Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Uinjilishaji, Haki na Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumamosi tarehe 4 hadi Jumatatu tarehe 6 Desemba 2021 anafanya hija ya kitume nchini Ugiriki kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Jiwekeni Wazi Kwa Mshangao wa Mungu.” Baada ya kuwasili na kusalimiana na wenyeji wake, Baba Mtakatifu alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali na Vyama vya kiraia pamoja na wanadiplomasia kwenye Ikulu la Athens nchini Ugiriki. Baba Mtakatifu katika hotuba yake ameelezea lengo la hija yake ya kitume nchini Ugiriki ili kuona mshangao wa Mungu na mwanadamu. Amegusia kuhusu demokrasia shirikishi, Mchango wa Ukanda wa Mediterrania, Athari za UVIKO-19 pamoja na Amri Kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru viongozi na watu wa Mungu nchini Ugiriki katika ujumla wao. Anatembelea Ugiriki kama hujaji katika nchi ambayo imesheheni utajiri wa tasaufi, utamaduni na maendeleo; chemchemi ya furaha inayorutubisha hekima na hivyo kushirikisha uzuri. Watu wote wa Mungu wanahimizwa kuwashirikisha wengine furaha inayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao na kwamba, Wagiriki wanayo nafasi ya pekee katika mchakato wa kunogesha furaha ya kweli nchini humo na Ulimwenguni.
Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu kuyaelekeza macho yao juu na kuanza hija ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu na kuendelea kubaki binadamu kweli. Ugiriki ni njia panda iliyosaidia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbalimbali za dunia. Neno la Mungu ambalo limeenezwa takribani duniani kote liliandikwa kwa Lugha ya Kigriki. Lugha ya mwanadamu, ikabeba hekima ya Mungu. Bahari ya Mediterrania ikawa ni daraja la kuwaunganisha watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Nchi ya Ugiriki imezalisha wanahistoria na wanafalsafa wakuu kama vile akina Aristotle aliyesema kwamba, kwa asili binadamu ni “kiumbe siasa” na huo ukawa ni mwanzo wa watu kuangaliana raia na huo ukawa ni mwanzo demokrasia. Hapa Baba Mtakatifu anasema, anazungumzia Umoja wa Ulaya, EU na ile ndoto ya amani na udugu wa kibinadamu na kwamba, demokrasia ya kweli inadai ushiriki unaofumbatwa katika kazi ngumu na uvumilivu. Lakini kwa bahati mbaya siasa za kutaka kujimwambafai zinaonekana kuwa na mvuto na mashiko kwa sababu zinatoa majibu mepesi mepesi. Zinaonekana kujibu kiu ya usalama unaofumbatwa katika tabia ya ulaji wa kupindukia na matokeo yake, watu wanashindwa kuwa na uelewa sahihi wa demokrasia.
Demokrasia shirikishi ni jambo muhimu sana kwa sabababu inawasaidia watu kufikia lengo la pamoja, kwani binadamu kama kawaida ni kiumbe jamii, ni wapekee lakini pia anawategemea viumbe wengine. Ukiritimba ni hatari sana kwa demokrasia ya kweli. Siasa inapaswa kuwa ni kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi ili kushirikishana na kwamba, maskini na wanyonge ndani ya jamii wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili wote kwa pamoja waweze kujielekeza kwenda mbele ili kufikia haki jamii. Juhudi zinapaswa kuelekezwa kwa ajili ya ushiriki wa wote. Ili kuweza kukabiliana na changamoto ya: Athari za mabadiliko ya tabia nchi, Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Soko la pamoja sanjari na kupambana na mifumo mbalimbali ya umaskini, kuna haja ya kukazia dhana ya ushiriki mkamilifu wa Jumuiya ya Kimataifa. Hii ni njia inayolenga amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu amezipongeza nchi zinazohusika kwa kuridhia Makubaliano ya Prespa “Treaty of Prespa, the Prespes agreement or the Prespa accord”. Haya ni makubaliano yaliyofikia hatima yake tarehe 17 Juni 2018 kati ya Ugiriki na Jamhuri ya Macedonia chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa ili kutoa suluhu ya mgogoro wa muda mrefu kati ya Ugiriki na Jamhuri ya Macedonia ya Kaskazini. Makubaliano haya yakaridhiwa 12 Februari 2019 kati ya Ugiriki na Jamhuri ya Macedonia ya Kaskazini.
Baba Mtakatifu anasema, Ukanda wa Bahari ya Mediterrania ni alama ya ushirika kama ilivyo miti ya Mizeituni, ingawa kwa sasa miti hii imeathirika na hatimaye, kukatwa. Jani la Mzeituni ni alama ya amani, mahusiano na mafungamano kati ya Mwenyezi Mungu, Muumbaji, binadamu na viumbe wengine. Changamoto ni kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote na kuachana na unafiki unaoendelea kuhatarisha mustakabali wa Mama Dunia. Jumuiya ya Ulaya haina budi kujielekeza zaidi katika ujenzi wa umoja na mshikamano, ili kukabiliana na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa wakati huu. Kuna haja ya kujenga pia uhusiano mwema kati ya Nchi za Kaskazini na Kusini mwa Dunia. Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Kwa njia hii, utu, heshima na haki msingi za watu hawa zitalindwa na kuheshimiwa na amani ya kweli itaweza kutawala na hivyo kuleta matumaini mapya.
Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, kwa kawaida mateso na mahangaiko yanawaunganisha watu na kuwa wamoja, kwa kutambua kwamba watu wote ni sehemu ya familia kubwa ya binadamu, inayopaswa kushikamana na kujielekeza katika ujenzi wa amani kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Jumuiya ya Kimataifa itumie fursa ya kile kinachoonekana kuwa ni majanga na kuyageuza kuwa ni fursa makini za maendeleo fungamani ya binadamu. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni changamoto pevu ambayo imefunua na kuanika udhaifu wa binadamu. Kumbe, kuna haja ya kukazania kampeni ya chanjo dhidi ya UVIKO-19, mshikamano na pale inapowezekana kutoa ruzuku ili kupambana na janga hili ambalo kwa sasa linahatarisha maisha ya watu wengi. Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kuchangia katika mapambano dhidi ya UVIKO-19. Haki ya huduma bora ya afya inapaswa kuheshimiwa, ili maskini na wazee wasitumbukie kwenye utamaduni wa kutupa kwa kutowajali, kwa sababu kila mtu ana haki ya kuishi na wala hakuna haki ya mtu kufa. Watu wajifunze kulipokea fumbo la kifo na kamwe si kuratibu kifo.
Baba Mtakatifu amegusia pia Fumbo la Umwilisho, zawadi kubwa inayoambatana na uhuru wa kumpenda Mungu. Sheria, Kanuni na Taratibu zimewekwa ili kuhakikisha kwamba, hatima hii inafikiwa. Kumbe, kuna haja ya kujifunza kuwajibika, ili kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu sheria. Baba Mtakatifu amelipongeza Kanisa nchini Ugiriki kwa kusimama kidete kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na kuunda mazingira bora zaidi yatakayoliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu. Lengo ni kutekeleza Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani na kuendelea kudumisha ushirika miongoni mwa Wakristo, ili hatimaye, kujenga jamii ambayo iko wazi, fungamani na yenye kutetea haki, ili kukuza upendo kwa jirani na kudumisha demokrasia. Hizi ni tunu msingi dhidi ya utawala wa mabavu, ubinafsi, tabia ya kutowajali wala kuwathamini wengine, hasa maskini na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema, haya ni mambo msingi katika mchakato wa kupyaisha ubinadamu katika nyakati hizi na kwa hakika Bara la Ulaya linazihitaji sana!