Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Madonda ya Watu wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus kuanzia Alhamisi tarehe 2 hadi Jumamosi tarehe 4 Desemba 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Tufarijiane Katika Imani.” Haya ni maneno yanayotokana na jina na Mtume Barnaba, maana yake Mwana wa Faraja! Ni yule Mtume aliyekuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa Mitume! Rej. Mdo 4: 36. Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 3 Desemba 2021 baada ya kukutana na kuzungumza na wajumbe wa Sinodi Takatifu ya Kanisa la Kiorthodox la Cyprus, ameadhimisha pia Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja maarufu wa “Il Pancyprian Gymnastic Association Stadium” maarufu kama New GSP, Kwa lugha ya Kigiriki “Στ?διο Γυμναστικ?? Σ?λλογο? "Τα Παγκ?πρια"). Takwimu zinaonesha kwamba, Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na waamini zaidi ya elfu kumi. Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada hii ya Misa Takatifu amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa waamini kumwendea Kristo Yesu ili aweze kuwaganga na kuwaponya. Waamini wachukue madonda na wathubutu kuomba huruma, msamaha na upendo wa Kristo Yesu, ili hatimaye waweze kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa furaha na bashasha!
Mwana wa Timayo, Bartimayo aliposikia kwamba Yesu Mnazareti anapita karibu yake, alipiga kelele na kusema, “Mwana wa Daudi, Yesu, Unirehemu”. Sauti hii, iliwachefua baadhi ya watu, wakataka kumnyamazisha na kumshikisha adabu, lakini Bartimayo, akazidi kupaaza sauti akisema “Mwana wa Daudi, Yesu, Unirehemu”. Hiki ni kielelezo cha mwamini anayeomba rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu bila kuchoka, mwamini anayetaka ishara ya huruma na uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Bartimayo, kipofu anamtambua Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Daudi, yaani Masiha. Hii ni kiri ya imani kutoka kwa mtu ambaye alidharauriwa na watu wote pale njiani. Kristo Yesu, akakisikiliza kilio chake, kwa sababu aligusa sakafu ya moyo wake, kiasi hata cha kuwa tayari kumfungulia malango ya wokovu! Yule waliyetaka kumshikisha adabu, sasa “amepewa jeuri” anaitwa na Kristo Yesu ambaye anamuulizia kile alichotoka kutoka kwake.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini katika kipindi hiki cha Majilio kumpokea na kumkaribisha Kristo Yesu anayekuja na kupita katika hija ya maisha yao hapa duniani! Huu ni mwaliko kwa waamini kumwendea Kristo Yesu ili aweze kuwaganga na kuwaponya. Nabii Isaya anasema Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Rej. Isa 35:5. Macho ya vipofu yataona katika upofu na katika giza. Rej. Isa 29: 18. Vipofu walimtega Kristo Yesu na kuamua kufuatana naye, ili aweze kuwakirimia mwanga ili kushinda upofu wao. Kristo Yesu anawaalika wale wote wanaoelemewa na mizigo kumwendea, badala ya kujifungia katika ubinafsi wao na kuanza kulalama. Kristo Yesu ni mganga wa kweli, anayemwangazia mwanadamu, mwanga, huruma na upendo wake wa daima na hatimaye kumkomboa yule anayeelemewa na uzito wa dhambi moyoni mwake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumpatia nafasi Kristo Yesu ili aweze kuwaganga na kuwaponya kutoka katika undani wa maisha yao! Mwana wa Timayo, Bartimayo kipofu alikuwa peke yake, lakini Mwinjili Mathayo 9: 27-31 anaonesha jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyowaponya vipofu wawili. Wote wawili katika umoja wao, waliomba huruma na upendo wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kutoka katika ubinafsi wao unaotesa na kuunyong’onyesha moyo.
Waamini waombe nguvu ya uponyaji ili waweze kumwona Mwenyezi Mungu, Baba wa milele na kuwatambua wengine kuwa ni ndugu na jirani zao na wala si kama mzigo wa kutua! Si rahisi sana kuweza kupambana na changamoto na matatizo ya maisha katika ubinafsi! Kumbe kuna haja ya kushirikiana na kushikamana kama ndugu wamoja, ili kushirikishana madonda ya ubinadamu na hatimaye kupambana na changamoto mamboleo kwa pamoja. Huu ni wito wa kupyaisha tena udugu wa kibinadamu kwa kujenga na kudumisha umoja unaosimikwa katika majadiliano. Nguvu ya uponyaji inajionesha ikiwa kama watu wote kwa pamoja wataweza kushirikiana kupambana na matatizo pamoja na changamoto za maisha. Hii ndiyo neema ya kuishi katika jumuiya kwa kutambua kwamba wote ni watoto wa Baba mmoja licha ya tofauti zao msingi. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, wale vipofu wawili baada ya kuponywa, wakaambiwa kuchunga ili watu wasijue, lakini wao wakatoka na kuanza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Vipofu wanageuka kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili ambayo huijaza mioyo na maisha ya wale wote wanaokutana na Kristo Yesu. Rej. Evangeliii gaudium, 1.
Furaha ya Injili inawaokomboa waamini na hatari ya imani inafumbatwa katika ubinafsi, imani kavu na ya watu wanaolalamika na hivyo kugeuka kuwa ni kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji. Baba Mtakatifu amewapongeza watu wa Mungu nchini Cyprus kwa ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; imani inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao; imani inayosimikwa katika upendo. Huu kamwe si wongofu wa shuruti bali ushuhuda wa imani. Huu ni mwaliko wa kutoka ili kwenda kukutana na Kristo Yesu, ili aweze kuwaangazia upofu wa maisha yao, ili waweze kuwa ni mashuhuda na faraja kwa jirani zao. Wakristo waendelee kuwasha moto wa matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha. Wakristo wapandikize na kuotesha mbegu ya Injili katika uhalisia wa maisha, ili iwe ni faraja katika upweke, mateso na umaskini. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa mahubiri yake amewakumbusha waamini kwamba, Kristo Yesu anaendelea kupita hata katika barabara za Cyprus. Anasikiliza na kujibu kilio chao! Anagusa nyoyo zao, jambo la msingi kwa waamini ni kuwa na imani kwa Kristo Yesu ili aweze kuwakirimia mwanga, ili kuwaganga na kuwatibu katika upofu wao ili watembee katika mwanga. Kristo Yesu anaweza kuganga, kuponya na kupyaisha udugu wa kibinadamu, kwa kuwaongezea furaha. Pamoja na Kanisa zima, wote wanasema, Njoo Bwana Yesu!