Papa Francisko: Mkristo anapigana na shetani ambaye anataka kuharibu kila kitu
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Jumamosi jioni tarehe 7 Oktoba 2023 ikiwa Mama Kanisa anakumbuka Bikira Maria wa Rozari, Baba Mtakatifu Francisko aliongoza Ibada ya Misa Takatifu mjini Vatican kwa ajili ya Kikosi cha Ulinzi wa Mji wa Vatican, katika Uwanja wa Groto ya Lourdes iliyoko kwenye bustani ya Vatican. Kikundi hili cha Ulinzi wa mji wa Vatican kilikuwa kinamkumbuka Somo wao, Mtakatifu Mikaeli Malaika Mkuu iliyoaadhimishwa tarehe 29 Septemba iliyopita.
Katika mahubiri, Papa Fransisko alilinganisha kazi ya askari na shamba la mizabibu ambalo adui, kama ilivyoelezwa katika somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Isaya (Isa 5:1-7), kulingana na liturujia ya Dominika ya XXVII ya kawaida, wakati, giza linaingia ili kuharibu kile kilichopandwa huko. Shamba la mizabibu pia ni picha ya maisha ya kila mtu ambapo wema na uovu hupambana kati yao, Papa Francisko alisema. Bwana ametupanda sisi sote, kana kwamba tulikuwa matawi ya shamba zuri la mizabibu, lakini adui huja kutuharibu daima. Haya ni mapambano ya kila siku: yako na yangu na sisi sote. Mtu ambaye hajisumbui si Mkristo, asiyepata majaribu si Mkristo.
Kwa hiyo Papa alisema lazima tulinde shamba la mizabibu la kila mmoja wetu. Sisi sote, Papa aliendelea, ni wadhambi, lakini tunataka kusonga mbele na kwa hiyo tunapaswa kupambana na shetani ambaye anataka kuingia katika maisha yetu. Papa akikimbusha kwamba Malaika Mkuu Mikaeli husaidia katika vita hivyo alihimiza kuwa: Lazima tuwe makini na kulinda shamba la mizabibu: shamba la mizabibu la kila mmoja wenu, shamba la mizabibu la familia zenu, la watoto wenu na shamba la mizabibu, hapa, mko Vatican, ili pasiwepo matawi mabaya ya kuingia.
Katika Kifungu cha Injili ya Mathayo (Mt 21:33-43) ambacho kinatoa mfano wa wakulima walioamua kumiliki kile ambacho walikabidhiwa, Papa alisema kinatuambia kwamba shetani anapotaka kumiliki kitu anakiharibu. Vita ambayo inataka kuharibu kila kitu ni vita chafu, na kwamba shetani anajaribu kushinda kwa kuharibu. Lakini Mtakatifu Mikaeli hutusaidia kumfukuza.