Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Ujumbe Maalum
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cyprus kuanzia tarehe 2-4 Desemba 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Tufarijiane Katika Imani. Akiwa nchini Cyprus, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza naWakleri, Watawa, Makatekista na Vyama vya Kitume. Atapata fursa pia ya kuwahutubia viongozi wa serikali, wanadiplomasia na viongozi wa vyama vya kiraia nchini Cyprus. Atakuwa na mazungumzo ya kiekumene na Askofu mkuu Chrysostomos II wa Cyprus na baadaye atakutana na kuzungumza na Sinodi Takatifu ya Kanisa la Kiorthodox. Ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa GSP mjini Nicosia. Baadaye kutakuwepo pia Ibada ya Kiekumene pamoja na Wakimbizi na Wahamiaji. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 4-6 Desemba 2021 anafanya hija ya kitume nchini Ugiriki kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Jiwekeni Wazi Kwa Mshangao wa Mungu. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa Serikali ya Ugiriki, Wanadiplomasia pamoja na viongozi wa vyama vya kiraia. Atakutana na kufanya majadiliano ya Kiekumene na Askofu mkuu Hieronymos pamoja na ujumbe wake. Itakuwa pia ni fursa ya kukutana na: Wakleri, watawa, majandokasisi na makatekista. Atakutana kwa faragha na Wayesuit wanaoishi na kufanya utume wao nchini Ugiriki.
Baba Mtakatifu atakwenda kuwatembelea wakimbizi na wahamiaji na baadaye kusali Sala ya Malaika wa Bwana. Jioni ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kufunga hija hii ya kitume kwa kukutana na vijana wa kizazi kipya nchini Ugiriki. Kwa hakika nchi ya Ugiriki imepepetwa sana na athari za myumbo wa uchumi Kimataifa sanjari na athari kubwa za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliowatumia watu wa Mungu nchini Cyprus na Ugiriki anawaambia kwamba, kwa sasa anaendelea kujiandaa kwa ajili ya kufanya hija ya kitume katika nchi zao ambazo zimebahatika kupambwa na historia na utamaduni wa Injili. Anataka kufuata nyayo za wamisionari wakuu, hasa Mitume Paulo na Barnaba, ili kugundua tena ile furaha ya Injili kwa kufanya hija kwenye chemchemi ya udugu wa kibinadamu! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu katika nchi hizi mbili, kumsaidia kujiandaa kwa njia ya sala na majitoleo yao. Hii ni hija ya neema ya Kisinodi, inayokita mizizi yake katika udugu wa kitume. Baba Mtakatifu anasema, katika hija hii ya kitume anapenda kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Makanisa ya Kikristo ili kukuza imani na kuendelea kukumbatia amani katika Kristo Yesu! Hakuna sababu msingi ya kuogopa kwani anakwenda kwao ili kuwatia shime.
Kwa njia ya hija yake ya Kitume, Baba Mtakatifu Francisko anasema, atapata pia fursa ya “kuzima kiu” yake kutoka katika Visima vya Bara la Ulaya, kwani Ugiriki ni maskani ya utamaduni wa kale Barani Ulaya. Bahari ya Mediterrania imeshuhudia wamisionari wakichakarika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia pamoja na maendeleo makubwa ya tamaduni mbalimbali. Bahari ya Mediterrania, “Mare Nostrum” inaunganisha nchi nyingi duniani na huo ni mwaliko wa kushikamana na kusafiri kwa pamoja, huku wakiwa wameungana, na hasa katika mapambano dhidi ya Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi katika ujumla wake! Bahari ya Mediterrania inayowaunganisha watu wengi, huku ikiwa na bandari zake, inawakumbusha watu wa Mungu kwamba, chanzo cha kuishi pamoja kinakita mizizi yake katika hali ya maridhiano. Baba Mtakatifu anawashukuru wale wote wanaojisadaka usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, hija hii ya kitume inazaa matunda yanayokusudiwa.
Baba Mtakatifu kwa masikitiko makubwa anawakumbuka wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Ni watu wanaokimbia vita na umaskini, kwa bahati mbaya wanakumbana na “mkono wa chuma”, ambao unakataa kuwapokea na matokeo yake wanakumbana na kinzani, chuki na uhasama na hata kunyonywa. Lakini ikumbukwe kwamba, hawa ni ndugu zetu na kwamba, kuna maelfu ya watu ambao wamepoteza maisha na kumezwa kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania ambayo imegeuka na kuwa ni kaburi lisilo na alama. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anasema, kati ya maeneo maalum atakayotembelea wakati wa hija yake ni Kisiwa cha Lesvos, chemchemi ya maisha ya pamoja, ili kukuza na kuragibisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu na maendeleo fungamani. Hii ndiyo dira ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye chemchemi ya ubinadamu. Baba Mtakatifu anasema, anapenda kukutana na kuzungumza na watu wote wa Mungu! Mwishoni anapenda kutoa baraka zake za kitume kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Tayari amekwisha kumwekea mbele yake nyuso, matamanio yao halali, hofu na mashaka pamoja na matumaini yao!