Papa Francisko Akutana na Wahanga wa Vita DRC: Asikiliza Shuhuda Zao! Msamaha
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya 40 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 3 Februari 2023 inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Baba Mtakatifu baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Ndege wa “Ndolo” Jimbo kuu la Kinshasa, jioni alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wahanga wa vita na machafuko ya kisiasa kutoka eneo la Mashariki wa DRC, ambako Baba Mtakatifu Francisko alitamani kwenda ili kujionea mwenyewe maafa yaliyoko huko, lakini kutokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wake, amesikiliza shuhuda za wahanga hawa kwenye Ubalozi wa Vatican nchini DRC. Hawa ni wawakilishi kutoka Bunia, Beni-Butembo, Goma, Masisi, Rutshuru, Bukavu na Uvira, ambayo mara chache sana wanaweza kusikika kwenye vyombo vya mawasiliano Kimataifa. Hawa ni waathirika wa watu wenye nguvu wanaotumia silaha kali kupandikiza utamaduni wa kifo. DRC haitaweza kamwe kupata amani ya kudumu, hadi maeneo ya Mashariki wa DRC yamekuwa na amani. Baba Mtakatifu katika hotuba yake ameonesha ukaribu wake kwa waathirika, amelaani vita, mauaji ya kinyama, ubakaji, uchomaji wa vijiji, uporaji wa mazao na mifugo. Vita imesababisha uvunjwaji wa haki msingi za binadamu, mafungamano ya kijamii na kiuchumi na hivyo kuacha madonda ambayo ni vigumu kuweza kuponyeka. Yote haya ni matokeo ya biashara haramu ya silaha duniani.
Baba Mtakatifu amewaonya wale wote wanaojitajirisha kwa damu ya maskini kuacha mara moja vitendo hivi. Huu ni mwaliko wa kuachana na vita na mizizi yake ambayo ni: uchoyo, husuda na tabia ya kutaka kulipiza kisasi, ili amani ya kweli iweze kuchipua na kuzamisha mizizi yake katika nyoyo za watu. Huu si wakati wa kukata wala kukatishwa tamaa, bali wajifunze kujenga udugu wa kibinadamu kwani jirani mwema ni ndugu, tayari kujikita katika mchakato wa upatanisho na hivyo kuanza maisha mapya yanayosimikwa katika matumaini, tayari kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani. Baba Mtakatifu Francisko amewambia wahanga wa vita na vurugu nchini DRC kwamba, uwepo wake miongoni mwao ni kutaka kuwaonesha ukaribu wake na kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anathamini utu, heshima na haki zao msingi na kwamba, hata katika magumu yao, bado Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwakumbuka, kumbe, hata binadamu nao wanao wajibu wa kuwakumbuka! Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kulaani vikali vita, mauaji ya kinyama, ubakaji, uchomaji na uvamizi wa vijiji; wizi wa mazao mashambani na mifugo, unyonyaji wa amana, utajiri na rasilimali ya DRC pamoja na kishawishi cha kuigawa DRC ili iweze kutawaliwa kwa urahisi.
Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Mwenyezi Mungu msamaha, faraja na hatimaye, awaongoe wauaji na kuwapatia watu ujasiri wa kuona vitendo hivi viovu! Vita nchini DRC imesababisha wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, uvunjwaji wa haki msingi za binadamu pamoja na mahusiano na mafungamano ya kijamii na kiuchumi na hivyo kusababisha madonda makubwa ambayo si rahisi kuponyeka kiasi cha kupandikiza chuki ya kikabila. Haya yote ni matokeo ya udhaifu wa mifumo ya kitaasisi na matokeo yake, baadhi ya mashirika ya Kimataifa yanatumia mwanya huu kujichotea kwa urahisi malighafi na hivyo biashara haramu ya silaha kuendelea kushamiri. Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu amewataka wale wote wanaohusika na vitendo hivi kuacha mara moja, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia na kuendelea kujitajirisha kwa damu ya maskini. Huu ni wakati wa kukataa vita na wale wote wanaotaka kupandikiza utamaduni wa kifo kwa jina la Mwenyezi Mungu, ambaye kimsingi ni Mungu wa amani na wala si Mungu wa vita. Umefika wakati wa kuondokana na mahubiri ya chuki, uhasama na uchochezi na matokeo yake ni mauaji. Huu ni wakati wa kung’oa kabisa mizizi ya vita inayotokana na uchu wa mali na madaraka; wivu na tabia ya kutaka kulipizana kisasi, ili kuanza mchakato wa msamaha na uponyaji wa kweli unaomweka mtu huru na hivyo kumkirimia amani na utulivu wa ndani.
Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu nchini DRC kutokatishwa wala kujikatia tamaa ya maisha, bali kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa DRC inayosimikwa katika amani, upendo na mshikamano na hivyo kuondokana na magomvi ya kikabila kati ya Watutsi na Wahutu na kwamba, amani Mashariki wa DRC inawezekana kwa kujenga urafiki na ujirani mwema kwani jirani mwema ni ndugu, iwe ametoka Burundi, Rwanda au Uganda. Huu ni wakati wa kujikita katika upatanisho, kuwa na ujasiri wa kutafuta na kuambata amani; kwa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Msalaba wa Kristo Yesu uwe ni nguvu kwa wale wote wanaohitaji amani. Msalaba ni kielelezo cha upendo na upatanisho, kiasi kwamba, umekuwa ni mti wa maisha ya uzima wa milele. Wananchi wa DRC wawe ni mti wa uhai kwa kutenda mema, kwa kuishi upendo na hivyo kudumisha umoja na upatanisho; haki na msamaha kwa kuondokana na tabia ya kutaka kulipiza kisasi, tayari kuanza kutembea katika njia mpya inayosimikwa katika matumaini, uvumilivu na udumifu. Baba Mtakatifu anawapongeza wale wote ambao wanaendelea kupandikiza mbegu ya amani nchini DRC, wanaotamani kuona utu, heshima na haki msingi za binadamu zikilindwa na kuheshimiwa. Baba Mtakatifu amewakumbuka wale wote waliopoteza maisha yao kwa ajili kulinda na kudumisha amani kwa kumtaja Balozi Luca Attanasio, Vittorio Iacovacci na Mustapha Milambo Baguma waliouwa kikatili tarehe 22 Februari 2021. Hawa wamepandikiza mbegu ya amani na kamwe sadaka yao haitasahaulika. Baba Mtakatifu anawataka wananchi wa DRC kuwa ni watu wa upatanisho na matumaini.
Wawakilishi kutoka Bunia, Beni-Butembo, Goma, Masisi, Rutshuru, Bukavu na Uvira wametoa ushuhuda wa mateso na mahangaiko yao kutokana na vita, sasa wanataka DRC iwe ni nchi ya amani, furaha, upendo na amani; mahali ambapo watu wake wanapendana na kuishi kama ndugu wamoja. Wasichana na wanawake, wameshuhudia jinsi ambavyo walinyanyaswa na kudhulumiwa kijinsia, kiasi cha kushika mimba na hatimaye, kujifungua watoto mapacha. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, kuna vikosi vya wanamgambo wanaoendelea kupandikiza mbegu ya kifo, kiasi kwamba, kuna watoto wengi ambao wamebaki yatima, wengine wamepelekwa mstari mbele kama chambo cha vita na wasichana na wanawake wanaendelea kubakwa, hali inayodhalilisha utu, heshima na haki zao msingi. Wengi wao, wameliona Kanisa kama mahali pa faraja na kimbilio lao kwa ajili ya kupata msaada. Kanisa nchini DRC limekuwa ni msaada mkubwa kwa wahanga wa vita nchini DRC. Wamewaombea msamaha na kumwomba Mwenyezi Mungu awafundishe watu kuheshimu zawadi ya maisha ya binadamu. Wahanga hawa wanasema, wameshuhudia ukatili wa kinyama dhidi ya watu wa Mungu nchini DRC.
Mauaji na ukatili huo umepelekea madhara makubwa: kimwili, kiroho, kimaadili na kiutu. Wanamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia amani na utulivu ili waendelee kutekeleza dhamana na wajibu wao katika ujenzi wa DRC mpya. Wamesimulia jinsi ambavyo vikosi vya askari walivyowavamia na kuanza kupora mali, chakula na mifugo. Waliwateka wakiwa vijana na kuwafanyisha kazi za suluba kwenye kambi zao za kijeshi. Tarehe 17 hadi tarehe 20 Aprili 2020, mafuriko yalipelekea watu 60 kufariki dunia katika eneo la Uvira kwa kufukiwa na kifusi. Watu 45 walijeruhiwa vibaya, nyumba 3500 ziliharibiwa na familia 7, 700 zilikosa makazi, tangu wakati huo mji wa Uvira umekuwa kama makaburi, ukahaba umeongezeka kiasi cha kutisha. Kutokana na vita katika maeneo ya Fizi, Mwenga, Itombwe na Uvira, zaidi ya watu 346, 000 hawana makazi ya kudumu, na wengi wao wamefariki dunia kwa kukosa huduma muhimu. Wahanga hawa wanasema, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kati yao umeacha alama ya kudumu, zawadi ya upendo, sasa wanao ujasiri wa kuanza kuandika historia ya maisha yao, wanamwomba Mwenyezi Mungu awakirimie haki na amani, ili kweli DRC iweze kuwa ni nchi inayosimikwa katika: maridhiano, amani na udugu wa kibinadamu.