi wa mtoto anyonyaye Wagandamana na kinywa chake kwa kiu; Watoto wachanga waomba chakula, Wala hakuna hata mmoja awamegeaye.” Omb 4: 4. Maandiko Matakatifu yanaonesha nyanyaso na ukatili mkubwa waliofanyiwa watoto wadogo.

Watoto wanafanyishwa kazi ngumu na hivyo jupokwa matumaini yao.
Watoto wanafanyishwa kazi ngumu na hivyo jupokwa matumaini yao.   (ANSA)

Hata leo hii Baba Mtakatifu anasema, kuna watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanaoteseka na kupoteza maisha kutokana na baa la njaa, magonjwa na ujinga; ni watoto wanaofariki dunia kutokana na mashambulio ya makombora. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwenye utawala wa Mfalme Herode aliyetishia maisha ya Mtoto Yesu kiasi cha wazazi wake kukimbilia Misri, kama inavyojidhihirisha hata leo hii, watu kukimbia nchi zao kwajili ya kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Rej Mt 2: 13-18. Baada ya kupita ile dhoruba kali, iliyopelekea watoto wa Bethlehemu kuuwawa kwa ukatili wa Mfalme Herode, Bikira Maria pamoja na Mtakatifu Yosefu walirejea na kwenda kuishi Nazareti, mji ambayo haukutajwa kwenye Agano la Kale. Kristo Yesu akajifunza kazi kutoka kwa Mtakatifu Yosefu. Rej Mk 6:3; Mt 13:55. “Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.” Lk 2: 40. Kristo Yesu katika maisha na utume wake alitoa fursa kubwa kwa watoto, ili aweze kuwabariki na kuwaombea, kiasi cha kubadili mila na desturi zilizokuwa hapo akisema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao.” Lk 18: 16-17. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani na kwamba, “Bali atakae mkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia na kutoswa katika kilindi cha bahari. Mt 18: 6.

Watu wasimame kidete kulinda na kupinga nyanyaso dhidi ya watoto
Watu wasimame kidete kulinda na kupinga nyanyaso dhidi ya watoto   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi kusimama kidete kuwalinda na kuwaendeleza watoto; wasimame imara kukemea nyanyaso na dhuluma dhidi ya watoto wadogo. Hata leo hii kuna watoto wanaofanyishwa kazi za suluba, kiasi kwamba, hawana ndoto tena, wala nafasi ya kufurahia maisha; sehemu mbalimbali za dunia kuna watoto wanaonyonywa, kiasi cha kufutilia mbali matumaini na mapendo, lakini ikumbukwe kwamba, watoto wanao upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu, kumbe, mtu yeyote anayemtendea mtoto kinyume cha maadili na utu wema, anawajibika mbele ya Mungu. Kwa wale wote wanaomtambua Kristo Yesu, Neno wa Mungu wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu; kwa kuwapenda, kuwalinda na kuwatunza watoto, ili kamwe wajanja wachache katika jamii wasithubutu kuwapoka utoto wao, ndoto za maisha yao na hivyo kunyanyaswa na kudhulumiwa. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia moyo wa huduma na mapendo, ili hatimaye, kila mtoto sehemu mbalimbali za dunia aweze kukua, kuendelea katika hekima na kimo, huku akimpendeza Mungu na wanadamu. Rej Lk 2: 52.

Venite Adoremus Dominum
Venite Adoremus Dominum   (Vatican Media)

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kwenda mjini Bethlehemu kumwabudu Mtoto Yesu “Venite Adoremus Dominum.” Wajitahidi kujenga utamaduni wa upendo unaosimikwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Huu ni wito wa kudumu katika maisha ya waamini, kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kutetea Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Waamini washiriki kikamilifu katika hija ya imani, matumaini na mapendo, katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Uwe kweli ni mwaka wa toba na wongofu wa ndani, kwa kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha. Mama Kanisa anawaalika watoto wake baada ya kumwabaudu Mtoto Yesu aliyelazwa pangoni na kushuhudia utukufu wake, wawe na ujasiri wa kutafakari mwanga wa Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Waamini waendelee kutunza ndani mwao, ile furaha ya Noeli kwa sala, tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama njia mahususi ya kukutana na Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Baba Mtakatifu Francisko amempongeza Kardinali Mauro Gambetti, O.F.M. Conv., Makamu Askofu kwa mji wa Roma, aliyepewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 8 Januari 2000, katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo. Baba Mtakatifu amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia.

Unyanyasaji wa Watoto
08 Januari 2025, 15:02