杏MAP导航

Tafuta

Mkutano wa Mwaka wa Jukwaa la Kiuchumi Ulimwenguni 2025 huko Davos. Mkutano wa Mwaka wa Jukwaa la Kiuchumi Ulimwenguni 2025 huko Davos.  (ANSA)

Davos,Papa:AI,isivunje hadhi ya binadamu kwa sababu ya kutaka ufanisi!

Katika Ujumbe wa Papa Francis kwa Washiriki wa Jukwaa la Kiuchumi Duniani kuanzia Januari 20-24 anasema:Maendeleo ya kiteknolojia ambayo hayaboreshi maisha ya watu wote lakini badala yake yanaunda au kuongeza ukosefu wa usawa na migogoro,hayawezi kufafanuliwa kama maendeleo ya kweli.Serikali na makampuni yanapaswa kutumia bidii na umakini ili Akili Mnemba ikuze manufaa ya wote,haki na udugu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko alituma ujumbe wake kwa Washiriki wa Jukwaa la Kiuchumi la Dunia huko Davos, katika tukio la kila mwaka linalowaleta pamoja wajumbe elfu tatu kutoka ulimwengu wa kisiasa na kifedha katika mji wa Uswiss.  Jukwaa hilo linaongozwa na mada kwa mwaka huu 2025: "Ushirikiano wa Enzi ya Akili  kuanzia tarehe 20 hadi 24 Januari 2025. Katika Ujumbe huo Papa anabainisha kuwa “Kauli mbiu ya jukwaa la Uchumi Duniani,  mwaka huu "inatoa fursa nzuri ya kutafakari Juu ya Akili Mnemba kama chombo si tu cha ushirikiano bali pia kuleta watu pamoja. Mapokeo ya Kikristo yanachukulia kipawa cha akili kama kipengele muhimu cha mwanadamu aliyeumbwa “kwa mfano wa Mungu.” Wakati huo huo, Kanisa Katoliki daima limekuwa mhusika mkuu na mfuasi wa maendeleo ya sayansi, teknolojia, sanaa na aina nyinginezo za jitihada za binadamu, likizingatia kuwa ni maeneo ya “ushirikiano wa mwanamume na mwanamke na Mungu katika ukamilifu wa uumbaji unaoonekana”(Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 378).

AI inafunzwa matokeo ya ubunifu wa binadamu

Akili Mnemba (AI) imekusudiwa kuiga akili ya binadamu iliyoiunda, hivyo basi kuibua maswali na changamoto mbalimbali. Tofauti na uvumbuzi mwingine mwingi wa binadamu, AI inafunzwa juu ya matokeo ya ubunifu wa binadamu, ambayo huiwezesha kuzalisha kazi za sanaa mpya zenye kiwango cha ujuzi na kasi ambayo mara nyingi hushindana au kuzidi uwezo wa binadamu, na kuibua wasiwasi mkubwa kuhusu athari zake kwa jukumu la binadamu duniani. Papa aidha anasisitiza kuwa “Zaidi ya hayo, matokeo ambayo AI inaweza kutoa karibu hayawezi kutofautishwa na yale ya wanadamu na hivyo kuzua maswali kuhusu athari yake kwenye mgogoro unaoongezeka wa ukweli katika jukwaa la umma. Vile vile, teknolojia hii imeundwa kujifunza na kufanya chaguo fulani kwa uhuru, kukabiliana na hali mpya na kutoa majibu ambayo hayakutarajiwa na watayarishaji wake, na hivyo kuibua maswali ya kimsingi kuhusu uwajibikaji wa kimaadili, usalama wa binadamu, na athari pana za maendeleo haya kwa jamii.

Binadamu ana uwezo wa kuchagua na kuamua.AI si akili bali ni bidhaa ya binadamu  

Papa Francisko anakazia kueleza kuwa ingawa AI ni mafanikio ya ajabu ya kiteknolojia yenye uwezo wa kuiga matokeo fulani yanayohusiana na akili ya binadamu, teknolojia hii "hufanya chaguo la kiufundi kati ya uwezekano kadhaa kulingana na vigezo vilivyobainishwa vyema au juu ya makisio ya takwimu.  Wanadamu, hata hivyo, sio tu kuchagua, lakini mioyoni mwao wana uwezo wa kuamua: Kwa hakika, matumizi yenyewe ya neno "akili" kuhusiana na Akili Mnemba (AI) ni jina potofu, kwani AI sio aina ya akili ya mwanadamu bali ni bidhaa yake. Inapotumiwa kwa usahihi, AI humsaidia mwanadamu katika kutimiza wito wake, katika uhuru na wajibu.

AI iwe sehemu za jitihada za kufikia haki kuu,udugu na utaratibu wa kibinadamu 

Baba Mtakatifu kadhalili amesisitiza kuwa kama ilivyo kwa shughuli nyingine zote za binadamu na maendeleo ya kiteknolojia, AI lazima iamriwe kwa binadamu na iwe sehemu ya jitihada za kufikia "haki kuu, udugu mpana zaidi na utaratibu wa kibinadamu zaidi wa mahusiano ya kijamii", ambayo ni "thamani zaidi kuliko maendeleo katika nyanja ya kiufundi” (Gaudium et Spes, 35; taz. Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 2293). Hata hivyo, Papa Francisko anabinisha kuwa “kuna hatari kwamba AI itatumiwa kuendeleza "mtazamo wa kiteknolojia", ambao huona matatizo yote ya ulimwengu kuwa yanaweza kutatuliwa kupitia njia za kiteknolojia pekee. Ndani ya dhana hii, hadhi na udugu wa binadamu mara nyingi huwekwa chini katika kutafuta ufanisi, kana kwamba ukweli na wema hutoka katika nguvu za kiteknolojia na kiuchumi.

Maendeleo yasiyojali binadamu na usawa hayawezi kuitwa maendeleo

Hata hivyo hadhi ya binadamu kamwe isivunjwe kwa ajili ya ufanisi. Maendeleo ya kiteknolojia ambayo hayaboreshi maisha kwa kila mtu, lakini badala yake yanaunda au kuzidisha ukosefu wa usawa na migogoro, hayawezi kuitwa maendeleo ya kweli. Kwa sababu hiyo, AI inapaswa kuwekwa katika huduma ya afya bora, zaidi ya binadamu, zaidi ya kijamii na muhimu zaidi maendeleo. Maendeleo yaliyoainishwa na mapambazuko ya AI yanataka ugunduzi upya wa umuhimu wa jumuiya na kujitolea upya kutunza nyumba ya wote tuliyokabidhiwa na Mungu.

Ili kukabiliana na ugumu wa AI Serikali na biashara ziwe makini

Ili kukabiliana na ugumu wa AI, serikali na kampuni lazima zitumie bidii na umakini. Ni lazima watathmini kwa kina matumizi ya mtu binafsi ya AI katika miktadha fulani ili kubaini kama matumizi yake yanakuza utu wa binadamu, wito wa binadamu na manufaa ya wote. Kama ilivyo kwa teknolojia nyingi, athari za matumizi Akili Mnemba (AI) haziwezi kutabirika kila wakati tangu kuanzishwa kwake. Kadiri utumiaji wa AI na athari zake za kijamii zinavyozidi kuwa wazi, kwa kadiri muda unavyopita, majibu yanayofaa yanapaswa kufanywa katika ngazi zote za jamii, kulingana na kanuni ya usaidizi, na watumiaji binafsi, familia, mashirika ya kiraia, mashirika, taasisi, serikali na mashirika ya kimataifa, kufanya kazi katika viwango vyao vinavyofaa ili kuhakikisha kuwa AI inaelekezwa kwa manufaa ya wote.

Changamoto na fursa za AI

Baba Mtakatifu hatimaye amebainisha kuwa leo hii kuna changamoto na fursa muhimu wakati AI inawekwa ndani ya mfumo wa akili ya uhusiano, ambapo kila mtu anashiriki jukumu la ustawi muhimu wa wengine. Kwa hisia hizi, Papa alitoa matashi yake na maombi  kwa ajili ya mijadala ya Jukwaa na kwa wote wanaoshiriki kwa hiari yake  aliwaombea  baraka nyingi kutoka kwa Mungu.

Ujumbe wa Papa kwa washiriki wa Jukwaa huko DAVOS
23 Januari 2025, 16:43