杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu Jumapili tarehe 7 Machi 2021 amewashukuru watu wa Mungu nchini Iraq kwa kufanikisha hija yake ya kitume! Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu Jumapili tarehe 7 Machi 2021 amewashukuru watu wa Mungu nchini Iraq kwa kufanikisha hija yake ya kitume! 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Shukrani Kwa IRAQ

Papa amewashukuru watu wote wa Mungu nchini Iraq; wale wote walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake pamoja na mashuhuda wa imani ambao wako mbinguni, wote wanawataka washikamane ili kuonesha umoja kamili. Amewashukuru na kuwapongeza viongozi wa Kanisa na Serikali walioshirikiana kwa karibu sana ili kufanikisha hija hii ya kitume nchini Iraq.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya 33 ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia Ijumaa tarehe 5 hadi Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amejikita kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba ufunuo wa nguvu na hekima ya Mungu; Umuhimu wa waamini kusafisha nyoyo zao kwani ni maskani ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Yesu anawasamehe na kuwapatia waja wake fursa ya kushiriki nguvu na hekima yake. Yesu alizungumzia kuhusu Hekalu la Mwili wake na Hekalu kama Kanisa. Kristo Yesu alifunua nguvu na hekima yake kwa njia ya msamaha na huruma; kwa kuteswa, kufa na kufufuka kwa wafu. Kwa njia hii akaonesha uaminifu wake kwa upendo wa Mungu na Agano lake la Kale lililomwezesha kuwatoa Waisraeli utumwani na kuwaongoza katika uhuru wa watoto wa Mungu. Waamini wanahitaji nguvu na hekima ya Mungu iliyofunuliwa juu la Msalaba.

Mara baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kutoka kwenye Uwanja wa Michezo wa “Franso Hariri” huko Erbil. Baba Mtakatifu amewashukuru watu wote wa Mungu nchini Iraq; wale wote walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake pamoja na mashuhuda wa imani ambao wako mbinguni, wote wanawataka washikamane ili kuonesha umoja kamili. Amewashukuru na kuwapongeza viongozi wa Kanisa na Serikali ya Iraq walioshirikiana kwa karibu sana ili kufanikisha hija hii ya kitume nchini Iraq. Amewapongeza Wakurdi na wale wote walioshiriki katika maandalizi na hatimaye utekelezaji wa hija hii ya kitume. Baba Mtakatifu anakaza kusema, amesikiliza sauti ya mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Iraq, lakini pia amesikiliza sauti ya matumaini na faraja. Anawashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya mchakato wa ujenzi wa Iraq mpya.

Kwa namna ya pekee kabisa amelipongeza na kulishukuru Shirika la Misaada kwa Ajili ya Makanisa ya Mashariki, ROACO pamoja na Mashirika mbalimbali ya misaada kwa huduma yao! Baba Mtakatifu anasema, anajiandaa kurejea tena mjini Roma ili kuendelea na maisha na utume wake kama kawaida, lakini Iraq itaendelea kubaki katika akili na moyo wake. Anawataka watu wa Mungu nchini Iraq kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ujenzi wa amani, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu, ili kamwe asiwepo mtu atakayeachwa nyuma. Anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa daima kwa njia sala na sadaka yake. Hii iwe ni fursa ya kujenga na kuimarisha mafungamano ya udugu na mshikamano katika huduma kwa ajili ya: amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Papa Shukrani
07 Machi 2021, 17:17