Hija ya Kitume Ya Papa Francisko Nchini DRC: 2-5 Julai 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amepokea na kukubali mwaliko wa viongozi wa Serikali na Kanisa na ametia nia ya kutembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, mjini Kinshasa na Goma kuanzia tarehe 2-5 Julai 2022. Hija hii ya kitume inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Kamati ya Maandalizi ya Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC Kitaifa imepokea kwa mikono miwili nia ya Baba Mtakatifu kutembelea nchini mwao. Nembo ya hija hii inaonesha ile kiu ya watu wa Mungu kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko anayekwenda kuwaimarisha ndugu zake katika mchakato wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa.
Itakuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu Francisko ya kukutana na ndugu zake kutoka DRC ambao wameteseka na kumwaga damu kwa miaka mingi kutokana na utajiri, amana na rasilimali za DRC ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa ni chanzo cha vita, kinzani na migogoro nchini DRC. Wananchi wa DRC kwa sasa wanayo kiu kubwa ya amani ambalo ni jina jingine la ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Familia ya Mungu nchini DRC ina ibada kubwa kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa. Bikira Maria amekuwa ni kimbilio la watu wa Mungu katika shida na mahangaiko yao mbalimbali. Daima wamekuwa wakimwomba, ili awafikishie sala na kilio chao kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, anayewatia nguvu ya kusonga mbele, licha ya matatizo na changamoto za maisha wanazokabiliana nazo.
Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC imejenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kama zawadi kubwa inayopaswa kumwilishwa katika vipaumbele vya maisha ya wananchi wa DRC. Kwa hakika, watu wa Mungu nchini DRC wanataka kumpokea Baba Mtakatifu Francisko kwa kishindo kikuu, huku wakionesha umoja na ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha yao ya Kikristo. Hija hii ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha fura ya watu wa Mungu nchini DRC. Huu ni mwaliko wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.