杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Cyprus amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Sinodi Takatifu ya Kanisa la Kiorthodox nchini Cyprus. Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Cyprus amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Sinodi Takatifu ya Kanisa la Kiorthodox nchini Cyprus. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Sinodi Takatifu

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wajumbe wa Sinodi Takatifu ameelezea asili moja ya kitume na umuhimu wa waamini kukutana mara kwa mara, dhamana na utume wa Mtakatifu Barnaba, Mtume na kwamba, utume wa Kanisa unapitia sadaka na majaribio mbalimbali kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Barnaba, Mtume. Ushuhuda, Ushirika na Mapokeo ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus kuanzia tarehe 2-4 Desemba 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Tufarijiane Katika Imani”. Haya ni maneno yanayotokana na jina na Mtume Barnaba, maana yake Mwana wa Faraja! Rej. Mdo 4: 36. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 3 Desemba 2021 ameianza siku kwa kumtembelea Askofu mkuu Chrysostomos II, wa Kanisa la Kiorthodox la Cyprus na kumzawadia Nyaraka za Mtume Paulo “Codex Pauli, Acta Epistolae Apocrypha” zenye kurasa 424, kilichotunzwa kwa takribani miaka elfu moja iliyopita. Baba Mtakatifu amesema kwamba, zawadi hii ni alama ushirika wa watoto wa Mama Kanisa. Baadaye, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Sinodi Takatifu ya Kanisa la Kiorthodox nchini Cyprus.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wajumbe wa Sinodi Takatifu ameelezea asili moja ya kitume na umuhimu wa waamini kukutana mara kwa mara, dhamana na utume wa Mtakatifu Barnaba, Mtume na kwamba, utume wa Kanisa unapitia sadaka na majaribio mbalimbali kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Barnaba, Mtume. Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi na waamini wote wa Kanisa la Kiorthodox nchini Cyprus, ambao kwa njia ya sala na sadaka yao wanasaidia kutakasa na kuiinua imani. Uwepo wao katika fursa hii ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus ni kielelezo cha neema inayowawezesha kutambua asili ya utume wao unaopata chimbuko lake kwa Paulo Mtume aliyetoka Kisiwani hapo hadi mjini Roma; wote ni warithi wa Biblia Takatifu na wote wanasafiri kuelekea kwenye udugu na umoja kamili.

Katika safari hii Wakristo wanaongozwa na maisha ya Mtakatifu Barnaba, Mtume. Barnaba, maana yake “Mwana wa Faraja au “Mwana wa Mawaidha” Ni yule Mtume aliyekuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa Mitume! Rej. Mdo 4: 36. Faraja na wosia ni maneno mawili yanayoweza kutumika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kuwaongoza na kuwaelekeza katika uhuru na wema kwa kuzamisha mizizi kwa faraja ya uwepo wa Mwenyezi Mungu, huku ikisindikizwa na upendo wa kidugu. Lengo ni kuendeleza utume wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, kwa kuzingatia utamadunisho na bidii ya watu wa Mungu kukutana binafsi na Kristo Yesu. Kama watoto wa faraja wanapaswa kwanza kabisa kujenga utamaduni wa kusikiliza, ili kujenga mawasiliano yatakayo kuza ushirika. Hii ndiyo dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anawapongeza viongozi wa Kanisa la Kiorthodox kwa kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya kiekumene na hivyo kuwa ni wajumbe hai wa Tume ya Pamoja ya Taalimungu Kimataifa kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, tume hii itaweza kukutana mara kwa mara, na kuendelea kuwa wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu mintarafu mang’amuzi yao ya kiimani. Wakristo wajitahidi kushirikiana katika mateso na faraja, kwa sababu kwanza kabisa wao wamefarijiwa katika dhiki zao zote ili nao wapate kuwa ni faraja kwa wale walio katika dhiki za namna zote kwa faraja hizo hizo wanazofarijiwa na Mungu. Rej. 2 Kor 1: 3-5 Kanisa Katoliki litaendelea kuwa ni chombo cha faraja kwa wenye shida na mahangaiko mbalimbali, kumbe ni wajibu wa Wakristo wote kusali na kuombeana.

Wakristo wa Kanisa la Mwanzo walikuwa na roho moja na vitu vyao waliviweka kwa ushirika. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinasimulia haya na kukaza kusema “Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro, alikuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa Mitume.” Mdo 4:36-37. Hiki ni kielelezo cha ushirika na utume mambo msingi yanayohimizwa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, kama fursa ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha ya waamini. Kuna haja kwa waamini wa Makanisa haya mawili kujipatanisha mintarafu tunu msingi za Kiinjili kwa kukikita zaidi katika Mapokeo ya Kanisa kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Barnaba Mtume, aliyeacha yote ili kujenga na kudumisha ushirika nguzo ya kwanza ya upendo unaozima kiu ya ujenzi wa umoja!

Baba Mtakatifu anawataka Wakristo wa Makanisa haya mawili kujielekeza zaidi katika kufuata nyayo za Mtakatifu Barnaba, Mtume kwa kujitahidi kujenga ujirani mwema, ili kuvuka vikwazo vya utengano kwa kuendelea kujikita katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika uvumilivu na udumifu mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; huduma ya elimu sanjari na kusimama kidete kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili hatimaye udugu na ushirika vitakuwa na kukomaa kama alama ya sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu. Makanisa yaendelee kuhifadhi desturi na utambulisho wake, lakini yajielekeze katika mchakato wa maridhiano, ili hatimaye, yaweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, lakini zaidi ushirika wa kitume!

Baba Mtakatifu Franciko anasema, Kanisa la “Panaghia Chryssopolitissa” yaani “Kanisa la Bikira Maria wa Mji wa Dhahabu” ni maarufu sana kwa maadhimisho ya Sakramenti ya Ndoa Takatifu, linaweza kuwa ni alama ushirika wa imani na neema chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Hapa ni mahali ambapo Wakristo wanapakumbuka sana kwani Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa alipata bakora 30 baada ya kukutwa na hatia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu huko Paphos. Baba Mtakatifu anakaza kusema, utume wa Kanisa unajikita katika sadaka na kupitia katika majaribu mengi kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Barnaba Mtume. Katika maisha na utume wake alikutana na mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu alishindana nao na kutaka kumtia Liwali moyo wa kuiacha ile imani.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa hotuba yake anasema, hata leo Mama Kanisa anakabiliana na changamoto ya utengano miongoni mwa watoto wake. Kumbe, kuna haja ya kujikita katika majadiliano ya kiekumene ili kujenga na kuimarisha umoja, utakatifu na upendo wa Kanisa linalojikita katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Cyprus ni nchi ambayo imebarikiwa kuwa na watakatifu, waungama na mashuhuda wengi wa imani. Baadhi yao wanafahamika zaidi, hawa ni Barnaba na Paulo Mitume, Marko na Epiphanius bila kusahau umati mkubwa wa Jeshi la watakatifu mbinguni waliojenga daraja la kuwakutananisha watu Mashariki na Magharibi. Hawa ni wale waliounganisha mbingu na dunia. Sifa na utukufu viwe kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwa wema wa Kanisa na watu wote katika ujumla wao.

Sinodi Takatifu
03 Desemba 2021, 16:03