Papa Francisko:Kesheni na kuomba ili kulinda moyo dhidi ya ulegevu wa kiroho
Sr. Angella Rwezaula – Vatican
Papa Francisko, Dominika tarehe 28 Novamba 2021, wakati Mama Kanisa anaanza kipindi kipya cha Majilio, akiwageukia waamini na mahujaji waliokusanyika katika uwanja wa Mtakatifu Petro Vatican amesema: "Injili ya liturujia ya siku ya Dominika ya kwanza ya Majilio yaani Dominika ya kwanza ya kujiandalia na Siku Kuu ya kuzaliwa kwa Bwana, inazungumzia juu ya ujio wa Bwana katika mwisho wa nyakati". Yesu anatangaza matukio ya kipee ya misukusuko na mateso lakini kutokana na hilo ndipo anatualika tusiwe na hofu. Ni kwa nini? kwa sababu kila kitu kitaenda vizuri? Hapana ni kwa sababu yeye atakuja. Yesu atarudi, atakuja kama alivyohaidi. Yeye anasema hivi: “mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia. (Lk 21, 28). Ni vizuri Papa Francisko anasema kusikiliza maneno ya kutia moyo kuwa changamkeni na kuviinua vichwa vyenu wakati ambao utafikiri kila kitu kimekwisha na Bwana anakuja kutuokoa; kumsubiri kwa furaha lakini hata na moyo wa misuko suko katika migogoro ya maisha na katika majanga ya historia. Ni kumsubiri Bwana.
Je ni jinsi gani ya kuinua vichwa, bila kukandamizwa na matatizo, bila mateso na kushindwa ? Yesu anatuelekeza njia na wito wa nguvu kwamba: “Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa (…).Kesheni kila wakati na kuomba (Lk 21, 34.36). Akindelea kufafanua neno Kesheni, Papa amesema kukesha ni muktadha muhimu sana katika maisha ya mkristo. Kwa maneno ya Kristo mwenyewe tunaona kuwa kukesha kunaunganisha na umakini. Jiangalieni na siyo kudorora, kwa maana ya kukesha! Kukesha maana yake ni kutoruhusu moyo ufungwe na maisha ya kiroho yasiingizie mambo mabaya. Kuwa makini kwa sababu unaweza kuwa mkristo aliye lala na wala hatujui, kuna wengi sana wakristo walio lala, waliogandamana na kubobea roho ya ulimwengu, bila kuwa na shauku ya kiroho, bila hamu ya kusali au wanasali kama kasuku, bila kuwa na shauku ya utume, bila kuwa na shauku kuu kwa ajili ya Injili. Mkristo hasiyetazama daima ndani hana uwezo wa kutazama upeo. Na hiyo inapelekea usingizi wa na kuangukia kwenye ubaridi, kutokujali kila kitu isipokuwa kile tu tunachojali kwa manufaa binafsi. Haya ni maisha ya huzuni, kwenda namna hii… pale hakuna furaha. Lakini hali halisi ni kinyume, Papa Francisko amesisitiza
Tunahitaji kukesha ili kutoendelea na siku ya ukawaida wa kuelemewa na mambo ya maisha kama asemavyo Yesu (34). Mahangaiko ya maisha yanatuelemea. Leo hii kwa maana hiyo ni fursa nzuri kwa ajili ya kujiuliza: Ni kitu gani kinaelemea moyo wangu? je ni kitu gani kinanielemea katika roho? Ni kitu gani kinanifanya kuwa mzito kwenye sofa la uvivu wangu? Ni mbaya sana kuona wakristo wanaokaa kwenye sofa, wakristo ambao kila kitu wanatunza katika usingizi na katika sofa. Ni mambo gani mabaya ambayo yanagandisha, maovu ambayo yananibamiza chini na kunizuia kuamsha kichwa? Je ninatazama uzito unaowalemea kwenye mabega ya ndugu zangu?, je niko makini au nina sintofahamu? Maswali haya kwa mujibu wa Papa yatatusaidia kwa sababu yanasaidia kuhifadhi moyo dhidi ya ulegevu ambao ni adui mkubwa wa maisha ya kiroho, hata wa maisha, na maisha ya kikristo.
Je ulegevu ni nini? Ulegevu ni uvivu ambao unafanya kuanguka, uteleze katika huzuni, unaondoa ladha ya kuishi na utashi wa kufanya kitu. Ni roho moja mbaya iliyo hasi na ni moja ya roho iliyo mbaya ambayo inapiga moyo msumari katika lepe la usingizi, kwa kuiba furaha. Inaanza na ule huzuni, inateleza hadi kuona hakuna furaha ya kitu chochote. Kitabu cha Mithali kinasema: “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.” (Mith 4,23). Kulinda moyo ndiyo maana ya kukesha amesisitiza Papa mara kaadhaa na kwamba wawe na haraka ya kukesha na kulinda kila mmoja moyo wake. Ni muhimu kuongeza chachu. Siri ya kukesha ni maombi. Yesu kwa hakika anasema hivyo kwamba: “kesheni kila wakati kwa kuomba (Lk 21, 36). Ni sala ambayo inawezesha moyo kubaki unawaka. Na hasa tunapohisi kuwa shauku imekuwa baridi, maombi yanaamsha, kwa sababu inatupeleka kwa Mungu yaani katika kiini cha mambo. Sala inaamsha tena moyo kutoka katika lepe la usingizi na kukazia macho kile ambacho kinahesabika, yaani kinachohusu mwisho wa maisha.
Hata katika siku ambazo zinakuwa zimejaa mambo ya kufanya, Papa Francisko ameshauri kutoacha kusali. Ametoa mfano kwamba alikuwa anatazama kipindi kimoja kwenye Televisheni ya Baraza la maaskofu Italia (TV2000), na kwamba ni tafakari nzuri juu ya sala na ameshauri kuitazama kwani itasaidia. Sala inaweza kusaidia taa ya moyo kubaki inawaka na mara nyingi iliyo fupi. Katika kipindi cha Majilio tuzoee kusema kwa mfano: “ Njoo Bwana Yesu. Ni kusema hili hilo tu: Njoo Bwana Yesu". Katika Kipindi cha maandalizi ya Kuzaliwa kwa Bwana ni vizuri kufikiria pango, kufikiria siku hiyo na kusema ndani ya moyo “Njoo Bwana Yesu Njoo”. Papa mewaomba waamini na mahujaji wote kurudia sala hiyo kwa pamoja. "Turudie sala hiyo kwa siku nzima yote na moyo utabaki unakesha! Kwa kuhitimisha Papa ameomba kusali kwa Mama Maria ambaye anasubiri Bwana kwa moyo unaokesha ili atusindikiza katika safari ya Majilio.