杏MAP导航

Tafuta

Huko  circo massimo katika Jubilei  ya Vijana  Roma vijana walipata fursa ya kukaribisha sakramenti ya kitubio Huko circo massimo katika Jubilei ya Vijana Roma vijana walipata fursa ya kukaribisha sakramenti ya kitubio 

Dominika ya 23,Mwaka C:“Kujenga kwa Hekima,kusamehe na kubeba mzigo wa huduma”

Katika Jubilei ya Matumaini,tumaini letu linapatikana pale tunapopanga kwa hekima,kusamehe kwa moyo,na kujitoa bila kutarajia malipo kwa sababu tunajenga kwa moyo wa huduma,sio kwa uchu au sifa.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio vatican leo Dominika ya 23 Mwandishi wa somo la kwanza Mwandishi anashauri: kabla ya kusafiri, fikiri hatua zako; usije ukajikuta umetumalika bila mipango. Maamuzi ya maisha, kama familia, kazi, imani, yanayohitaji umakini. Hekima huanza na mchakato wa kupanga Hekima 9:13–19. Paulo anamtumia Filemoni maneno ya kiasi cha furaha kinachosababisha msamaha. Anamhimiza kuachilia Onesimu kama kaka, si mtumwa. II –( Flm 9-10, 12-17.) Kwa kawaida tunafurahi makanisa yanapojaa waamini, tunajisikia vizuri na kuona ni dalili njema ya wongovu, dini imekolea na ufalme wa Mungu umetufikia. Hizi ni fikra nzuri, hakuna anayefurahi wenzetu wanaporudi nyuma katika imani na kupoa kidini au mwenzetu akiwa anahangaika katika makanisa na misikiti bila kuwa na msimamo wa imani yake hivi tunapokuwa wengi Kanisani ni hamasa kubwa, na dalili hiyo ni waamini kuwa wengi hadi kukosa nafasi ya kuketi...

Ibada ya upatanisho

Ibada ya upatanisho   (ANSA)

Tunapofurahia jambo hili kwa Kristo ni kinyume kabisa, uwingi wa wanaomfuata unamuogopesha na kumpa mashaka... daima amewaona wafuasi wake kama kundi dogo “Msiogope enyi kundi dogo kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme” (Lk 12:32), pia ameulinganisha ufalme wa Mungu na vitu vidogovidogo mfano hamira kidogo lakini inayoumua unga mwingi, mbegu ya haradali nk.. ndio maana leo anashangaa anapoona umati mkubwa unamfuata... Yupo safarini kuelekea Yerusalemu, haendi Ikulu kuwa mfalme, haendi vitani kupigana ili kutafuta nchi ya kuitawala, hapana, anakwenda kuteswa, kufa na kufufuka atukomboe. Umati huu ulimfuata Yesu bila kujua lengo halisi la ufuasi wao ni nini? Wengi walimfuata walau wajipatie ahueni ya shida zao, wengine wakitaka uponyaji, wengine wakitamani kushiba mikate na samaki, wapo waliotaka tu kumsikia, baadhi ya akina mama walimpenda tu na kutamani kumuona na kuongea naye mawili au matatu nk kila mmoja na nia yake... hata hivyo hoja ya msingi ya kumfuata Yesu umati mkubwa vile ilikuwa ni nje ya lengo halisi la ufuasi wa kweli.

Sisi tunapoogopa kupoteza waamini na kufurahi wanapofika kwa wingi Kanisani Yesu anaogopa wanapokuwa wengi... ndipo anapowageukia umati huo na kuwapa masharti matatu wanaotaka kumfuata. Mosi ni kuwachukia baba, mama, mke na ndugu wote kwa ajili ya Injili... Pili ni kuubeba msalaba kama alivyobeba Yeye... na tatu kuacha vyote tulivyo navyo... kwa kila agizo mara zote tatu anasisitiza tusipofanya hivyo hatuwezi kuwa wanafunzi wake. Yesu anatuuliza ikiwa tunapanga kujenga kitu cha maana, iwe: nyumba, uhusiano, utume, tutahesabu gharama? Nani yupo tayari? Kujenga imani au huduma kunahitaji kupima gharama: muda, afya, utajiri, uamuzi mgumu. hasa ukizingatia watu wa jamii moja wanavyopendana! kisha uanze tu kuwachukia ndugu, kweli! Kwa nini Yesu anatoa sharti gumu namna hii? Linapokuja suala la ufuasi wa kweli msimamo wa Kristo umekuwa imara kabisa, lakini ni kweli anatudai kuwachukia ndugu? Mbona amehimiza sana upendo, kwamba kumpenda Mungu na jirani ndio amri kuu? na vipi kuhusu amri ya 4 ya Mungu? tunamshangaa, anatushangaa, tunajaa ‘ushangazi’ na kuchanganyikiwa...

UFAFANUZI: Hayati Papa Francisko alisema Jubilei ichunge moyo wa kanisa: kuchukua jukumu, kujenga jamii ya unyenyekevu, huruma, na uwazi. “Tumaini halihusiani na mambo yenye matokeo yanayokutana—we, tukimbie kurudi kwa ule mlango wa hekima na huduma.” Mwamini usiogope, Neno la Kristo ni jema kabisa, kwamba tuondoe vikwazo, ikibidi hata watu au vitu vinavyotuzuia na kutuchelewesha kuingia mbinguni sababu hakuna upendo duniani wa kumlinganisha na Mungu... kuwa wengi tu haitoshi sababu inawezekana kumfuata Yesu kwenye kundi bila kuwa mfuasi, kuwapo kwenye kambi ya jeshi bila kuwa mwanajeshi, kuketi na wanakwaya bila kuwa mwanakwaya... ‘Mwalimu mmoja ‘aliambiwa fulani amesema zamani alikuwa mwanafunzi wako’, akajibu akisema “Inawezekana alihudhuria vipindi vyangu lakini hakuwa mwanafunzi wangu!” kumbe inawezekana tukawepo hapa kanisani bila kuwa waamini.

Ibada ya Upatanisho

Ibada ya Upatanisho   (ANSA)

Ukristo ni msalaba na wala hakuna lelemama. Na iwapo kweli katika uwingi wetu tumeamua kumfuata Kristo halafu tujitoe kwa moyo wote, hili ni agizo nayo ni kanuni... kuacha tulivyo navyo inahusisha kujitoa bila kujibakiza, kuwaka na kuteketea ili kuangaza, ikibidi kuvuja jasho na damu ili Injili ya Msulibiwa isonge mbele. Kwa kutenda hivi tunaweka mtaji, tunawezekeza, tunakuwa watu wa mahesabu, tunajihakikishia uzima wa roho zetu na huo ni werevu. Kinyume chake tutafanana na hawa jamaa aliotusimulia Kristo leo, mmoja anaanza ujenzi wa mnara (ilikuwa ni kawaida kwenye shamba la mzabibu kwa ajili ya ulinzi) bila kuwa na mtaji na kutofanya makisio (BOQ) ipasavyo, anashindwa kuumaliza watu wanamcheka. Kwenye sebule fulani kuna maneno “Mtaji wa mjinga ni majungu, wa mpumbavu ujinga, wa mvivu usingizi, wa majirani umbeya, wa jehanum ni dhambi, wa dhambi ni mauti, wa masikini ni nguvu zake mwenyewe, na wa mtu wa Mungu ni maombi”.

Mtaji wa mkristo ndio huo wa kuwa tayari kuwaacha hata ndugu wanaoleta vikwazo katika kumpenda na kumtumikia Mungu. Huyu aliyeshindwa kumaliza ujenzi wa mnara alichekwa na wote na hili linaweza kutukuta hata sisi, tukachekwa! ‘Ukitaka kumuwinda simba choma kwanza chini kwa mkuki wako, ukiona hauchomi chini acha kuwinda kalime’... ufuasi ni mtaji, ni kuwekeza. “Kujenga Kwa Hekima, Kusamehe Na Kubeba Mzigo Wa Huduma …” katika kila kipengele cha maisha tuwe watu wa mahesabu na wenye mitaji, wanatucheka kuwa tumeshindwa kumalizia mnara, ndipo hupayuka “Haa, wewe si ulikuwa kanisani, mbona sasa umelewa hivi?” au “Jamani, yaani unampiga hivi mkeo wakati umevaa rozari!” au “Wee baba nanihii, mbona unawahi Kanisani wakati hujaacha fedha hata ya chai?” hapa Kanisa ni kisingizio, tutachekwa!

Wakati wa kujipatanisha na Mungu

Wakati wa kujipatanisha na Mungu

Wanaotamani ndoa nao ni lazima wahesabu gharama, ndoa sio jambo dogo, ni maisha... ujenzi wa mnara wa ndoa unadai mtaji wa uhakika, tusije kuchekwa baadaye kuwa tuliuanza ujenzi huu kwa mbwembwe na kuishia kwenye ‘renta’ tu. “Kujenga Kwa Hekima, Kusamehe Na Kubeba Mzigo Wa Huduma tufanye hesabu na kuweka mtaji mbinguni kwa kudhibiti hasira na chuki, umbea na masengenyo, wivu na kijicho (jifunze kutunza mema ya wengine pia, wasaidie wenzako wafanikiwe), kutotumia muda mwingi kuhukumu wengine (tafakari juu ya huruma ya Mungu kwako), kutokata tamaa au kuwakatisha wengine (uwe jasiri, imarisha wengine pia), kutokuwa mlalamishi, kutokunung’unika na kutoridhika, kukataa kinyongo na kisasi, ufujaji fedha, kutokuwa kero kwa yeyote, udanganyi na uzushi (YbS 20:24, 4:7a).

Badala yake ‘ili tusichekwe’… tuungane na Mfalme Sulemani katika kukubali udhaifu wetu na kuomba paji la Hekima (somo I- Hek 9:13-19). Hekima hiyo ituongoze kulishika neno la Mt. Paulo katika somo II (Flm 9-10,12-17) akimuomba Filemoni ampokee tena dogo Onesmo aliyekuwa na kaukorofi kidogo ka utoro, ampokee kama ndugu katika Kristo na sio kama mtumwa... Filemoni alikuwa rafiki ya Mt. Paulo, jina hilo Filemoni  “philein” lina maana ya “kupenda”, “philema” ni ‘kubusu/kukumbatia”, “philos’ maana yake ‘mpendwa”... shime ndugu zangu tuufuateni upendo… upendo hujenga [1Kor 8:1], …kama sina upendo hainifaidii kitu (1Kor 13:3), …upendo huvumilia, hufadhili, hauhusudu, hautakabari, haujivuni [1Kor 13:4] basi na tupendane... tujue kwa nini tunamfuta Yesu? kwa nini tumekuja kwake? tumsikilize, tumtii, tushike maagizo yake, naye Mungu Mwenyezi atusaidie, tukue na kuongezeka imani, kwa huruma yake kuu atustahilishe utakatifu wa kweli, kusudi watu wasitucheke kuwa tumeanza kujenga na tumeshindwa kukamilisha,

Dominika ya 23 Mwaka C inatuita, Je, tumejijenga kwa hekima? Tumehesabu gharama ya moyo kupenda na kujitoa kuwa ustawi wa jirani na mimi mwenyewew? Tumejenga uhusiano wa huruma kwa wote na kujali utu na ubinadamu hasa katika kutafuta Mungu? Katika Jubilei ya Matumaini, tumaini letu linapatikana pale tunapopanga kwa hekima, kusamehe kwa moyo, na kujitoa bila kutarajia malipo kwa sababu tunajenga kwa moyo wa huduma, sio kwa uchu au sifa. Amina.

Lirurujia ya Dominika ya XXIII Mwaka C
06 Septemba 2025, 09:35