Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni: Imani na Matumaini Kwa Vijana
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 6 Agosti 2023 anashiriki katika Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni inayonogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Hii ni hija yake ya 42 ya Kitume Kimataifa na mwendelezo wa tema kuhusu dhamana na utume wa Bikira Maria katika maisha ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea Lisbon nchini Ureno tarehe 2 Agosti 2023 amemtumia salam na matashi mema, Rais Sergio Mattarella wa Italia akimwelezea furaha yake katika kushiriki Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni. Hii ni fursa kubwa kwa vijana wa kizazi kipya kuboresha imani na matumaini yao. Aliondoka akaenda kwa haraka, hii ni nguvu ya kuweza kukutana na Kristo Yes una hivyo kutiwa moyo katika kutafuta ukweli na maana ya maisha. Baba Mtakatifu anapenda kumshirikisha Rais Sergio Mattarella tumaini sanjari na kuwapatia baraka zake za kitume watu wa Mungu nchini Italia huku akiwaombea amani, ustawi na mafanikio.
Kwa upande wake, Rais Sergio Mattarella wa Italia anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa moyo wake wote wakati huu anaposhiriki katika Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni. Hii ni fursa ya kuweza kukutana na umati mkubwa wa vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia; vijana wanaoshuhudia urafiki wa udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika imani na matumaini ya ujenzi wa Ulimwengu fungamani unaosimikwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu.
Wakati huo huo, habari kutoka Lisbon, Ureno zinasema kwamba, Rais Marcelo Rebelo de Sousa, katika muktadha wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, ametangaza msamaha kwa vijana wanaotumikia adhabu yao magerezani, msamaha utakaoanza kutumika tarehe 1 Septemba 2023. Hawa ni vijana ambao wamejuta makosa yao wakaonesha moyo wa toba wakati wakitumikia vifungo vyao magerezani.