杏MAP导航

Tafuta

Papa Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Cyprus amegusia kuhusu mchango wa Cyprus katika mchakato mzima wa uinjilishaji, utamadunisho na madaraja ya kuwakutanisha watu. Papa Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Cyprus amegusia kuhusu mchango wa Cyprus katika mchakato mzima wa uinjilishaji, utamadunisho na madaraja ya kuwakutanisha watu. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus Na Ugiriki: Nafasi ya Cyprus Kimataifa

Papa amekazia: Heri za Mlimani, Utamadunisho, Cyprus na changamoto zake; umuhimu wa kudumisha majadiliano ili kuweza kupata amani ya kudumu inayosimikwa katika msingi wa upatanisho na umoja. Cyprus inaweza kuonekana kama ni nchi ndogo lakini ni umuhimu katika mchakato wa ukuaji wa utamaduni Barani Ulaya na ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus kuanzia tarehe 2-4 Desemba 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Tufarijiane Katika Imani”. Haya ni maneno yanayotokana na jina na Mtume Barnaba, maana yake Mwana wa Faraja! Rej. Mdo 4: 36. Baba Mtakatifu katika hija hii ya kitume anapenda kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kufarijiana katika imani, kama sehemu ya nyenzo muhimu katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano, ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu sanjari na ukarimu; amali za watu wa Mungu nchini Cyprus. Baba Mtakatifu Francisko,  Alhamisi tarehe 2 Desemba 2021 amehitimisha siku yake ya kwanza nchini Cyprus kwa kukutana na kuzungumza kwa faragha na Rais Nikos Anastasiadīs wa Cyprus na baadaye akazungumza na viongozi wa Serikali na vyama vya kiraia pamoja na wanadiplomasia.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi hawa amekazia Heri za Mlimani, Utamadunisho wa Injili, Cyprus na changamoto zake; umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi ili kuweza kupata amani ya kudumu inayosimikwa katika msingi wa upatanisho na umoja. Baba Mtakatifu anasema, Cyprus inaweza kuonekana kama ni nchi ndogo katika ramani ya dunia, lakini ni nchi ambayo ina umuhimu wa pekee katika mchakato wa ukuaji wa utamaduni Barani Ulaya na ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu katika msingi wa ukarimu. Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake na Askofu mkuu Makarios alibahatika kuwa ni Rais wa kwanza wa Cyprus. Kiongozi aliyekirimiwa na Mwenyezi Mungu heri na baraka katika maisha. Lakini heri maskini wa roho, ambao wameonja mateso na magumu katika maisha; heri wapole na wenye huruma; watetezi wa haki na wajenzi wa amani. Heri za Mlimani ni tabia na utambulisho wa kudumu wa Mkristo, ni dira na mwongozo wa safari ya maisha ya Mkristo.

Cyprus anasema Baba Mtakatifu ni mahali ambapo Bara la Ulaya linakutana na Nchi za Mashariki; mahali pa kwanza kabisa ulipoanzia mchakato wa utamadunisho Barani Ulaya. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ameguswa sana kuweza kufuata nyayo za wamisionari wakuu wa kwanza wa Kanisa kama vile Watakatifu Paulo, Barnaba pamoja na Marko. Baba Mtakatifu yuko nchini Cyprus kama hujaji na hamu yake kubwa ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, ili Cyprus iweze kuwa ni chemchemi ya furaha chini ya mwamvuli wa Heri za Mlimani. Na kama ilivyokuwa kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo, watu wote wabahatike kupata ujumbe wa uzuri wa Heri za Mlimani sanjari na sera makini za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Cyprus ni lulu ya thamani kubwa katika moyo wa Bahari ya Mediterrania, kwa sababu Cyprus imekuwa ni kitovu cha tamaduni za watu mbalimbali na nchi ambayo ina wahamiaji na wakimbizi wengi kuliko nchi nyingine yoyote kwenye Umoja wa Nchi za Ulaya, EU. Uvumilivu na maridhiano yanawawezesha watu wa Mungu nchini Cyprus kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Kanisa Katoliki na wadau mbalimbali wa maendeleo fungamani ya binadamu wamechangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu, ustawi na maendeleo ya jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, lulu ya Cyprus imechafuliwa na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambao umekuwa ni kikwazo kwa watalii kutembelea Kisiwani hapo. Ni nchi ambayo imeathirika kutokana na myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa, lakini taratibu, Cyprus inaanza tena kuimarika kiuchumi. Jambo la msingi ni kusimama kidete ili kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma; mambo yanayokwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu na matokeo yake ni kukua na kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Cyprus imejeruhiwa sana na ukosefu wa uhuru wa kuabudu kwani tangu kumeguka kwa Cyprus kuna watu ambao hawajapata mahali pa kuabudia.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi;  pamoja na maridhiano, amani itaweza kupatikana na hivyo kurahisisha ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu. Hapa kuna haja ya kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja; kwa kuangalia vipaumbele vya maisha ya watu wa Mungu; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha amana, utajiri na urithi wa kidini na kitamaduni pamoja na kuwarejeshea watu yale mambo matakatifu yaliyotaifishwa kutoka kwao sanjari na kuendelea kujikita katika “Njia ya Kidini Kama Mradi wa Amani nchini Cyprus” unaoragibishwa na Ubalozi wa Sweden, ili kuendeleza majadiliano ya kidini miongoni mwa viongozi wa dini mbalimbali nchini Cyprus.

Pale ambapo matumaini ya majadiliano yanaonekana kana kwamba, yanaanza kufifia, huo ndio wakati muafaka wa kujikita katika majadiliano kwa kukazia uvumilivu, kwa kuondokana na chuki na uhasama, kwa kuganga na kuponya majeraha, ili kujielekeza zaidi katika misingi ya amani, ushirikiano na maridhiano kati ya watu wa Mungu. Hakuna sababu msingi ya watu kudhaniana vibaya. Ni wakati muafaka wa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaoendelea kujitokeza kwenye Bahari ya Mediterrania. Bahari hii, iwe ni kitovu kinachowaunganisha watu wenye historia, tamaduni, dini na imani mbalimbali! Kimsingi Bahari ya Mediterrania igeuke na kuwa ni kitovu na karakana ya ujenzi wa amani inayojengwa kila siku na watu wa kawaida. Bara la Ulaya linahitaji kujikita katika mchakato wa upatanisho na amani; ujasiri na ari kuu, ili kuweza kusonga mbele, kwa kuondokana na hofu isiyokuwa na mvuto wala mashiko.

Ikumbukwe kwamba, mchakato wa kufufua uchumi peke yake, hautaweza kufua dafu ili kurejesha amani na usalama, bali utamaduni wa watu kukutana katika ukarimu, utaweza kuleta mabadiliko makubwa yanayokusudiwa. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, kama ilivyokuwa furaha kwa Mitume Paulo na Barnaba walipokuwa wanapitia katika Kisiwa hiki cha Cyprus, ndivyo hata yeye alivyo na furaha kuu katika siku hizi za uwepo wake kati ya watu wa Mungu nchini Cyprus, ili aweze kusafiri katika historia na roho ya nchi hii, ili umoja na uzuri viendelee kuwa ni dira na mwongozo wa Cyprus kuelekea huko mbeleni!

Viongozi wa Serikali
03 Desemba 2021, 15:33