Udugu wa Kibinadamu: Viongozi Wakuu Kuadhimisha Kwa Pamoja!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni kitovu cha Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, mintarafu masuala ya kijamii. Huu ni muhtasari wa mafundisho, hotuba na mawazo yake tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kunako mwaka 2013. Waraka huu wa kijamii unachota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu uliotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Muswada wa Waraka wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu uliandikwa na kufanyiwa marekebisho kwa muda wa mwaka mzima, lakini, ukaanikwa hadharani, tapo tarehe 4 Februari 2019, wakati wa Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu.
Ni katika amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 21 Desemba 2020, limetangaza kwamba, kuanzia sasa, tarehe 4 Februari 2021 itakuwa ni Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu. Tukio hili kwa mara ya kwanza katika historia ya Jumuiya ya Kimataifa linaadhimishwa kwa kuwashirikisha viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa, kuanzia majira ya saa 8:30 Mchana kwa saa za Ulaya. Tukio hili linatarajiwa kurushwa mubashara na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Washiriki wakuu ni pamoja na: Baba Mtakatifu Francisko, Dr. Ahmad Al-Tayyib, Bwana Antònio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na viongozi wengine kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni mchango mkubwa unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana ili kujenga na kudumisha udugu na urafiki wa kijamii.
Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Januari 2021 kwa njia ya video inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, alipenda kukita ujumbe wake katika huduma ya udugu wa kibinadamu. Watu wote wanahamasishwa kujielekeza katika huduma ya udugu wa kibinadamu. Papa anawaalika waamini kutoka katika dini, tamaduni na imani mbalimbali kurejea tena katika mambo msingi yaani upendo kwa jirani. Huu ni ujumbe unaopania kukabiliana na changamoto mamboleo ambazo zinazoikabili familia ya binadamu. Hizi ni changamoto zinazoweza kupatiwa ufumbuzi ikiwa kama watu watajenga umoja na mshikamano kwa kutambua kwamba, wao ni ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi za kiimani, kitamaduni na Kimapokeo. Jumuiya ya mwanadamu inaweza kujenga jamii inayoshikamana au vinginevyo kesho ya mwanadamu itakuwa mashakani. Dini na madhehebu mbalimbali duniani, yanayo dhamana ya ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu na tamaduni zao.
Watu wote wanapaswa kutambua kwamba, wao ni watoto wa Baba mmoja na kamwe wao si watoto yatima, kumbe, wote wanaweza kuishi kwa amani. Tofauti za kidini, kiimani na Kimapokeo, kamwe zisiwe ni sababu za kushindwa kufikia utamaduni wa watu kukutana, kwa sababu wote ni ndugu wamoja wanaosali! Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa fadhila ya imani kwa kutambua kwamba, kwa Wakristo, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapata chanzo chake kutoka katika Injili ya Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuchuchumilia na kuambata mambo msingi katika imani yaani: Uchaji kwa Mwenyezi Mungu na upendo kwa jirani. Waamini wa dini mbalimbali duniani wanaweza kuwa na vyanzo vyao vingine, lakini kwa Wakristo utu na udugu wa kibinadamu umesimikwa katika Injili ya Kristo Yesu.
Hizi ni juhudi zilizotekelezwa kwa kushirikiana na Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu: Wajumbe wa Kamati hii ni pamoja na Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Professa Mohamed Hussein Mahrasawi, Mkuu wa Chuo cha Al Azhar na Monsinyo Yoannis Lahzi Gaidi, Aliyekuwa Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko. Wengine katika kamati hii ni Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, mshauri mkuu wa Mufti mkuu. Wajumbe wengine ni wale walioteuliwa kutoka Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Baraza la Wazee wa Kiislam Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na watu maarufu katika tasnia ya habari Umoja wa Falme za Kiarabu.
Kwa upande wao, viongozi wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Amiri Jeshi Msaidizi, watahakikisha kwamba, Hati ya Udugu wa Kibinadamu inatekelezwa kwa dhati kabisa na Kamati iliyoundwa, ili kumwilisha malengo yaliyobainishwa kwenye Hati hii. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linapenda kutumia fursa hii, kuitia shime Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, mintarafu malengo yaliyobainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Hati hiyo. Umoja wa Mataifa unazihamasisha Nchi wanachama, Mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na Vyama vya kiraia kuhakikisha kwamba, vyote vinasaidia kunogesha Siku ya Kwanza ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu, yaani tarehe 4 Februari 2021.