杏MAP导航

Tafuta

2025.09.05 Injili ya Dominika ya  XXIII ya mwaka C. 2025.09.05 Injili ya Dominika ya XXIII ya mwaka C. 

Dominika ya 23 Mwaka C:Mungu anajifunua Yeye na thamani ya Msalaba

Katika sehemu ya Injili ya Dominika ya 23,Yesu anafundisha kuwa kumfuata Yeye,njia ya kuelekea uzima wa milele,ni kujitoa sadaka na kuacha yote yanayokinzana na kumfuata Yeye ikiwa ni pamoja na ndugu,jamaa na marafiki.Fundisho hili halipingani kabisa na Amri mpya ya mapendo na Amri ya nne ya Mungu,kuwaheshimu Baba na Mama,bali ni kututahadharisha kuwa ndugu,jamaa,marafiki na jirani wakiwa kikwazo katika kuitikia wito wa kuwa watakatifu,tunapaswa kujitenga nao kuliko kwenda kinyume na mapenzi Mun

Na Padre Paschal Ighondo –Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya XXIII ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatuelekeza kuomba hekima ya Mungu ituongoze katika maisha yetu, umuhimu wa kuheshimiana na kuthaminiana sisi kwa sisi, kwa maana mbele za Mungu sisi sote tuko sawa, na tumefanywa kuwa wana huru kwa njia ya Msalaba wa Yesu Kikristo. Ni katika muktadha huu Wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii unasema; “Ee Bwana, wewe ndiwe mwenye haki, na hukumu zako ni za adili. Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako (Zab. 119:137, 124). Naye mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Mungu, umetuletea ukombozi na kutufanya watoto wako. Ututazame kwa wema sisi wanao wapenzi, utujalie uhuru wa kweli na urithi wa milele sote tunaomwamini Kristo.”

Somo la kwanza ni kitabu cha Hekima ya Sulemani (Hek 9:13-18). Somo hili ni sehemu ya sala ya Mfalme Sulemani akiomba Hekima ya Mungu imuongoze katika kutambua mpango wake na kuwaongoza watu wake katika kweli na haki. Katika kuomba ufunuo wa Hekima ya kimungu, Sulemani anauliza maswali manne akionesha jinsi uwezo wa mwanadamu ulivyo mdogo katika kufahamu yaliyo mema kwa hoja kuwa hata yaliyoko duniani, karibu nasi ni shida kuyaona na kuyapambanua. Anahoji hivi; “Ni mtu yupi anayeweza kulijua shauri la Mungu? Au ni nani anayeweza kuelewa mapenzi yake? Mambo yaliyoko mbinguni ni nani anayeweza kuyagundua? Ni yupi anayeweza kuyavumbua mashauri ya Mungu? Anatoa jibu kuwa ni Hekima ya kimungu na nguvu Roho Mtakatifu, vinaweza kumsaidia mwandamu kuyatambua haya. Nasi daima tumwombe Roho Mtakatifu ili atuongoze vyema katika kuyatumbua mapenzi ya Mungu na kuyatimiza, atusaidie katika shughuli zetu pale changamoto na magumu yakitokea tuweze kung’amua namna iliyo sahihi ya kuyatatua. Hii ni kwa kuwa mawazo yetu wanadamu yana woga, na makusudi yetu yanaelekea kushindwa; na mwili wenye uharibifu huigandamiza roho, na kiwiliwili cha kidunia huzilemea akili zilizosongwa na masumbuko.

Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu kizazi baada ya kizazi. Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo, rudini, enyi wanadamu. Maana miaka elfu machoni pako, ni kama siku ya jana ikiisha kupita, na kama kasha la usiku. Wawagharikisha, huwa kama usingizi, asubuhi huwa kama majani yameayo. Asubuhi yachipuka na kumea, jioni yakatika na kukauka. Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima. Ee Bwana, urudi, hata lini? Uwahurumie watumishi wako. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako, nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote, na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu, na kazi ya mikono yetu uithibitishe” (Zab. 90:1, 3-6, 12-14, 17).

Somo la pili ni la barua ya mtume Paulo kwa Filemoni (Fil. 9-11, 12-17). Mtume Paulo alimwandikia Filemoni barua hii, akiwa mfungwa mjini Roma, kwa ajili ya imani yake kwa Kristo. Katika barua hii Mtume Paulo anamsihi na kumshauri Filemoni ampokee Onesmo, si kama mtumwa tena kwake, bali kama ndugu katika Kristo, maana kwa ubatizo sisi sote ni ndugu. Itakumbukwa kuwa nyakati hizo, katika milki na utawala wa Kirumi kulikwa na “watu huru” na “watumwa”. Kama ilivyo hata sasa, nyakati hizo maisha ya mtumwa yalikuwa mikononi mwa Bwana wake. Mtumwa aliweza kununuliwa, kuuzwa na hata kuuawa akionekana hana faida tena kwa sababu yoyote ile kama vile ugonjwa, uzee, au kilema.

Lakini Filemoni alikuwa nani hasa? Filemoni alikuwa kijana tajiri wa Kolosai. Mtume Paulo alimlea katika Imani akawa Mkristo mwema na Jumuiya ya kikristo ikawa inakusanyika nyumbani kwake kusali. Kama mtu huru na tajiri, alikuwa na watumwa wake, mmoja wao akiwa Onesmo. Mapokeo yanasema kuwa Onesmo aliiba fedha kwa Filemoni na kutoroka. Katika kukimbia kwake alijikuta mjini Roma. Baada ya kuishiwa fedha alizoiba, kama mwana mpotevu, alienda kujisalimisha kwa Mtume Paulo akiwa katika kifungo huru cha nyumbani, lakini chini ya uangalizi wa askari (Mdo 28:30). Mtume Paulo alimpatia Onesmo hifadhi kwa muda, akamfundisha imani ya kikrito, akamsaidia kutambua makosa yake, akafanya toba, na kumbatiza. Onesmo alionja upendo wa Mtume Paulo na hivyo alijitoa kikamilifu kumtumikia, naye akampenda sana. Lakini baadae aliamua kumrudisha kwa Bwana wake Filemoni kwa sababu alikuwa bado na chapa ya utumwa na kisheria alipaswa kumrudisha. Na kwa kuwa Onesmo alitoroka na zaidi sana aliiba, adhabu yoyote ilikuwa halali kwake, hata ya kifo. Ndiyo maana Mtume Paulo anapomrudisha kwa Filemoni hamuachi aende peke yake, bali anamtuma Tikito amsindikize akiwa na barua ya mbili, moja kwa Filemoni na nyingine kwa jumuiya ya Kikristo ya Kolosai (Kol. 4: 7-9).

Barua hii Mtume Paulo aliiandika kwa mkono wake mwenyewe (Film 1:19), sio kwa mkono wa Katibu wake, ili kuonesha msisitizo na umuhimu wa ujumbe wake wa kumsihi na kumwomba Filemoni ampokee Onesimo kama ndugu katika Kristo na aweze kumpiga chapa ya kumfanya mtu huru (Film. 1:16), kadiri ya sheria ya Kirumi, mtu mwenye watumwa alikuwa na uwezo wa kumuweka huru mtumwa wake, kwa kumpatia hati ya uhuru, akisisitiza kuwa; mbele ya Mungu hakuna mtu huru na mtumwa, kwa kuwa Kristo amewaweka watu wote huru kutoka utumwa wa dhambi, na kutufanya sote wana wa Mungu kwa sakramenti ya ubatizo. Naye Paulo yuko tayari kumlipa Filemoni chochote anachowiwa Onesmo (Film. 1:18). Jina Onesmo, asili yake ni lugha ya Kigiriki, likimaanisha “Anayefaa”. Mtume Paulo analitumia Jina hili na kumwambia Filemoni kwamba mtumwa wake alikuwa hafai kwa chochote, lakini sasa, anamfaa sana, kama ndugu katika Bwana (Film. 1:11).

Na katika barua kwa Jumuiya ya kikristo ya Kolosai, Mtume Paulo anawaasa Wakristo wanaomiliki watumwa akiwaambia: “Ninyi wakuu, watendeeni watumwa wenu kwa uadilifu na haki, mkikumbuka kuwa nanyi pia mnaye Bwana mbinguni” (Kol 4:1). Ni katika muktadha huu barua za mtume Paulo zikawa kichochoe cha kupinga biashara ya utumwa, ambayo ni ya aibu kabisa. Nasi tuone ubaya wa biashara haramu ya binadamu na tuweke nia dhabiti ya kupambana nayo na kuikomesha, kwani sote tulikuwa watumwa katika dhambi, nasi tumekombolewa kwa thamani ya Damu Azizi ya Yesu Kristo iliyomwagika Msalabani.

Kujitoa sadaka kama mwanakondoo
Kujitoa sadaka kama mwanakondoo

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 14:25-33). Katika sehemu hii ya Injili Yesu anafundisha kuwa kumfuata Yeye, njia ya kuelekea uzima wa milele, ni kujitoa sadaka na kuacha yote yanayokinzana na kumfuata Yeye ikiwa ni pamoja na ndugu, jamaa na marafiki. Fundisho hili halipingani kabisa na Amri mpya ya mapendo na Amri ya nne ya Mungu, kuwaheshimu Baba na Mama, bali ni kututahadharisha kuwa ndugu, jamaa, marafiki na jirani wakiwa kikwazo katika kuitikia wito wa kuwa watakatifu, tunapaswa kujitenga nao kuliko kwenda kinyume na mapenzi Mungu. Hii ndiyo gharama gharama ya imani yetu kwa Kristo, isiyoeleweka kwa walimwengu kwa maana; “Ujumbe wa msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu…upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu (1Kor 1:18, 25).

Katika kufikisha ujumbe huu, Yesu anatoa mfano wa umuhimu wa kuhesabu gharama kabla ya kuanza kujenga mnara, na mfalme anayetaka kwenda vitani kufanya tathimini ya uwezo wake akiulinganisha na wa adui yake. Hii ndiyo kusema kuwa maamuzi ya kutaka kuingia katika ufalme wa Mungu yanahitaji hekima, busara, umakini, ukomavu na uvumilivu ili kuvishinda vishawishi na vikwazo. Na ni hekima ya Mungu ndiyo inayoweza kutufahamisha haya yote kwa maana; “Mawazo ya Mungu si mawazo yetu, na njia zake si njia zetu kama mbingu zilivyo mbali na dunia ndivyo yalivyo mawazo ya Mungu na yetu”. Na ili kuyaelewa mambo haya na kupata matunda yake hatuna budu kumruhusu Roho Mtakatifu atuongoze.

Basi na tuufuate ushauri huu wa Mtume Paulo; “Basi nasema hivi, mwenendo wenu na uongozwe na roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia. Matokeo ya kuongozwa na roho ni Mapendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi (Gal 5:16, 22-25). Nasi tumwombe Roho Mtakatifu ayafungue macho ya mioyo yetu ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea Dhabihu anasali hivi; “Ee Mungu, uliye asili ya ibada ya kweli na amani, tunakuomba utuwezeshe kukuheshimu vema kwa sadaka hii na kwa kulishiriki fumbo hili takatifu tuunganike kabisa tuwe moyo mmoja”. Kristo Yesu katika antifona ya Komunyo anasisitiza; “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu; Yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima” (Yn. 8:12). Na katika sala baada ya komunyo mama Kanisa anasali hivi akituombea; “Ee Bwana, sisi waamini wako umetulisha neno lako na kututia uzima kwa chakula cha sakramenti hii takatifu. Utuwezeshe kuendelea kwa msaada wa neema nyingi za Mwanao mpenzi, hata tustahili kushirikishwa daima uzima wake”. Na hili ndilo tumaini letu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari ya Dominica ya 23 ya Laudato si
04 Septemba 2025, 18:01