杏MAP导航

Tafuta

2025.09.05 Tanzania,Watawa wa Mashirika ya Kike na kiume, Kanda ya Mlimani ya Mtakatifu Monica Lushoto, Tanga. 2025.09.05 Tanzania,Watawa wa Mashirika ya Kike na kiume, Kanda ya Mlimani ya Mtakatifu Monica Lushoto, Tanga. 

Lushoto,Tanzania:”Utawa na Maisha ya Familia vinategemeana !

Ni ndani ya familia wanapopatikana watawa na mapadre hivyo wanaowajibu wa kuziombea Familia,pale inaponekana kuwa mambo yanakwenda kinyume.Familia ni ushirika kati ya mume na mke.Ni tafakari ya Padre Tarimo,C.S.SP,kwa Watawa wa Mashirika ya Kike na kiume,Kanda ya Mlimani ya Mtakatifu Monica,Lushoto,waliunganika katika Jumuiya ya Masisita huko Mazinde Juu kwa ajili ya Sala,Misa na Mafundisho ili kukuza maisha ya kiroho ya ndani na ya Jumuiya zao.

Na Sr Paulina Mshana, UMTV na Angella Rwezaula – Vatican.

Watawa wa Mashirika ya Kike na kiume, Kanda ya Mlimani ya Mtakatifu Monica, huko Lushoto, waliunganika katika Jumuiya ya Masisita wa Mazinde Juu kwa ajili ya Sala, Misa na Mafundisho ili kukuza maisha ya kiroho ya ndani yao na ya Jumuiya zao. Kanda hiyo inaunganisha Mashirika mbali mbali  ya kike na kiume yanayofanya utume katika  Jimbo Katoliki la Tanga ambayo ni: Shirika la Masista wa Mama Yetu wa Usambara (COLU), Shirika la Wakarmeli, la Mtakatifu Teresa wa Mtoto Yesu, Damu Azizi, wakati mashirikia ya kiume: Warosmini(I:C), Wabenediktini(OSB), Shirika la Roho Mtakatifu(C.S.SP) na Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu(ALCP/OSS).Katika Misa Takatifu iliyofanyika tarehe 30 Agosti 2025 ilianza kwa maandamano ambayo yaliongozwa na Padre Thomas Akello, I.C akisaidiana na mapadre wengine.

Maandamano kwa ajili ya ibada na tafakari
Maandamano kwa ajili ya ibada na tafakari

Mada iliyochaguliwa na Padre Deus Tarimo(C.S.SP) katika siku hiyo  ilikuwa ni Utawa na Maisha ya Familia  jinis  vinavyotegemezana. Kwa mujibu wake alisema,  ili kuelewa tegemezi ya mambo hayo mawili   kwamba Familia ni kati ya mume na mke na Watoto ni zawadi ya familia. Familia ni msingi wa Kanisa na kiini cha Kanisa. Ni ndani ya familia wanapopatikana watawa na mapadre na hivyo wanaowajibu wa kuziombea Familia, pale inaponekana kuwa mambo yanakwenda kinyume. Akitoa mfano halisi wa watakatifu, aligusia sura ya Mtakatifu Monica, kwamba Mtakatifu alikesha akisali kwa miaka 17 huku akimwombea mwanaye ambaye alikuwa amepotoka katika Imani. Kwa sala zake na machozi mengi alifanikiwa kumrudisha mwanae, akabatizwa, akawa mtawa, Padre,  Askofu na leo hii ni Mtakatifu Agostino na  Mwalimu wa Kanisa. Padre Tarimo aliwasihi watawa, kusali, na kuwa na uvumilivu kama Mtakatifu Monica ambaye  ni Mama wa Familia, aliyeweza kuishi utakatifu wake ndani ya familia kwa uvumilivu na kumkabidhi mwanae na mumwe kwa Mungu. Kwa kifupi Padre alihitimisha akisema, “Utakatifu ni wito wa kila mmoja na utakatifu si kwa ajili ya watawa tu, bali kwa kila mtu anapaswa kusali kwa Imani na matumaini, bila kuchoka wala kukata tamaa kwa kufuata mfano wa Mtakatifu Monica.” Idhaa ya Kiswahili inakuletea, tafakari ya Padre Deus Tarimo kuhusu mada ya:

Watawa na maisha ya Familia.”

Tafakari kwa hii ni kwa lengo la  kujiimarisha zaidi katika utume wetu. Nilipokuwa na uongozi wa Kanda, wa kuandaa tafakari kwa ajili ya kushirikisha siku ya leo, nikaona umuhimu wa kuielekeza tafakari yetu ya siku ya leo katika suala zima la  “Familia,” na hasa  kwa kuangalia jinsi Utawa na Maisha ya Familia  vinavyotegemeana na kutegemezana,” (intedepence between the family and religious life) na hivyo basi, tuweze kuelewa vizuri ule utegemezi ambao upo kati ya hizi pande mbili za Utawa na Familia  kwa sababu kuna aja ya kuelewana na kukubaliana.

Padre Tarimo wakati wa kutoa tafakari kuhus Watawa na Familia
Padre Tarimo wakati wa kutoa tafakari kuhus Watawa na Familia

Tunapo zungumza familia tunamaanisha nini?

Familia ni ushirika kati ya mume na mke, kwa sababu mume na mke ndiyo wanaofanya familia. Ukiuliza kuhusu Watoto; watoto ni matunda ya familia, kwa hiyo kigezo cha familia si watoto, bali ni ushirika kati ya baba na mama, ushirika kati ya mume na mke, na ndicho kinachofanya familia na familia hiyo huwa inachukua sura nyingine, ya kuimarika na inapendeza zaidi pale ambapo mwenyezi Mungu anapotujalia zawadi, zawadi ya Watoto. Ni  katika hali hiyo ambapo Mtakatifu Yohane Paulo II, alisema kwamba: “familia ni msingi wa Kanisa, familia ni Kanisa dogo, familia ni shule ya sala,” kwa maana kwamba hatuwezi kuzungumzia Kanisa nje ya familia, na kwa sababu huwa tunasema kwamba, familia ni kiini cha Kanisa, lakini ni jambo ambalo daima tunapaswa, tuhimize, kuelimisha na kukumbushana kwamba familia ni kiini cha Kanisa.

Familia ni Kanisa dogo, msingi wa Kanisa, na shule ya sala

Kwa njia hiyo basi tafakari yetu ya leo itakuwa juu ya familia na maisha ya utawa. Lakini tutatumia mafundisho ya Mtakatifu Yohane Paulo wa II, kwamba “Familia ni Kanisa dogo, familia ni msingi wa Kanisa, familia ni shule ya sala, familia hiyo hiyo ndiyo kiini cha miito, au chimbuko la miito katika Kanisa. Kwa ugumu mwingi uliopo katika Kanisa,  kuna watu   watawa kama sisi, watu ni mapadre mashemasi,makatekista  na wengine wote, hayo ni matunda ya familia, hawajashuka kutoka mbinguni, wametoka kati yetu, wametoka ndani ya familia, kwahiyo tunapozungumzia sherehe, tafrija mbalimbali matukia mbalimbali kwenye Kanisa, kama upadrisho, tunapokuwa na nadhiri za utawa, labda pengine mmewahi kusikia wimbo wetu ambao umezoeleka, ule tunaoimba na kushangilia, tunashangilia mapadre wetu wapya, watawa wetu, wanadhiri wetu, kwa kuimba “Tunda la Kanisa hilo…” nafikiri tunaufahamu huo wimbo. … Sasa kuna baadhi ya waamini wetu wanapoimba huwa wakorofi kidogo, kwa sababu  huwa wanauliza ni tunda gani hilo? Je, ni parachichi, au chungwa au pera au ni ndizi? Ni tunda gani hilo? Sasa na mbaya zaidi,  wengine wanazidisha utani kwa kuimba “ndizi ya Kanisa hilo” wakifanya kama utani kwa ajili ya kuongeza shamra shamra kwenye sherehe.  Huo unaitwa utani wa gharama “expensive joke”. Kutoka na hilo ninataka  nianzie hapo kwenye utani wa gharama, katika kile nilichotaka kuwashirikisha siku ya leo kama watawa wenzangu, kwamba tukubali kuwa sisi ni matunda, matunda ya Kanisa, ambayo chimbuko lake ni katika familia. Kwa hiyo uwe ni embe, pera, parachichi, ndizi, uwe ni tunda Fulani.

Watawa wakiwa kwenye usikivu wa mada ya watawa na familia
Watawa wakiwa kwenye usikivu wa mada ya watawa na familia

Kwa mfano kuna tunda fulani huko ufilipino linaitwa “dulya” hilo tunda, lina miiba mirefu na mikali,  alafu linanuka lakini ni tamu sana,  kwa  hivyo hata kama wewe ni dulya utabaki kuwa ni tunda, kwa sababu utofauti wa tunda hauondoi hadhi ya tunda, tunda linabaki likiwa tunda pamoja na kwamba mengine ni makubwa, mengine ni madogo, mengine magumu, mengine ya miba mikali kama hilo “dulya”, mengine laini, mengine ni machungu, mengine matamu, mengine ya mti mkubwa mengine mti mdogo, mengine ni ya juisi nk… Kwa mfano chungwa kama tunda, lingine ukilikata lipo kama sponji lakini linabaki likiwa tunda, ile hadhi ya tunda haitoki inabaki kuwa tunda. Kuna siku moja tulikuwa mezani, mimi na wanovisi wangu, tukawa tunakula matunda mezani ambayo ni machungwa, kwa hiyo nilichukua chungwa nikalikata, lakini ndani lilikuwa sponji, wanovisi  wakawa wananiangalia wananicheka, wananiambia Father chukua lingine, walinionea huruma, lakini kabla sijachukua lingine mnovisi mmoja aliuliza hivi father, chungwa kama hili, linapokuwa hivi tatizo liko wapi? kosa ni la nani? Nila mkulima mwenyewe au ni la mti? Tuliishia tu kucheka… Sasa hili swali nililoulizwa na huyu mnovisi, tukilichukulia makini  katika kulitafutia jibu naamini tunaweza kugundua na kujifunza kitu.

"Nini Maana ya Tunda la Kanisa"

Je kinachofanya tunda lisiwe kama kile tunachotarajia ni nini? lazima kunakuwepo na kitu ambacho hakikwenda sawa. Mimi na wewe tunapotolewa na familia kama tunda la Kanisa, wakiwa wanatarajia kwamba tumeiva, tupo tayari kutumika katika jamii ya watu wa Mungu, swali ni kwamba kule tutakapopokelewa, watafurahia au watabaki kuguna na kujiuliza maswali? na tukirudi kwenye mfano ule ule wa chungwa, huyu mtawa sasa atakapokuwa na kasoro, swali litakuwa ni lile lile kwamba, kosa ni la nani? Kosa ni la mtawa mwenyewe au tatizo lipo kwenye malezi? au tatizo lipo kwenye familia? na hilo tutaulizwa, na pengine watauliza walezi wake huko utawani, hawakuwajibika ipasavyo, wakijiuliza maswali.  Sasa kwa nini matunda mengine watu wayafurahie lakini hili wasilifurahie? Shida ni kwamba hayakupata mbolea ya kutosha, kwamba hayakupata maji, hayakufanyiwa pruning au hayakufanyiwa matunzo? Ni kitu gani ambacho kinamfanya huyu mtawa awe wa hivyo?

Usikivu wa mada ya watawa na familia
Usikivu wa mada ya watawa na familia

Kwa nini mtawa huyo awe mkorofi, kwa nini mtawa huyu awe mvivu? na katika hilo “Barua ya Kwanza ya wakorintho 12:12-26, inatwambia kwamba “sisi sote ni viungo katika mwili mmoja,” lakini niwaambie ndugu zangu watawa, kuna malezi shirikishi na ni jambo la msingi sana katika kuandaa matunda bora ndani ya Kanisa. Wanaohusika katika malezi ya miito mbalimbali katika Kanisa, wasipofanya kazi bega kwa bega na wanafamilia kuna athari zake na hili suala si tu katika malezi ya familia hapana, kila mmoja wetu ana mchango wake katika hizi pande mbili za utawa na familia, kwa maana kwamba watawa wana wajibu wa kuchochea miito na malezi bora katika familia na wanafamilia nao wanapaswa washirikiane na walezi katika kukua, katika kuwasaidia na katika kuwaelekeza watoto kwenye wito wao ambao wameitiwa na Mungu. Mtakatifu Paulo kwa wakoritho akatuasa kwamba: “hakuna ambaye ni muhimu kuliko mwenzake” kwa maana kwamba, sisi sote ni viungo katika Kanisa, sasa katika vile viungo hamna ambacho ni muhimu au ni bora kuliko mwenzake, kwa maana kwamba sisi sote tunategemeana, katika ustawi wa Kristo,  ambao tumeuchagua, na mfano mkubwa alioutoa Mtakatifu Paulo ni huu wa malezi shirikishi,  kushilikiana katika kukuza miito katika Kanisa, kwa mfano anasema, “kama mwili wote ungekuwa jicho,” Paulo anauliza  “sikio lingekuwa wapi,” tungesikiaje, akauliza “mwili wote ungekuwa sikio, tungenusaje,” anatwambia Mtakatifu Paulo, na “jicho likimwambia moyo kwamba sikuhitaji ni nini kingetokea, kama kweli moyo utajitenga na kichwa kitakachotokea ni nini?”

Kushirikiana,upendo, kusaidiana na kuvumiliana

Kwa hiyo, kushirikiana, upendo, kusaidiana na kuvumiliana ni muhimu Ni muhimu kati ya watawa wenyewe na familia, kushirikiana na kutegemezana, kwa sababu mtawa ana nafasi kubwa sana ya kusaidia katika suala zima la malezi ya Watoto. Huyu mtawa anaweza kuchukua nafasi ya mzazi, huyu mtawa anaweza chukua nafasi ya mlezi pale alipo, iwe ni kanisani, iwe ni shuleni, iwe ni jumuiya ndogo hata katika familia, ule wakati tunaokuwa likizo nyumbani tulipozaliwa tuna nafasi ya pekee sana. Tunapopata kwa hiyo  nafasi ya kuwa katika familia zetu kwa nyakati fulani fulani, zile kasoro ambazo tunaziona katika familia zetu, na hata katika majirani zetu sio jambo la kufumbia macho, kusema kwamba mtajua na watoto wenu,  mimi sipo,  nyakati hizo ndugu zangu ndiyo fursa ya kuinjilisha, kwa sababu tusipo fanya hivyo, tutakuwa tunakosea Kanisa, tunalikosea haki katika suala zima la kuandaa matunda bora ndani ya Kanisa. Kwa njia hiyo, tusisahau kwamba sisi ni viungo, tunapaswa kuonesha ushirikiano wetu, kuonesha mchango wetu kwa kulea, kufundisha, kushauri, kuonya, kuombea familia zetu. Tunapaswa kuziombea familia zetu kwa sababu ndani ya familia zetu kuna watoto ambao ni wakorofi lakini utashangaa kuona kwamba watoto hao wakorofi, pale wanapokuwa kanisani, wanapopata msaada, wanapoelekezwa vizuri huwa wanabadilika, wanakuwa vyombo bora katika jamii, vyombo bora katika Kanisa. 

Miito ya Mapadre
Miito ya Mapadre

Nilipokuwa Uphilipino nilikuwa na Padre mwanashirika mwenzangu, Mnaigeria, ambaye daima alikuwa ananiambia hivi: “Father when I was younger I was very stubon, in the sense that when I ordained all the villagers came to witness, if it is true, that I ordained,” yaani “Nilipokuwa mdogo nilikuwa mtundu, kijiji kizima walikuwa wanajua na waliposikia kuwa napata upadrisho kila mtu aliacha mambo yake, kijiji kizima walikuja kushuhudia, mtoto wa Fulani amepadrishwa, ni kweli ni yeye, pasipo kuamini kama ni yeye.”  Lakini kilichomsaidia akafikia utawa, na akaweza kupata upadre na akawa padre mzuri na kufanya kazi kwa kufurahia ni malezi. Kwa hiyo malezi shirikishi ndiyo yaliyomtoa huko alikokuwa na yeye mwenyewe anakili. Ndugu zangu tunapokuwa katika utume na hasa malezi, malezi shirikishi shida inaanzia hapo, kwa hiyo mafanikio ya watoto wa wenzetu yanapaswa kuwa pia mafanikio yetu, furaha na matatizo ya familia fulani yanapaswa yawe ni ya wote.

Furaha ya familia ya Zakaria na Elizabeth na ndani ya familia zetu

Ukiisoma Injili ya Luka 1:56-57, ni kwamba “furaha ya familia ya Zakaria na Elizabeth ilikuwa ni furaha ya imani pia.” Injili inatwambia, wakafurahi pamoja naye,  alafu pale mwisho wa simulizi hiyo, hii familia ya Zakaria na Elizabeth, tunasikia jinsi ambavyo majirani hawa wanajionea mambo fulani fulani ambayo siyo ya kawaida, alafu wanapojionea mambo hayo wanajiuliza, mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Swali hili ndugu zangu ni swali la msingi sana kwa wanafamilia. Ni swali msingi sana kwetu sisi watawa, “mtoto huyu atakuwa wa namna gani?” kwa sababu hili ni swali ambalo siku za nyuma jamii ilikuwa ngumu kuuliza, na kufanyia kazi kwa uhuru. Leo hii ukiuliza swali hilo hilo kwa mtoto ambao siyo watoto wako, hasa sehemu ambapo kuna utata utata katika suala zima la malezi ukauliza mtoto huyu, atakuwa wa namna gani? Labda ni katoto kachokozi,kambea, kaongo, alafu unasema mtoto huyu atakuwa wa namna gani, ukauliza swali kama hilo, utaambiwa nenda uzae wa kwako umuulize swali… Kwa sababu siku hizi mtoto wa mwenzako siyo mtoto wako tena,  jamii inapoelekea, ukimuonya mtoto wa mtu ni matatizo, ukimwadhibu mtoto wa mtu unashtakiwa, ndipo tulipo sasa hivi, mtoto huyu atakuwa wa namna gani?

Miito ya upadre
Miito ya upadre

Tupende tusipende, tuna haja ya swali hilo katika kila hatua ya malezi. Katika familia zetu, mwelekeo wa watoto wetu tunaujua, hata katika makuu ya Mungu yanajidhihirisha kwa watoto wetu. Swali hili ni muhimu kuuliza,  ni muhimu kulifanyia kazi, kwa sababu watoto walipokuwa wadogo na wachanga, huwa tunawakumbatia, tunawabusu, lakini cha ajabu ni kwamba hawa watoto, ambao tunawakumbatia, na kuwabusu watoto hawa kesho wanaweza kuwa majambazi, maharamia(terrolist) na watoto hawa bado, kesho watakuwa watoto ambao ni muhimu ndani ya Kanisa, watakuwa watawa, mapadre, maaskofu, marais, na watakuwa wakuu wa mashirika. Swali kwa hiyo lililo ulizwa na Elezabeth na Zakaria ndugu zangu, tusilichukulie kuwa swali jepesi kwamba mtoto huyu atakuwa wa namna gani, mchango mkubwa ambao tunaoweza kuufanya sisi kama watawa, katika suala zima la usitawi wa familia zetu, ni kuuliza na kufanyia kazi swali hilo popote tutakapo kuwa katika utume wetu. Wale ambao utume wao upo mashuleni, wale wanaofanya utume wao malezini, maparokiani, na sehemu mbalimbali,  tuondoke na hili swali. Tukishirikiane katika hilo,  kuna uwezekano wa kuwa na matunda mengi ndani ya Kanisa na Taifa kwa ujumla.

Miito ya ndoa ya familia
Miito ya ndoa ya familia

Na nipende kutoa ufafanuazi, wa matunda bora, na hasa kwetu sisi watawa kwamba, tutambue tofauti zetu, tukisha tambua tofauti zetu, tupendane, tuvumiliane, tuchukuliane kwa upendo. Mimi nilipokuja utawani, sikujua kama nitakuja kukutana na fulani, au sista fulani, yeye ametoka zake huko, mimi nimetoka zangu kule, tumekuja kukutana utawani, familia ambaye ametoka huyo mtawa ni tofauti na familia yako, malezi ambayo ameyapata tangu utoto wake ni tofauti tofauti, lakini sote kama watunda ya kanisa, tunapaswa tuheshimiane, tusaidiane, tuvumiliane. Katika tofauti zetu, wakati mwingine unaona tunda kwa mara ya kwanza ambalo hukuwahi kuliona, unalichukia bila sababu, na huwa inatokea, halijakudhuru na halijakufanyia chochote,  ni basi tu hujampenda. Haya ni mambo ambayo yanajitokeza katika utawa wetu, yapo na madhara yake hayaishii katika nyumba zetu za kitawa yanaathiri mpaka zile familia zetu, yanaathiri mpaka Kanisa kwa ujumla, madhara yake ni makubwa.  Mema na mazuri kwa hiyo ambayo yanaonekana kwetu sisi kama watawa ni kivutio, huwavutia na kuwatia nguvu zaidi katika kujiunga na maisha ya wakfu, kujiunga na maisha ya utawa kwa sababu wanasema “kizuri cha jiuza na kibaya cha jitembeza.”

Kusaidiana kubeba misalaba yetu
Kusaidiana kubeba misalaba yetu
Malezi ya watoto
Malezi ya watoto

Kwa jinsi hiyo hiyo katika maisha ya ndoa, maisha ya familia, ndiyo hivyo hivyo maisha yetu ya utawa yana changamoto zake, hakuna maisha bila changamoto, walio katika maisha ya ndoa wakisikia kuwa kuna madhaifu au udhaifu katika maisha ya utawa,  wanashangaa, hawaamini. Hivyo basi, sote tunajua kwamba hakuna mtu ambaye ni mkamilifu, tunahitaji zaidi kutegemezwa na sala. Sala za familia, wanafamilia yetu, na sisi pia tunao wajibu wa kuwaombea kwansababu sote tunatafuta utakatifu. Tukitambua kwamba familia zetu zina changamoto pia, sala za mtawa zina nafasi kubwa sana, mtawa mmoja akasema kwenye familia za mapadre kuna kushikana vichwa sana… sijui kama ni kweli. Mambo mengi hayasemwi ili tuyachukuliye  uzito, tuyafanyie kazi na yatatusaidia sana na Baraka za mwaka huu Mtakatifu, wa Jubilei 2025, kwa sababu Jubilei ni mwaka wa kuachilia, ni mwaka wa uhuru, ni mwaka wa kuchangamka. Tuombeane kwa hiyo siku ya leo katika nchi yetu, tuziombee familia zetu, tuwaombee watawa wenzetu popote walipo katika utume, bila kusahau wanafunzi wetu ili waongozwe na Roho Mtakatifu katika safari yao ya malezi, ili waweze kuwa chombo cha matumaini, chombo cha faraja katika familia zetu, tuoyeshe kwamba sisi ni mahujaji wa matumaini.

Tumsifu Yesu Kristo.

Jubilee 2025……,

Mahujaji katika matumaini           

 

05 Septemba 2025, 14:52