Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni 2023: Bikira Maria wa Fatima, Ureno
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya mitandao ya kijamii, anawaalika vijana kabla ya kuanza safari ya kushiriki maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno au katika nchi zao, kufanya tendo la huruma kwa kuwatembelea wazee wanaoishi peke yao. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, sala na maombi ya wazee yatawalinda na kuwajalia kubeba nyoyoni mwao baraka za wazee! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yanafunguliwa rasmi kwa Ibada ya Misa takatifu tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Mwenyezi Mungu kwa njia ya mahusiano na mafungamano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, wanatambua kwamba, wameitwa kukuza na kudumisha kumbukumbu na kutambua uzuri wa kuwa ni sehemu ya historia kubwa zaidi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, urafiki na wazee unaweza kuwasaidia vijana kuona maisha yao si tu kwamba, ni jambo la mpito na kwamba, si kila kitu kinawategemea wao na uwezo wao. Kwa wazee, uwepo wa kijana katika maisha yao unaweza kuwapa matumaini kwamba, uzoefu wao hautapotea na kwamba, ndoto zao zinaweza kupata utimilifu katika maisha ya vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 30 Julai 2023 amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumsindikiza katika Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, fursa ya vijana kukutana na Kristo Yesu pamoja na ndugu zao katika Kristo, huku wakiongozwa na Bikira Maria ambaye baada ya kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu aliondoka akaenda kwa haraka. Bikira Maria ni nyota angavu ya safari ya Kikristo anayeheshimiwa sana nchini Ureno! Baba Mtakatifu amewakabidhi mahujaji wa Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni pamoja na vijana wenyewe chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 Agosti 2023 anashiriki katika maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni. Hii ni hija yake ya 42 ya Kitume Kimataifa na mwendelezo wa tema kuhusu dhamana na utume wa Bikira Maria katika maisha ya Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2019 huko Panama, kuanzia tarehe 22 – 27 Januari 2019, yalinogeshwa na kauli mbiu “Mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kama ulivyonena” Lk. 1:38. Baba Mtakatifu katika hija hii anapania Jumamosi tarehe 5 Agosti 2023 kutembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, nchini Ureno. Ataongoza Ibada ya Rozari Takatifu kwa vijana wagonjwa. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 13 Mei anaadhimisha kumbukumbu ya Bikira Maria wa Fatima. Hii ni kumbukumbu ya Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima: Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos, tarehe 13 Mei 1917 na kujitambulisha kuwa ni Bikira Maria wa Rozari Takatifu, kwa kuwakabidhi watoto hawa ujumbe wa matumaini kwa binadamu wote, akiwataka wajizatiti katika kupambana na ubaya, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unaweza kufupishwa kwa maneno makuu matatu: Sala, Toba na Wongofu wa ndani! Sala ni majadiliano ya kina kati ya mwamini na Muumba wake; majadiliano yanayomwongoza mwamini kuelekea katika maisha ya uzima wa milele. Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kuwa na mwelekeo mpya katika maisha yao. Bikira Maria wa Fatima anawaalika waamini kuchuchumilia utakatifu na kuendelea kusali kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani; kwa kujiweka wakfu kwa Moyo wake usiokuwa na doa!
Bikira Maria anawaalika waamini kusali Rozari Takatifu ili kuombea amani duniani! Hii ni chngamoto endelevu hata kwa watu wanaoishi katika ulimwengu mamboleo! Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unafumbatwa kwa kiasi kikubwa katika Injili, kiasi kwamba, Fatima inakuwa ni shule ya imani na ushuhuda wa maisha ya Kikristo, na Bikira Maria ndiye Mwalimu wake mkuu! Bikira Maria anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na imani kwa Kristo Yesu na kamwe wasikatishwe tamaa na: Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia; majanga katika maisha ya watu; tawala za kifashisti na kikomunisti, tawala ambazo zimedhalilisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu; kiasi hata cha kutaka kumng’oa Mungu katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu. Kilio cha waamini kilikuwa ni kumwomba Mwenyezi Mungu asimame mwenyewe na kujitetea! Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ulijikita zaidi katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na Vita Kuu ya Pili ya Dunia; vita ambavyo vimesababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu sehemu mbalimbali za dunia. Siri zote za Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima zikafunuliwa hadharani kunako Mwaka 2000 kwa kuonesha madhara makubwa yaliyosababishwa na Urusi kwa wakati ule kwa kupandikiza “ndago” za Ukanimungu; dhuluma, nyanyaso na mauaji ya kikatili dhidi ya Wakristo! Katika kipindi hiki cha utawala wa giza na chuki dhidi ya imani ya Kikristo, hapa kukaibuka makundi ya Wakristo waliosimama imara kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Jeuri ya maisha yao ya kiroho! Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako tarehe 13 Mei 1981 akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican akapigwa risasi katika jaribio la kutaka kumuua na kumfutilia mbali kutoka katika historia na uso wa dunia! Lakini akasalimika na kwamba, huu ni muujiza wa pekee kabisa aliotendewa na Bikira Maria wa Fatima. Mtakatifu Yohane Paulo II akaamuru hata ile Siri ya Tatu ya Fatima iwekwe hadharani! Ni siri ambayo ilionesha kwamba kulikuwa na mapambano makali dhidi ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II akachukua risasi iliyotoka mwilini mwake na kuiweka kwenye taji ya nyota kumi na mbili zinazopamba kichwa cha Bikira Maria wa Fatima.
Tarehe 25 Machi 1984 Mtakatifu Yohane Paulo II akauweka ulimwengu na kwa namna ya pekee kabisa, Urussi chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria. Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ni endelevu hata kwa watu wa nyakati hizi kwani unafumbatwa katika Injili ya Kristo na Kanisa lake; Unahimiza Ibada kwa Bikira Maria, Toba, Wongofu wa ndani, Utakatifu wa maisha na umuhimu wa kusali Rozari Takatifu ili kuombea amani duniani. Waamini watambue daima kwamba, hata katika shida na mahangaiko yao, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahali! Bikira Maria anataka kuwaachia watoto wake, ujumbe wa matumaini, wokovu, amani na kwamba, Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha ya mwanadamu! Takwimu zinaonesha kwamba, kuna vijana zaidi ya 330, 000 kutoka katika nchi zaidi ya mia mbili waliojiandikisha tayari kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni Jimbo kuu la Lisbon nchini Ureno kwa mwaka 2023. Siku mbili za mwisho, yaani mkesha na Dominika tarehe 6 Agosti 2023 idadi ya vijana inaweza kugota milioni moja na ushee. Baba Mtakatifu katika kipindi chote hiki cha maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, katika hotuba zake atajikita katika katekesi ya kina inayochambua tema muhimu za maisha na utume wa ujana ndani ya Kanisa na katika jamii katika ujumla wake: Ndoto na matumaini ya vijana wa kizazi kipya; matatizo, changamoto na fursa mbalimbali katika malezi na makuzi yao. “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39 ni kauli mbiu itakayochambuliwa na Makardinali 20 wakisaidiana na Maaskofu 700 wanaoshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni. Baba Mtakatifu anatarajia kutoa hotuba na mahubiri tisa.