杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu wakati wa hija yake ya kitume nchini Iraq amesikiliza shuhuda za mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu waliolazimika kuyakimbia makazi yao, wakateswa na wengine kuuwawa kikatili. Baba Mtakatifu wakati wa hija yake ya kitume nchini Iraq amesikiliza shuhuda za mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu waliolazimika kuyakimbia makazi yao, wakateswa na wengine kuuwawa kikatili. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Shuhuda za Wahanga

Hii ni siku ya kuwakumbuka na kuwaombea wahanga wa vita, machafuko na vitendo vya kigaidi, mambo yanayoonekana wazi kabisa katika mji huu. Ukatili usiokuwa na kifani, ukasigina amana na utajiri wa utamaduni wa watu wa Iraq. Nyumba za Ibada zikanajisiwa na kuharibiwa sana na watu wa dini na madhehebu mbalimbali ya Kikristo wakalazimika kuyakimbia makazi na nchi yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko yuko nchini Iraq katika hija yake ya kitume ili kuonesha uwepo wake wa karibu wake kwa Wakristo wote. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, Wakristo katika ujumla wao wamateseka sana. Wengi wao wamepoteza maisha na wengine kulazimika kuikimbia nchi yao, ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi ughaibuni. Ni katika muktadha huu, Iraq inahitaji uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili, aweze kuwatia shime katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu hata katika hali na mazingira magumu kama haya. Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 7 Machi 2021 ametoka mjini Baghdad na kuelekea mjini Erbil. Huu ni kati ya miji kongwe sana duniani na katika miaka ya hivi karibuni ulianza “kuchomoka” kwa maendeleo makubwa, lakini ndoto hii imezimwa kutokana na vita na ghasia na hivyo kugeuka kuwa ni kambi ya wakimbizi na wahamiaji zaidi 540, 000 kutoka Siria. Ni watu wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi baada ya kushambuliwa na wapiganaji wa Dola ya Kiislam “Islamic State, IS”. Baba Mtakatifu akiwa mjini Mosul amesali na kuwaombea wahanga wa vita iliyoanza tarehe 20 Machi 2003.

Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa dini na serikali ya Kurdistan ya Iraq kwa muda mfupi na baadaye akaendelea na safari ya kwenda Mosul, mji wa biashara nchini Iraq.  Eneo hili lilikuwa na Makanisa mengi ya Kikristo, lakini kati ya Mwaka 2014 hadi 2017 mengi yalishambuliwa, yakanajisiwa na kuharibiwa vibaya sana. Vita ya Mwaka 2003 iliendeshwa na Marekani chini ya utawala wa Rais George W. Bush na Tony Blair, Waziri mkuu wa Uingereza wakiwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Iraq. Kulikuwa na tuhuma kwamba, Iraq ilikuwa inamili silaha za maangamizi. Sababu ya pili ilikuwa ni kukomesha utawala wa Rais Saddam Husein kwa sababu alituhumiwa pia kujihusisha na ufadhili wa vitendo vya kigaidi sehemu mbalimbali za dunia. Hatima ya yote haya, ilikuwa ni kuwarejeshea wananchi wa Iraq uhuru wao; ndoto ambayo imegeuka na kuwa ni majanga kwa watu wa Mungu nchini Iraq.  Wakati wa sala ya kuwakumbuka na kuwaombea wahanga wa vita nchini Iraq, waamini wa dini mbalimbali pamoja na viongozi wao wametoa ushuhuda wao. Baba Mtakatifu akatoa utangulizi na hatimaye, sala maalum kwa ajili ya kuwaombea wahanga wa vita na vitendo vya kigaidi nchini Iraq.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake elekezi wakati wa sala hii, amewashukuru waamini pamoja na viongozi wa Kanisa kwa shuhuda zao, hasa kuhusu jinsi ambavyo Wakristo walilazimishwa kuyakimbia makazi na nchi yao, kiasi cha kusababisha madhara makubwa si tu kwa hao waliokuwa wanakimbia, bali hata kwa jamii nzima iliyobaki nyuma! Ni kitendo kilicho vuruga amana na utajiri mkubwa wa mafungamano ya kijamii, kitamaduni na kidini. Baada ya kurejea tena mjini Mosul, Wakristo walianza mchakato wa upatanisho, umoja na mshikamano wa kidugu na waamini wa dini ya Kiislam, ili kujenga tena upya ule udugu wa kibinadamu, kwa kuheshimiana na kushirikiana kwa pamoja, licha ya tofauti zao msingi. Haya ndiyo maua ya udugu wa kibinadamu yanayochomoza hata kwenye jangwa, kielelezo cha matumaini ya upatanisho na mwanzo wa maisha mapya.

Utambulisho wa Mosul unafumbatwa katika uwepo wa waamini wa dini mbalimbali; watu kutoka katika tamaduni na mazingira tofauti. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kutoa mwaliko kwa Jumuiya ya Kikristo kurejea tena mjini Mosul ili kuanza kushiriki katika mchakato wa kuganga, kuponya na kupyaisha maisha ya watu wa Mungu huko nchini Iraq. Hii ni siku ya kuwakumbuka na kuwaombea wahanga wa vita, machafuko na vitendo vya kigaidi, mambo yanayoonekana wazi kabisa katika mji huu. Ukatili usiokuwa na kifani, ukasigina amana na utajiri wa utamaduni wa watu wa Iraq. Nyumba za Ibada zikanajisiwa na kuharibiwa sana na watu wa dini na madhehebu mbalimbali ya Kikristo wakalazimika kuyakimbia makazi na nchi yao. Ikumbukwe kwamba, Jumuiya ya Wayazidi iliteketezwa vibaya sana na vitendo vya kigaidi.

Wengi wakageuka kuwa wakimbizi na wahamiaji na wengi wakauwawa kikatili kabisa. Siku ya Sala kwa ajili ya kuwaombea wahanga wa vita, ghasia na vitendo vya kigaidi ni kutaka kukiri kwamba udugu wa kibinadamu una nguvu na unadumu zaidi kuliko chokochoko na vita. Matumaini yana nguvu zaidi kuliko chuki na kwamba, amani ina nguvu zaidi kuliko vita. Utambuzi huu ni muhimu sana kuliko sauti za chuki na vita na kamwe hautaweza kuzimishwa na watu wanaomwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia kwa kutumia pia vibaya Jina la Mwenyezi Mungu.

Wahanga wa Vita

 

07 Machi 2021, 16:38