杏MAP导航

Tafuta

Carlo Acutis alielewa maana hii ya kina ya Ekaristi Takatifu si kwa kusoma vitabu tu bali kwa kuishi kwa moyo wake wote. Carlo Acutis alielewa maana hii ya kina ya Ekaristi Takatifu si kwa kusoma vitabu tu bali kwa kuishi kwa moyo wake wote.  

Carlo Acutis kijana Mkatoliki aliyeishi Ekaristi kama Barabara ya kwenda Mbinguni

Ekaristi Takatifu ndiyo kitovu cha maisha ya Mkristo na Kanisa.Katika adhimisho hilo,Kanisa linapata utakaso wa Mungu kupitia Kristo,na binadamu hutoa ibada yao kwa Mungu Baba.Ndani ya Ekaristi Takatifu Kristo yupo kwa njia ya ajabu na kwa Kristo,pamoja na Kristo na ndani ya Kristo tunaunganishwa naye hadi kwa Baba.Carlo Acutis alikutana na Kristo Yesu si tu kama fundisho, bali kama Rafiki wa kweli,Mwalimu,Mwokozina Sababu ya maisha yake.

Na Sarah Pelaji

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican tusikilize simulizi maalum la Padre Arturo Elbert, Mjesuit S.I kuhusu maisha ya Carlo Acutis katika miezi ya kwanza ya mwaka 2006, wakati wa alipokuwa akihitimu masomo yake huko Roma, nchini Italia ambapo alipata nafasi ya kutembelea Chuo cha Leo XIII kilichopo Milano Italia, kinachosimamiwa na Shirika la Kijesuit (Compagnia di Gesù). Padre wa Kiroho wa chuo hicho, alimuonesha kijana mmoja kati ya wanafunzi wengi wa chuo hicho na kusema, “Huyu ni kijana mwenye kujitolea katika maisha ya kiroho na mwenye tabia ya furaha ya kudumu.” Kijana huyo alikuwa Carlo Acutis. Baada ya miezi michache, Carlo alifariki dunia. Miaka iliyofuata, baada ya kusikia sifa za utakatifu wa kijana huyo, Elbert anaeleza kuwa alipata nafasi ya kujifunza zaidi kuhusu maisha yake kupitia wasifu wa Carlo Acutis pamoja na tafiti mbalimbali zilizofanywa juu yake. “Ndipo nilipogundua kuwa alikuwa ni kijana wa kipekee ambaye alipenda kutumia ujuzi wake wa kompyuta kwa ajili ya huduma kwa Mungu.

Carlo Acutis alipenda Yesu
Carlo Acutis alipenda Yesu   (ANSA)

Akiwa na rafiki yake aliyekuwa mwanafunzi wa uhandisi wa kompyuta, alianza kutengeneza na kusimamia tovuti ya Parokia yake. Mwaka huohuo alibuni tovuti mpya kwa ajili ya mradi wa kujitolea wa Chuo cha Leone XIII, akiandaa pia matangazo ya video yaliyotengenezwa na wanafunzi mbalimbali kwa shindano la kitaifa. Alitumia likizo yake ya kiangazi mwaka 2006 kubuni tovuti hiyo kwa moyo wote. Alikuwa pia ameandaa tovuti ya “Pontificia Accademia Cultorum Martyrum.” Carlo alikuwa maarufu kwa ucheshi wake ambao uliwavuta marafiki wake wengi kuwa karibu naye. Alitambuliwa sana kupitia vipaji vyake vya kiufundi ambavyo alivitumia kuwasaidia wenzake na watu wengine waliokuwa na uhitaji. Lakini kilichomtofautisha na vijana wengine wengi wa rika lake ni kitu kimoja: upendo wake kwa Yesu Kristo.

Carlo siku ya kutangazwa mwenyeheri
Carlo siku ya kutangazwa mwenyeheri

Upendo wa Carlo kwa Yesu

Tangu akiwa mdogo, Carlo alikutana na Kristo Yesu si tu kama fundisho, bali kama Rafiki wa kweli, Mwalimu, Mwokozi, na Sababu ya maisha yake. Bila Yesu, haiwezekani kuelewa maisha ya Carlo. Ingawa alikuwa kama vijana wengine, moyo wake ulihifadhi fumbo kubwa na la kipekee. Kwa msaada wa viongozi wake wa kiroho, Carlo alijikita katika nguzo kuu mbili za maisha ambazo ni Ibada kwa Ekaristi Takatifu na Ibada kwa Mama Bikira Maria. Alikuwa akihudhuria Misa kila siku na kutumia muda mwingi katika sala ya kimya mbele ya Tabernakulo. Alisema mwenyewe kwa Padri wake wa Kiroho: “Kutoka katika Fumbo la Ekaristi, najifunza upendo usio na kipimo wa Bwana Yesu Kristo kwa kila mtu.” Kwa Carlo kuwa mtu mwema hakutoshi bali aliona hitaji la kujitoa kwa Mungu na kuwatumikia ndugu zake. Ndipo pale alipoanzisha juhudi zake za kimisionari kwa ajili ya wokovu wa roho za watu hasa wale waliokuwa mbali na Mungu.

Carlo Acutis wakati wa moja ya siku kuu  ya kuzaliwa kwake
Carlo Acutis wakati wa moja ya siku kuu ya kuzaliwa kwake

Alikuwa akitoa sadaka, sala na toba kwa ajili ya dhambi za watu dhidi ya Upendo wa Mungu, hasa dhidi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu aliye hai katika Ekaristi Takatifu. Kauli yake maarufu inayojulikana hadi leo ni: ‘Ekaristi Takatifu ni barabara yangu ya haraka kuelekea mbinguni.’ Ushuhuda wa watu waliomfahamu Mwenyeheri Carlo Acutis: Federico Oldani ambaye ni rafiki wa Carlo wa shule ya sekondari, alithibitisha kuwa imani ya Carlo ilikuwa thabiti na ya kuheshimu wengine, akimtaja kuwa mfano kwa vijana wote wanaotamani kuwa wafuasi wa kweli wa Kristo Yesu. Padre Roberto Gazzaniga, mmoja wa Mapadri waliomfahamu karibu, alisema kuwa ni kwa sababu ya imani ya ajabu, Carlo aliweza kuendesha juhudi za uinjilishaji katika mazingira aliyokuwamo kila siku. Ushuhuda wake haukuwa maneno tu, bali maisha yaliyojaa Ibada ya kweli kwa Ekaristi, kwa Sakramenti Takatifu kwa Bikira Maria na kwa Kanisa la Kikatoliki.

Ekaristi na Utambulisho wa Mkristo

Ekaristi Takatifu ndiyo kitovu cha maisha ya Mkristo na Kanisa. Katika adhimisho hilo, Kanisa linapata utakaso wa Mungu kupitia Kristo, na binadamu hutoa ibada yao kwa Mungu Baba. Ndani ya Ekaristi Takatifu Kristo yupo kwa njia ya ajabu na kwa Kristo, pamoja na Kristo na ndani ya Kristo tunaunganishwa naye hadi kwa Baba. Ekaristi si tu kumbukumbu ya Karamu ya Mwisho, bali ni ukumbusho hai wa sadaka ya msalaba mahali ambapo Yesu alijitoa kwa Baba na Baba alimfufua kwa nguvu ya Roho. Katika Ekaristi Takatifu Kanisa linapita kutoka dunia hii kwenda kwa Baba wa milele kwa njia ya Roho Mtakatifu. Ni tendo la ushirika la agano kati ya Mungu na watu wake. Ndiyo maana, tendo la waumini haliwezi kutenganishwa na tendo la Mungu mwenyewe. Kuhubiri upande mmoja tu wa tendo la Mungu au wa tendo la waumini ni kulipotosha fumbo hili. Ekaristi ni tendo la sadaka, la ushirika na la ukuhani wa Kristo Yesu. Carlo Acutis alielewa maana hii ya kina ya Ekaristi Takatifu si kwa kusoma vitabu tu bali kwa kuishi kwa moyo wake wote. Alielewa kuwa katika Ekaristi, Kristo yupo kweli. Na hiyo ndiyo sababu alipenda kuwa karibu na Yesu kila siku. Kwa vijana wa leo, maisha ya Carlo ni mfano hai kwamba utakatifu unawezekana hata katika enzi ya teknolojia. Alitumia kipawa chake kwa ajili ya Mungu na akatambua kuwa, kuzaliwa wote huzaliwa kama asili ya kipekee, lakini wengi hufa kama nakala. Kwa upande wa Carlo aliamua kuwa asili halisi, ya Kristo aliyemtawala moyo wake.

Carlo wakati akiwa mdogo
Carlo wakati akiwa mdogo   (Divulgação Lumine)

Mtakatifu Chipukizi

 Carlo Acutis, Mfano wa Imani Hai kwa Vijana wa Karne ya 21. Katika nguvu ya Roho Mtakatifu, Kanisa linaendeleza sadaka iliyotolewa “mara moja tu” Msalabani na hivyo kuingia katika utajiri wa ufufuko wa Kristo. Carlo Acutis, kijana wa Kiitaliano aliyefariki akiwa na miaka 15, aliishi imani yake kwa namna ya pekee, hasa kupitia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kiini cha maisha ya Kikristo.

Ekaristi: Chanzo cha Nguvu Yake

 Carlo alihudhuria Misa kila siku na hakukosa hata katika siku za sikukuu. Alielewa Ekaristi si tu kama sherehe bali pia kama ibada yaani, kushiriki na pia kuabudu. Katika mafundisho ya Kanisa Katoliki, Ekaristi inaeleweka kuwa ni sadaka, chakula na pia uwepo wa kweli wa Kristo si tu wakati wa Misa, bali hata baada ya sherehe, katika Sakramenti iliyohifadhiwa katika tabernakulo. Papa Paulo VI katika waraka wake “Mysterium Fidei (1965),” alisisitiza kuwa uwepo wa Kristo katika Ekaristi ni wa kipekee, kwa sababu unadumu hata baada ya Misa Takatifu. Ni Kristo yuleyule tunayemwabudu mbele ya Tabernakulo si kama sadaka tena, bali kama Sakramenti hai. Carlo alielewa haya vyema. Hakuona tofauti kati ya kushiriki Misa na kumwabudu Kristo katika Ekaristi Takatifu. Hili ndilo lililomfanya awe na uhusiano wa karibu na Mungu na kumpelekea kuwa shahidi hai wa Injili kwa wenzake.

Carlo Acutis wa kizazi cha sasa
Carlo Acutis wa kizazi cha sasa   (© Stefanie Stahlhofen (Radio Vatikan/Vatican News))

Mjasiri wa Imani

 Licha ya kudharauliwa na baadhi ya marafiki kwa ajili ya imani yake, Carlo hakutetereka. Alijua kuwa wengi si kigezo cha kuwa sahihi, bali ukweli ndio unaoleta haki. Alijitoa kwa moyo wote kueneza Injili, hata kwa kutumia kipaji chake cha kompyuta. Alitumia teknolojia kama chombo cha kutangaza ukweli wa Mungu na kuhubiri uzuri wa Ekaristi kwa vijana wenzake. Aliwashawishi hata watu wa dini nyingine ambao baada ya kukutana naye waliamua kubatizwa. Alikuwa mwerevu katika teknolojia, lakini pia bingwa wa roho kwa imani yake thabiti. Upendo kwa Papa na Kanisa: Carlo alikuwa mwaminifu kwa Papa akiwemo Yohane Paulo II au Benedikto XVI na alimwombea kila siku. Aliona Kanisa kama Mama na Mwalimu wa wokovu, akisema: “Kukosoa Kanisa ni kujikosoa sisi wenyewe.” Alikuwa mwana wa Kanisa kwa moyo wote na alilithamini fundisho rasmi la Kanisa Katoliki. Kujitoa kwa Bikira Maria: Carlo pia alikuwa na ibada ya dhati kwa Bikira Maria. Alijitoa kwake mara nyingi na alikuwa mwaminifu katika kusali Rozari kila siku. Alisema mara nyingi: “Rozari ni ngazi fupi zaidi ya kupanda mbinguni.” Ukaribu wake na Mama wa Yesu ulimpa nguvu na ujasiri wa kuishi utakatifu katika maisha ya kila siku.

Hakuwa tofauti na vijana wenzake
Hakuwa tofauti na vijana wenzake   (ANSA)

Kifo cha Mtakatifu Chipukizi

 Mnamo Oktoba 2006, Carlo aligundulika kuwa na aina kali sana ya Leukemia (aina ya M3), na alifariki tarehe 12 Oktoba 2006, akiwa na miaka 15 pekee. Alikabiliana na ugonjwa wake kwa utulivu na imani kubwa akisema: “Natoa mateso yote kwa Bwana, kwa ajili ya Papa na Kanisa, ili nisiingie toharani bali niende moja kwa moja mbinguni.” Alipewa Sakramenti ya Wagonjwa na Ekaristi ya mwisho (Viatico), akitabasamu hadi mwisho, na kuwa mfano wa imani, tumaini na upendo kwa wote waliomzunguka. Mtakatifu wa Vijana: Kanisa, likiongozwa na Papa Francisko lilimtangaza Carlo kuwa mwenyeheri, si kwa sababu alikuwa mwanafunzi wa taalimungu, bali kwa sababu aliishi imani kikamilifu katika mazingira ya kisasa. Carlo anatufundisha kuwa hata vijana wa leo wanaweza kuwa watakatifu kwa kupitia Ekaristi, upendo kwa Maria na utii kwa Kanisa. Wengine waliotangulia kama yeye ni Maria Goretti, Piergiorgio Frassati, na wengine wengi. Wote wana tabia moja ya pamoja ya kutegemea Ekaristi Takatifu, Bikira Maria na mafundisho ya Kanisa ili kuwa mashahidi wa imani. Carlo Acutis sasa anaorodheshwa kati ya watakatifu vijana wa nyakati zetu. Mfano wake ni mwanga kwa vijana wote wa karne hii, kuwa inawezekana kuwa mtakatifu hata katika ulimwengu wa kidijitali.

Carlo anatufundisha kuabudu Yesu wa Ekaristi
Carlo anatufundisha kuabudu Yesu wa Ekaristi
Acutis II
05 Septemba 2025, 11:32