Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki:Misa ya Papa Nikosia
Na Sr. Angella Rwezaula – Vatican.
Ijumaa tarehe 3 Desemba 2021 ikiwa ni siku ya Pili ya Papa Francisko huko Cyprus, ameongoza misa Takatifu katika uwanja wa mpir wa miguu wa Nicosia. Katika mahubiri yake kwa waamini Baba Mtakatifu Francisko amejikita kufafanua sehemu ya Injili ya Marko ambayo ilikuwa ni somo la siku kuhusu Yesu alipokuwa akipita, na kukutana na vipofu wawili ambao walipaza sauti: " Yesu Mwana wa Daudi Utuhurumie". Papa amebainisha kuwa watu hao wawili ni vipofu, lakini wanatambua kwamba Yesu ndiye Masiha aliyekuja ulimwenguni. Kwa maana hiyo Watu hao wanaweza kutusaidia, katika kipindi hiki cha majilio, kumkaribisha Bwana atakapokuja. Video fupi na picha vinaonesha matukio mazuri ya Misa takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu.
Papa akiendelea na mahubiri hayo ameshauri watu wa Mungu wa Cyprus kufuata hatua tatu ili kuachilia mbali giza ambalo mara nyingi tunajikuta nalo. Hatua ya kwanza ni kwamba watu wawili hao walikwenda kwa Yesu kwa ajili ya uponyaji. Ingawa hawakuwa na uwezo wa kumwona, lakini walisikia sauti yake na kufuata nyayo zake. Watu wawili katika Injili walimwamini Yesu na hivyo wakamfuata katika kutafuta mwanga kwa macho yao. Papa amebainisha kuwa wawili hao walimwamini Yesu kwa sababu walitambua kwamba, ndani ya giza la historia, yeye ndiye nuru inayoangaza usiku wa moyo na ulimwengu. Pamesema kwamba sisi pia tuna aina fulani ya upofu mioyoni mwetu na kama wale vipofu wawili mara nyingi wamezama katika giza la maisha na mara nyingi sisi wenyewe tungependelea kubaki tukiwa tumejifungia wenyewe, peke yetu gizani, tukijihurumia na kuridhika kuwa na huzuni, lakini badala yake lazima twende kwa Yesu na tumpatie Yesu nafasi ya kuponya mioyo yetu.
Hatua ya pili ambayo Papa ameifafanua ni kwamba wote wawili walikuwa ni walishiriki wa maumivu yao. Wote wawili waliomba msaada kwa pamoja. Hii ni ishara fasaha ya maisha ya Kikristo na sifa bainifu ya roho ya kikanisa, tendo la kufikiri, kusema na kutenda kama sisi, kukataa ubinafsi na hisia ya kujitosheleza ambayo huambukiza moyo,amesisitiza Papa.
Hatua ya tatu na ya mwisho, Papa amebainisha kwamba wao walitangaza Habari Njema kwa furaha. Baada ya Yesu kuwaponya vipofu hao wawili, walianza kueneza habari njema katika eneo lote. Kuna kejeli kidogo katika hili, amebainisha Papa. Yesu alikuwa amewaambia wasimwambie mtu yeyote atakayetokea, lakini walifanya kinyume kabisa. Nia yao haikuwa kumwasi Bwana lakini. Hii ni kutokana na kwamba hawakuweza tu kuzuia msisimko wao katika uponywaji wao na furaha ya kukutana kwao na Yesu. Hiyo ndiyo ishara nyingine ya kipekee ya Mkristo, Papa Francisko amesisitiza.