杏MAP导航

Tafuta

Papa Francisko amezindua Waraka wake "Fratelli tutti": Yaani "Wote ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii. Waraka unajikita katika masuala ya kijamii zaidi. Papa Francisko amezindua Waraka wake "Fratelli tutti": Yaani "Wote ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii. Waraka unajikita katika masuala ya kijamii zaidi. 

Waraka wa Papa Francisko: "Fratelli tutti": Wazinduliwa Rasmi

Papa Francisko: Waraka wake wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Huu ni Waraka unaojikita zaidi katika masuala ya kijamii kama changamoto ya kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini katika ulimwengu huu ambao umejeruhiwa sana kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 3 Oktoba 2020 majira ya jioni baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa lililoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko wa Assisi, mjini Assisi, nchini Italia, lililojengwa kunako karne ya 13, ametia mkwaju kwenye Waraka wake wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Huu ni Waraka unaojikita zaidi katika masuala ya kijamii kama changamoto ya kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini katika ulimwengu huu ambao umejeruhiwa sana kutokana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema kwamba, kwa moyo wa unyenyekevu mkuu anapenda kuukabidhi Waraka huu wa kitume mintarafu masuala ya kijamii kwa watu wote wa Mungu ili waweze kuufanyia tafakari ya kina, ili kuondokana na mwelekeo wa sasa wa kutowajali wengine, ili hatimaye waweze kufikiri na kutenda kwa kuwa na ndoto mpya ya udugu na urafiki wa kijamii unaomwilishwa si tu katika maneno bali katika matendo kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji!

Baba Mtakatifu katika Ibada ya Misa Takatifu, hakutoa mahubiri, bali alitafakari na kusali katika ukimya. Na kabla ya kuweka mkwaju kwenye Waraka wake wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” amemshukuru na kumpongeza Monsinyo Paolo Braida, mkuu wa kitengo cha hotuba na tafsiri za nyaraka za Baba Mtakatifu pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhariri na kuhakiki nyaraka za Baba Mtakatifu. Akiwa njiani kuelekea mjini Assisi kwa njia ya barabara, Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kusimama na kusalimiana na watawa wa ndani wanaoishi kwenye Monasteri ya Vallegloria iliyoko Spello. Alipowasili mjini Assisi, Baba Mtakatifu amepokelewa na Askofu Domenico Sorrentino wa Jimbo Katoliki la Assisi-Nocera Umbra-Gualdo Tadino, Kardinali Agostino Vallini, Mwakilishi wa Papa kwenye Makanisa makuu ya “Santa Maria degli Angeli” na Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko mjini Assisi. Hii ni mara ya nne kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea mjini Assisi.

Kwa upande wake, Padre Mauro Gambetti, Mlinzi mkuu wa konventi ya Assisi anasema, Baba Mtakatifu Francisko amewapatia heshima kubwa, katika siku ya kumbukumbu ya kifo cha Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa kuwapatia Waraka wa Kitume, “Fratelli tutti”, Meli ya amani na furaha ya kweli inayopaswa kusafiri sehemu mbali mbali za dunia, kwa ajili ya watu wote wa Mungu. Baba Mtakatifu ameweka saini katika nakala tatu: Nakala ya kwanza itahifadhiwa kwenye Pango Hifadhi ya Nyaraka za Vatican, Nakala ya pili imetolewa kwa ajili ya Idara la Uchapaji ya Vatican, (LEV) na nakala ya tatu, Baba Mtakatifu ameitoa kwa ajili ya Jalida la Mtakatifu Francisko wa Assisi, ambalo linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Hii ni zawadi mwanana, dira na mwongozo wa Jalida hili. Baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu amekutana na kusalimiana na watawa 65 wanaoishi katika konventi ya Mtakatifu Francisko wa Assisi.

Papa: Fratelli Tutti

 

04 Oktoba 2020, 13:13