Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Ushirika-Udugu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, kuhusu Mtakatifu Yosefu, Jumatano, tarehe 1 Desemba 2021, amesema, Alhamisi tarehe 2 Desemba hadi tarehe 6 Desemba 2021 anafanya hija ya kitume nchini Cyprus na Ugiriki. Anakwenda kuwatembelea watu wa Mungu katika nchi hizi mbili ambazo zina utajiri mkubwa wa historia, tasaufi na utamaduni. Hii ni hija inayolenga kuzima kiu ya maisha ya kiroho kutoka katika chemchemi ya imani ya kitume na udugu wa kibinadamu kati ya Wakristo wa Makanisa mbalimbali. Ni nafasi ya kukaribia na kugusa madonda ya majeraha ya ubinadamu miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na matumaini zaidi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, atatembelea Kisiwa cha Lesvos. Anawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza katika hija yake kwa sala na sadaka ya maisha yao!
Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus kuanzia tarehe 2-4 Desemba 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Tufarijiane Katika Imani”. Haya ni maneno yanayotokana na jina na Mtume Barnaba, maana yake Mwana wa Faraja! Ni yule Mtume aliyekuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa Mitume! Rej. Mdo 4: 36. Baba Mtakatifu katika hija hii ya kitume anapenda kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kufarijiana katika imani, kama sehemu ya nyenzo muhimu katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano, ujenzi wa madaraja ya watu kukutana sanjari na ukarimu; amali za jamii nchini Cyprus. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Barnaba ni Mlinzi na Mwombezi wa nchi ya Cyprus. Watu wa Mungu nchini Cyprus wanatarajia kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao itasaidia kunogesha zaidi amani na ushirika.
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 4-6 Desemba 2021 anafanya hija ya kitume nchini Ugiriki kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Jiwekeni Wazi Kwa Mshangao wa Mungu.” Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Ulimwenguni. Huu ni ujumbe makini hasa katika kipindi hiki ambacho kuna maambukizi makubwa ya Virusi vya Korona, UVIKO-19 vinavyotishia maisha, ustawi na maendeleo ya wengi. Ugiriki ni nchi ambayo ilitikiswa sana na myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa. Kumbe, hija hii ya kitume, ni kielelezo cha mwanga wa matumaini kwa nchi ya Ugiriki ambayo kimsingi ina utajiri mkubwa wa historia ya imani. Hiki ni kipindi kigumu sana cha maisha ya watu wengi nchini Ugiriki. Watu wa Mungu nchini humo wanamwona Baba Mtakatifu Francisko kama rafiki anayewatembelea ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo!
Wakati huo huo, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano na Vatican News kuhusiana na Hija ya 35 ya Kimataifa ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus na Ugiriki anasema, Baba Mtakatifu anataka kuwashirikisha ile furaha ya Injili na mwanga wa matumaini; kwa kukazia ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kwa kusaidiana na kushikamana na maskini na wale wote wenye mahitaji zaidi. Hii ni fursa inayopania kuleta mtazamo mpya wa Bahari ya Mediterrania inayoonekana kuwagawa watu na kuanza kujielekeza kuwa ni mahali pa kuwakutanisha watu. Baba Mtakatifu anapenda kukutana na watu wa Mungu katika nchi hizi mbili. Hii ni hija katika mwanzo wa historia na maisha ya Kanisa kama wanavyosimulia Watakatifu Paulo na Barnaba, Mitume.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, dira na mwongozo wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kunako mwaka 1974, mtafaruku ulitokea nchini Cyprus na hivyo kujikuta ikiwa imemeguka vipande viwili. Hadi wakati huu, juhudi za kuziunganisha pande mbili zinazosigana bado zimegonga mwamba. Vatican kwa upande wake, inakazia zaidi majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Cyprus. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kama sehemu ya mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Maaskofu wa Makanisa ya Mashariki, kuanzia tarehe 4-6 alifanya hija ya kitume nchini Cyprus. Lengo lilikuwa ni kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene. Ilikuwa ni nafasi ya pekee kwa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuweza kuwakabidhi Maaskofu Hati ya Kutendea Kazi “Instrumentum laboris.” Alikazia msingi wa amani, umoja na ushuhuda.
Baba Mtakatifu Francisko anatembelea pia Ugiriki, mahali ambapo pana mizizi ya historia ya Kanisa. Hapa ni mahali ambapo Mtume Paulo na Barnaba walisadaka maisha yao ili kuhakikisha kwamba, Habari Njema ya Wokovu inatangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Bahari ya Mediterrania badala ya kuwagawa watu na kugeuka kuwa ni kaburi lisilokuwa na alama, itageuka na kuwa ni mahali pa watu kukutana. Bahari ya Mediterrania ni kitovu cha wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Kumbe, kuna haja ya kusafiri kwa pamoja, ili kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kukabiliana na changamoto za maisha kwa amani na utulivu. Janga la Ugonjwa wa Virusi wa Korona, UVIKO-19, Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya changamoto pevu za kimataifa zinazopaswa kushughulikiwa kwa pamoja katika umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.
Bado kuna vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, baa la njaa, ujinga na umaskini; yote haya hayana budi kushughulikiwa kwa pamoja. Hija hii ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko inawakumbatia watu wote, ili kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu kwa masikitiko makubwa anawakumbuka wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Ni watu wanaokimbia vita na umaskini, kwa bahati mbaya wanakumbana na “mkono wa chuma”, ambao unakataa kuwapokea na matokeo yake wanakumbana na kinzani, chuki na uhasama na hata kunyonywa. Lakini ikumbukwe kwamba, hawa ni ndugu zetu na kwamba, kuna maelfu ya watu ambao wamepoteza maisha na kumezwa kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania ambayo imegeuka na kuwa ni kaburi lisilo na alama. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anasema, kati ya maeneo maalum atakayotembelea wakati wa hija yake ni Kisiwa cha Lesvos, chemchemi ya maisha ya pamoja, ili kukuza na kuragibisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu na maendeleo fungamani. Ni hija inayopania pia kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene na Wakristo wa Kanisa la Kiorthodox na hatimaye, kuimarisha udugu wa kibinadamu miongoni mwa watu wa Mungu!