Chuo Kikuu cha Kipapa Cha Capranica: Mashuhuda wa Imani Kwa Kristo na Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Pallium yaani “Pallia Takatifu” ni vazi la kiliturujia linalovaliwa na Mapatriaki pamoja na Maaskofu wakuu wakati wa Ibada kwenye eneo la majimbo yao makuu mintarafu Sheria za Kanisa za Mwaka 1983. Pallia takatifu hutokana na sufu safi iliyokatwa kutoka kwa kondoo waliobarikiwa wakati wa Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, Bikira na Shahidi inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Januari. “Agnes” maana yake kwa lugha ya Kiswahili ni “Mwanakondoo.” Mtakatifu Agnes, Bikira na shahidi, aliuwawa kunako karne ya tatu; akaonesha upendo wa pekee sana kwa Kristo Yesu mchumba wake wa daima, kiasi cha kuyasadaka maisha yake, ili asiuchafue ubikira wake. Mtakatifu Agnes pia ni msimamizi na mwombezi wa Chuo kikuu cha Kipapa cha Capranica, kilichoko mjini Roma. Sikukuu hi kwa mwaka huu inabeba uzito wa hali ya juu kwani Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Mahujaji wa matumaini.” Maadhimisho ya Juma la 58 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2025 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, yananogeshwa na kauli mbiu “Je, unayasadiki hayo?” Yn 11:26 Tafakari ya Mwaka huu inajikita zaidi katika Kanuni ya Imani ya Nicea, ambayo kwa Mwaka 2025, Kanisa linaadhimisha kumbukizi ya Miaka 1700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipofanyika kunako mwaka 325. Kunako mwaka 2019 Baba Mtakatifu Francisko alipitisha Katiba ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Capranica, mwongozo unaowasaidia wanachuo kukua na hatimaye, kukomaa katika uhuru katika uaminifu, kwa kuwajibika ndani ya Kanisa kwa watu ambao wamedhaminishwa kwao.
Hii ni Jumuiya inayosimikwa katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, huku ikiwa na shauku na ari ya kuitikia wito kutoka kwa Kristo Yesu. Hiki ni chuo kinachowasaidia majandokasisi kujiandaa kwa ajili ya kupokea Daraja Takatifu ya Upadre au kuboresha malezi na majiundo yao mwanzoni kabisa katika maisha na utume wa Kipadre. Hiki ni Chuo kinachopokea wanafunzi kutoka katika majimbo 39, kati yake kuna majimbo ishirini na sita kutoka nchini Italia, hali inayoonesha ile taswira ya watu wa Mungu. Hiki ni Chuo kinachotoa na kulinda uhai si tu katika maisha ya kitawa bali katika medani mbalimbali za maisha. Kumbe, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanajenga na kukuza mahusiano yatakayowawezesha kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukaribu wa Mungu kwa watu wake, ukaribu kwa Maaskofu wao na Ukaribu kwa Mapadre. Mapadre hawa wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, kwa kuendelea kulijenga Kanisa la Kisinodi linalojikita katika upyaisho wa maisha ya kiroho; katika miundo mbinu ya Kanisa, ili kuwawezesha watu wa Mungu kuwa na ushiriki mkamilifu na wa kimisionari, tayari kutoa mwanga angavu wa Kristo Yesu.
Baba Mtakatifu anawataka Mapadre hawa kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni sehemu muhimu sana ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi hasa wanapotekeleza dhamana na utume wao ndani ya Chuo hiki cha Kipapa, kwenye vyuo mbalimbali wanakosoma, katika Gereza kuu la Rebibbia, kwenye Hospitali ya Watoto ya “Bambin Gesù” bila kusahau sehemu mbalimbali wanazohudumia kama sehemu ya uzoefu na mang’amuzi yao ya kichungaji na kama sehemu ya majiundo yao. Hiki ni Chuo kinachotoa huduma ya Kiliturujia katika Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu na wakati mwingine katika maadhimisho yanayofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kielelezo cha ukaribu wao kwa watu wa Mungu. Kumbe, Liturujia ya Kikristo lazima ishuhudiwe katika maisha ya imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huduma ya upendo ni sehemu ya vinasaba vya Chuo hiki cha Kipapa, kwa kusaidiana na kushirikiana na kwamba, inawasaidia kudumu katika huduma, bila ya kupoteza lengo la maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wote waliohudhuria mkutano huu na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Afya ya Warumi pamoja na ya Mtakatifu Agnes Bikira na Shahidi.