Hija ya Kitume ya Papa Francisko Hungaria: Imani na Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya Kitume ya 34 ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Hungaria tarehe 12 Septemba 2021, ilikuwa ni kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) yaliyozinduliwa na Kardinali Angelo Bagnasco, Jumapili tarehe 5 Septemba 2021 huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Baba Mtakatifu amekubali mwaliko ulitolewa na Serikali pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Hungaria, HCBC, kutembelea nchini mwao kuanzia tarehe 28 Hadi 30 Aprili 2023. Akiwa nchini Hungaria, Baba Mtakatifu atazungumza na viongozi wa serikali, vyama vya kiraia na wanadiplomasia. Atakutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa, Watawa, Waseminaristi na Wafanyakazi katika Idara ya Kichungaji. Baba Mtakatifu atapata nafasi pia ya kutembelea Kituo cha Watoto cha Mwenyeheri Laszlo Batthyan-Strattmann. Kama kawaida yake, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na maskini, wakimbizi na wahamiaji. Atakutana na vijana wa kizazi kipya na hatimaye, atakuwa na mazungumzo ya faragha na Wayesuit wanaoishi na kufanya utume wao nchini Hungaria. Dominika, tarehe 30 Aprili 2023 Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kossuth Lajos. Baadayae jioni atakutana na wasomi pamoja na ulimwengu wa wasanii na kuzungumza nao, na hatimaye, ataagana na watu wa Mungu nchini Hungaria a hatimaye kurejea tena mjini Vatican kuendelea na utume wake.
Baba Mtakatifu Francisko, Dominika 23 Aprili 2023 mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, aliwakumbusha waamini kwamba Ijumaa tarehe 28 hadi Dominika tarehe 30 Aprili 2023 atafanya hija ya kitume ya siku tatu nchini Hungaria, hii ikiwa ni mwendelezo wa hija yake ya Kitume ya Mwaka 2021. Hii ni fursa ya kukutana na kuzungumza na watu wa Mungu nchini Hungaria. Hii ni hija inayofanyika Kati kati ya Bara la Ulaya, ambako bado kuna vuma upepo wa vita kati ya Urusi na Ukraine bila kusahau changamoto ya wimbi kubwa na wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anasema anakwenda kati yao kama hujaji, rafiki na ndugu yao na anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sala na sadaka zao. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu katika mahubiri Ibada ya Misa takatifu ya kufunga Kongamano la Ekaristi alikazia umuhimu wa wafuasi wa Kristo Yesu kupyaisha maisha yao kwa kufuata hatua kuu tatu: Kumtangaza Kristo Yesu; Kufanya mang’amuzi ya kina pamoja naye na kutembea nyuma yake kwa kumtambua Kristo wa kweli, ili hatimaye waweze kukiri kwa imani thabiti kwamba, “Wewe ndiwe Kristo. Kwa namna ya pekee kabisa wafuasi wa Kristo Yesu wanapaswa kupyaisha maisha na utume wao wanapokiri imani yao kwa Kristo Yesu, ikiwa imekamilika barabara yaani kwa kutambua Ubinadamu na Umungu wake unaofumbatwa katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Huu ni utambulisho pia unaojionesha kwenye Fumbo la Ekaristi Takatifu na kwamba, utume wa Kristo Yesu unakamilika kwa Fumbo la Pasaka. Na hii ndiyo katekesi iliyofuata baada ya kiri ya imani ya Mtakatifu Petro, Mtume!
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Msalaba wa Kristo Yesu utakuwa ni chemchemi ya matumaini mapya kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Hungaria kwa sasa na kwa siku za usoni. Msalaba wa Kristo uwe ni chachu ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Msalaba wa Utume ndicho kilichokuwa kielelezo cha Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa. Msalaba wa Kristo uwe ni nguvu ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayobubujika upendo wa Kristo usiokuwa na mipaka kwa watu wote. Upendo huu ukate na kuzima kiu ya watu wote wasiopendwa duniani. Katika hotuba yake iliyokuwa inabubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, amegusia kuhusu ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Maaskofu wanapaswa kuwa ni watangazaji wa Injili. Wawe ni mashuhuda wa udugu wa kibinadamu na wajenzi wa Injili ya matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo! Baba Mtakatifu anasema, Ekaristi Takatifu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Kanisa nchini Hungaria limejengeka juu ya ushuhuda wa waungama na wafiadini. Hawa ndio wale waliosagwa kama “ngano”, ili kuwashirikisha jirani zao upendo wa Mungu. Ni watu waliopondwa na kugeuka kuwa ni “divai” chemchemi ya maisha mapya, tayari kujenga historia ya watu wa Mungu nchini Hungaria. Injili ya upendo ni kielelezo muhimu sana cha ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Kwa kutunza mizizi ya historia ya Kanisa, Maaskofu wawe na ujasiri wa kuangalia mbele kwa matumaini, kwa kuibua mbinu mpya za kutangaza na kushuhudia Injili. Baba Mtakatifu anasema, anayo kumbukumbu endelevu ya Watawa wa Shirika la Yesu, waliolazimika kuikimbia nchi yao kutokana na madhulumu. Lakini kutokana na uaminifu kwa wito wao, wakaanzisha makao mapya nchini Argentina. Baba Mtakatifu anasema amejifunza mengi kutoka kwa watawa hawa!
Na kwa njia yao, Baba Mtakatifu amewakumbuka watu wote ambao wamelazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na madhulumu na nyanyaso mbalimbali. Mapokeo ya Kanisa ni mto wa maisha mapya unaobubujika kutoka katika asili, yaani Kristo Yesu hadi kulifikia Kanisa kwa wakati huu, na hivyo kushirikishwa historia ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 12 Septemba 2021 baada ya kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Hungaria alipata nafasi ya kukutana na viongozi wawakilishi wa Baraza la Makanisa nchini Hungaria pamoja na baadhi ya viongozi wa Jumuiya za Kiyahudi nchini Hungaria. Baba Mtakatifu katika hotuba yake alikazia zaidi pamoja na mambo mengine kuhusu: Umoja wa wafuasi wa Kristo Yesu kujikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa kubomoa kuta za utengano na kuanza mchakato wa ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu na kuwaimarisha kwa pamoja. Mambo mengine ni kuhusu: Agano, dhuluma pamoja na umuhimu wa kuwa na mizizi inayorutubisha kumbukumbu hai! Baba Mtakatifu aliwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Baraza la Makanisa nchini Hungaria kwa kujenga na kudumisha uekumene wa sala na ushirikiano kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza maisha mapya yanayosimikwa katika umoja na udugu wa kibinadamu na wala si uhasama, ili kujenga umoja na mshikamano kama ilivyokuwa kwa Waisraeli kule Jangwani.