Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu: Wajenzi wa Amani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni kitovu cha Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, mintarafu masuala ya kijamii kadiri ya Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni muhtasari wa mafundisho, hotuba na mawazo yake tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kunako mwaka 2013. Waraka huu wa kijamii unachota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu uliotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu inakazia pamoja na mambo mengine kuhusu: Ujenzi wa utamaduni wa majadiliano ya kidini; umuhimu wa waamini wa dini mbali mbali kufahamiana, ili kushirikiana na kushikamana, kwa kutambua na kuheshimu tofauti zao msingi. Udugu wa kibinadamu ni sehemu ya utu wa mwanadamu unaowasukuma kusumbukiana katika maisha.
Udugu huu unapaswa kusimikwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa kuondokana na vizingiti vinavyowatenganisha watu kwa misingi ya udini pamoja na vita vya kidini. Hii ni changamoto ya kushikamana ili kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Ikumbukwe kwamba, majadiliano ya kidini yanapata chimbuko lake katika majadiliano kati ya Mungu na waja wake. Waamini wa dini mbali mbali hawana budi "kufyekelea" mbali misimamo mikali ya kidini na kiimani ambayo imekuwa ni chanzo cha maafa na mahangaiko ya watu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu itaendelea kupokelewa kwa mikono miwili na Jumuiya ya Kimataifa, ili kujenga jamii stahimilivu inayosimikwa katika amani, kwa kushirikiana na kushikamana kwa dhati katika huduma kwa watu wa Mungu katika ujumla wao.
Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya kazi kwa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kujenga na kudumisha utamaduni wa amani na ujenzi wa jamii shirikishi, inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ilitiwa mkwaju na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Baada ya miaka miwili, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likatangaza kwamba, tarehe 4 Februari 2021 Jumuiya ya Kimataifa kwa mara ya kwanza inaadhimisha Siku ya Udugu wa Kimataifa. Kutokana na changamoto ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na changamoto zake, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika mshikamano unaoongozwa na kanuni auni!
Ilikuwa ni tarehe 21 Desemba 2020 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipopitisha Azimio Kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu. Lengo ni kudumisha majadililiano ya kidini na kitamaduni; umoja, mshikamano na ushirikiano wa Kimataifa, ili kujielekeza zaidi katika ujenzi wa utamaduni wa amani, maridhiano, mshikamano wa kidugu na upatanisho wa Kitaifa na Kimataifa. Mambo makuu yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ni: Udugu wa kibinadamu, Mshikamano na Amani. Yote haya yanapania “kufyekelea” mbali “ndago” za uchoyo na ubinafsi, ili kujenga utamaduni wa majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Siku hii inawakumbusha watu wote wa Mungu kwamba, ni ndugu wamoja! Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu tarehe 4 Desemba 2019 iliwasilisha mapendekezo kwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres na matunda yake ni Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu tarehe 4 Februari 2021.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, sala ina umuhimu wake wa pekee katika maisha ya waamini ndiyo maana alipokea na kuridhia mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, ili kwamba, hapo tarehe 14 Mei 2020 waamini wa dini na madhehebu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waweze kuunganika na kushikamana kwa njia ya sala, kufunga na kutenda matendo ya huruma kama njia ya kumwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo aweze kuwasaidia binadamu kuvuka janga hili la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot anasema, dini mbalimbali duniani zina mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, ili kujenga urafiki na udugu wa kibinadamu. Hii ni changamoto kwa waamini kushuhudia tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni katika maisha yao kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, umoja na usawa.
Ni mwaliko kwa waamini kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi, hasa wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapopambana na changamoto ya Virusi vya Corona, COVID-19. Ni wakati wa kuondokana na kinzani, misigano na mipasuko ya kidini na kuanza kujielekeza zaidi katika misingi ya haki, amani, maridhiano na upatanisho. Tarehe 4 Februari 2021 kwa mara ya kwanza tuzo la Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, Muasisi wa Umoja wa Falme za Kiarabu ulioanzishwa tarehe 2 Desemba 1971 inatolewa. Tuzo hii inatolewa kwa heshima ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri. Viongozi hawa ndio waasisi pia wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu. Tuzo hii pamoja na mambo mengine, inataka kunogesha jitihada za watu binafsi, vikundi na taasisi mbalimbali zinazojipambanua katika kutafuta, kujenga na kukuza mahusiano na mafungamano ya kibinadamu; madaraja ya majadiliano ya kidini sehemu mbalimbali za dunia; umoja, mshikamano na ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa. Kimsingi Tuzo hii ni alama ya ushirikiano na mshikamano kati ya waamini wa dini mbalimbali wanaojipambanua kwa huduma kwa ajili ya binadamu wote! Tayari limekwisha undwa jopo la Majaji, litakaloshughulikia Tuzo hii Kimataifa.