Papa Francisko Anawataka Waamini Kuwa ni Manabii wa Haki na Amani Duniani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ilikuwa ni tarehe 27 Julai 1953, miaka 70 iliyopita, Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini zilipotiliana saini mkataba wa kusitisha vita na hivyo kuanza mchakato wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa, ingawa bado kumekuwepo na mgogoro kati ya nchi hizi mbili. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Askofu Matthias Ri Iong-hoon, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Korea na kusomwa wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Myeong-dong, Jimbo kuu la Seoul, Korea ya Kusini na Kardinali Lazarus You Heung-sik, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makleri anasema, leo hii kuna vita, kinzani na migogoro mingi inayowatesa wanadamu sehemu mbalimbali za dunia. Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: haki na amani; kuendeleza ushirikiano, urafiki na udugu wa kibinadamu kati ya watu na katika jumuiya ya binadamu. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa anawaalika watu wa Mungu nchini Korea kuwa ni manabii wa amani inayopata chimbuko lake katika heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kujali mahali wala historia ya watu; huu ni mwaliko wa kulinda na kudumisha sheria, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, bila kusahau kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu kuitunza na kuiendeleza, kama urithi na utajiri wa kimaadili unaopaswa kurithishwa kwa vijana wa kizazi kipya.
Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia watu wa Mungu Korea, kuhusu uwepo wake kiroho. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu nchini Korea, kuhakikisha kwamba, Maadhimisho ya miaka 70 tangu Korea ya Kusini na Kaskazini watiliane saini Mkataba wa kusitisha vita, iwe ni fursa adhimu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Ni Ufalme unaosheheni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu. Rum 14:17. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kumbukizi ya Mkataba huu si tu kusitisha vita, kinzani na mipasuko, bali uwe ni dira na mwongozo unaoangaza mambo yajayo yaani: Upatanisho, udugu wa kibinadamu; amani na utulivu si tu kwa Korea bali pia sehemu mbalimbali za dunia.
Wakati huo huo, Prof. Dr Jerry Pillay, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, anasema, Wakristo wanaitwa na kualikwa kuwa ni vyombo na mashuhuda haki, amani na upatanisho, dhidi ya nguvu zinazowapelekea watu wengi kwenye mipasuko, kinzani na hatimaye vita. Anapenda kulipongeza Baraza la Makanisha ya Kikristo nchini Korea “National Council of Churches of Korea” ambalo kwa takribani miaka 40 limekuwa mstari wa mbele kunogesha mchakato wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa. Kuna wakati ambapo kinzani zinapanda na wakati mwingine muktadha wa masuala ya kisiasa hautoi nafasi kwa ajili ya amani, hapo ndipo mchango wa Baraza la Makanisa Korea linapaswa kujitokeza hadharani kulinda, kutetea na kudumisha haki na amani. Huu ni wakati wa kukomesha vita na kuanza kujielekeza katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano. Ni wakati wa kupunguza kinzani na kuanza kujielekeza katika mchakato wa wa ujenzi wa mazingira yatakayosaidia kunogesha majadiliano katika ukweli na uwazi. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., linahitimisha ujumbe wake kwa kusema kwamba, huu ni wakati wa ujenzi wa mshikamanano na udugu wa kibinadamu, kwa kuendelea kuchuchumilia ujenzi wa amani: Vikazo na changamoto wanazokumbana nazo njiani zisiwakatishe tamaa, bali ziwe ni ngazi ya kuwasaidia kujizatiti katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu Korea. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., litaendelea kushirikiana na kushikamana na watu wa Mungu katika hija ya haki, upatanisho, umoja na amani.