杏MAP导航

Tafuta

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu 4 Februari 2021: Udugu wa Kibinadamu katika mchakato wa ujenzi wa amani duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu 4 Februari 2021: Udugu wa Kibinadamu katika mchakato wa ujenzi wa amani duniani. 

Papa Francisko: Siku ya Kimataifa Ya Udugu wa Kibinadamu! AMANI

Kwa kuheshimu tamaduni, mapokeo na mahali anapotoka mtu, yote haya yasaidie mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu; kwa kusikilizana na kukaribishana katika ukweli na uwazi. Huu ni mchakato wa ujenzi wa urafiki wa kijamii, vinginevyo, watu watageuka na kuwa maadui. Hakuna sababu ya kuwa na vita, ili kujenga uadui, inatosha tu kutomjali wala kumthamini jirani yako!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Mataifa unatambua na kuthamini mchango wa majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbalimbali duniani, kama sehemu ya mchakato wa kufahamiana sanjari na kutambua tunu msingi za maisha ya kiroho wanazoweza kushirikisha kwa familia nzima ya binadamu. Hii ndiyo changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na waamini, kila kukicha! Itakumbukwa kwamba, ilikuwa ni tarehe 21 Desemba 2020 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipopitisha Azimio Kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu. Maadhimisho haya kwa mara ya kwanza yamefanyika tarehe 4 Februari 2021. Washiriki wakuu wakiwa ni: Baba Mtakatifu Francisko, Dr. Ahmad Al-Tayyib, Bwana Antònio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na viongozi wengine kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa. Lengo ni kudumisha majadililiano ya kidini na kitamaduni; umoja, mshikamano na ushirikiano wa Kimataifa, ili kujielekeza zaidi katika ujenzi wa utamaduni wa amani, maridhiano, mshikamano wa kidugu na upatanisho wa Kitaifa na Kimataifa. Mambo makuu yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ni: Udugu wa kibinadamu, Mshikamano na Amani.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video katika maadhimisho haya anakazia udugu wa kibinadamu. Kwa namna ya pekee, anamshukuru na kumpongeza Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, ambaye amekuwa kwa hakika mwandani wa changamoto na hatari katika mapambano ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Anamshukuru kwa mchango wake mkubwa katika kuhariri Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa mkwaju hapo tarehe 4 Februari 2019 huko mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Uwepo wa Dr. Ahmad Al-Tayyib, umekuwa msaada mkubwa na ushuhuda wa ujasiri kwa Baba Mtakatifu Francisko kiasi cha kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Hii ilikuwa ni dhamana nyeti, lakini Dr. Ahmad Al-Tayyib ameitekeleza na hivyo kwa pamoja kuweza kusaidiana. Mchakato huu umeendelea kujenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu.

Baba Mtakatifu anamshukuru pia Sheikh Mohammed Bin Zayed kwa jitihada zake zote ili kufanikisha safari hii ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Aliamini na kuwaamini wadau katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Katika shukrani hizi, Baba Mtakatifu anampongeza pia Jaji Abdel Salam, mchapakazi hodari na kiongozi mwenye mawazo mapana, aliyewatia shime kusonga mbele pasi na mawaa, kiasi kwamba, leo hii, udugu wa kibinadamu ni mpaka mpya wa ubinadamu. Hapa hakuna cha uchaguzi, au ni kushikamana na kuwa wamoja kama ndugu, au wote kuangamizana na kupotea kama “ndoto ya mchana”. Hakuna tena muda wa kuangaliana kwa “jicho la kengeza”, wala kunawa mikono kwamba, hakuna anayehusika au kujiweka pembeni! Wote ni ndugu wamoja, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga katika ulimwengu mamboleo.

Udugu wa kibinadamu maana yake ni kushikamana, kusaidiana, kuthaminiana na kuheshimiana hata katika tofauti msingi. Majadiliano ni muhimu katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kwani wote ni watoto wa Baba mmoja, Mungu Mwenyezi. Ni watu wenye tamaduni tofauti, lakini wote ni ndugu wamoja. Kwa kuheshimu tamaduni, mapokeo na mahali anapotoka mtu, mambo yote haya yasaidie mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu; kwa kusikilizana kwa makini na kukaribishana katika ukweli na uwazi. Huu ni mchakato wa ujenzi wa urafiki wa kijamii, vinginevyo, watu watageuka na kuwa maadui. Hakuna sababu ya kuwa na vita, ili kujenga uadui, inatosha tu kutomjali wala kumthamini jirani yako na huo ukawa ni mwanzo wa uadui.

Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru na kumpongeza Dr. Ahmad Al-Tayyib, kwa msaada na ushuhuda wake wenye mvuto na mashiko, lakini zaidi kwa kutembea kwa pamoja kama ndugu wamoja. Tarehe 4 Februari 2021 kwa mara ya kwanza tuzo la Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, Muasisi wa Umoja wa Falme za Kiarabu ulioanzishwa tarehe 2 Desemba 1971 imetolewa kwa heshima ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri. Viongozi hawa ndio waasisi pia wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu. Tuzo hii pamoja na mambo mengine, inataka kunogesha jitihada za watu binafsi, vikundi na taasisi mbalimbali zinazojipambanua katika kutafuta, kujenga na kukuza mahusiano na mafungamano ya kibinadamu; madaraja ya majadiliano ya kidini sehemu mbalimbali za dunia; umoja, mshikamano na ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa.

Kimsingi Tuzo hii ni alama ya ushirikiano na mshikamano kati ya waamini wa dini mbalimbali wanaojipambanua kwa huduma kwa ajili ya binadamu wote! Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kumshukuru pia Bwana Antònio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kuwapatia tuzo pamoja na jitihada zake mbali mbali zinazopania kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano; mambo yanayoweza kupatikana ikiwa kama watu wanao ule moyo wa udugu. Ni kiongozi ambaye amejipambanua kwa kusadaka maisha yake, ili watu wote waweze kujisikia kuwa ni ndugu wamoja. Huu ni wakati wa kupandikiza maneno ya mbegu ya amani ili kujenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu.

Papa Udugu
04 Februari 2021, 16:08