WAWATA Tulieni Kwani Kwenye Kanisa Katoliki Daima Kumenoga!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kamati Tendaji ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, Jimbo kuu la Dar Es Salaam linawapongeza na kuwashukuru Wanawake Wakatoliki Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa kujitokeza kwa wingi na hatimaye, kushiriki kikamilifu katika “Bonanza” lililotimua vumbi tarehe 8 Agosti 2025 katika Viwanja vya Parokia ya Kristo Mfalme, Tabata, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Ushirikiano, mshikamano na furaha walioiona ni ushuhuda wa Injili ya upendo, umoja na mshikamano katika Kristo Yesu na kwamba, utume wa WAWATA ni chemchemi ya furaha! Hii ni sehemu ya maneno ya shukrani yaliyotolewa na Mama Stella Rwegasira, Mwenyekiti wa WAWATA Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kwa upande wake Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi OFM Cap., wa Jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam ameliona tukio la Bonanza, Jimbo kuu la Dar es Salaam kuwa ni: Semina, warsha na fursa ya kujengana, kurithishana na kuaminishana tunu msingi za maisha ya Kikristo. Iwe ni siku njema inayowawezesha kurithishana mema, yaliyo halali na mambo matakatifu, ili kila WAWATA anapotoka mahali hapo awe amejengeka, ameimarishwa na amewezeshwa kuwajibika vyema zaidi kama Mkristo na WAWATA. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, amewataka WAWATA kufundishana: wema na uadilifu; waishi imani yao safi, watulie ndani ya Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume, ambamo wana kila kitu wanaochohitaji kwa ajili ya ustawi na wokovu wa roho zao. Huko kwenye “vijiwe vya manabii wa uongo WAWATA wanahemea nini? Amewataka WAWATA wasiwe ni vigeugeu, bali wamtambue Mungu ambaye ni Muumbaji, Mwokozi na Mkombozi wao. Mungu ni mkamilifu, mwingi wa huruma na mapendo; Mungu ni mwaminifu anayeutazama unyonge wa waja wake na kuwahumia, kielelezo makini cha uaminifu, upendo na huruma yake isiyokuwa na kifani. Mwenyezi Mungu aliwakomboa Waisraeli kutoka utumwani, akaangalia mateso na mahangaiko yao na hivyo kuwaweka huru. Amewataka WAWATA kutambua heshima, wito na utume wao na kamwe wasitangetange kwenye “vijiwe vya manabii wa uwongo.” Waisraeli katika maisha yao, walikuwa na kumbukumbu fupi, kiasi cha kumwacha Mungu wa kweli na kuwageukia miungu wa uwongo.
WAWATA wasikimbilie kwa miungu na manabii wa uwongo. WAWATA wajitahidi kuwa ni wafuasi waaminifu wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watambue dhamana, wajibu, jukumu na wito wao wa: kulinda, kutetea na kutunza Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kamwe WAWATA wasiwe mashabiki na mashuhuda wa utamaduni wa kifo na kwamba, uhai ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Pili wanawake ni Makatekista wa kwanza, wanaopaswa kuwarithisha watoto wao imani, maadili na utu wema. WAWATA wajitahidi kuwafundisha watoto wao imani ya kweli. WAWATA watambue kwamba, wao ni mihimili ya Kanisa ndogo la nyumbani na kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Mama mtulivu, mkomavu na mwenye imani thabiti ni kielelezo cha Kanisa dogo la nyumbani, kwani wao ni washauri wa kwanza wa wanaume wao na kwamba, wao wanaweza kuwasaidia wanaume wao kuwa ni washiriki wazuri wa Kanisa dogo la nyumbani; huku wakipenda kukaa nyumbani na kamwe wasinyanyasane na familia kuonekana kuwa ni “Uwanja wa masumbwi.” Wana familia wasipigane, wawafundishe watoto wao Injili ya upendo kwa watu wote. WAWATA watulie tuli na kuanza kujikita katika ujenzi wa Kanisa na kwamba, ukuu wa kweli unafumbatwa katika huduma kwa watu wa Mungu. WAWATA wakimezwa na malimwengu, wakitafuta ukubwa, umaarufu na mafanikio ya chapuchapu, wanaweza kujikuta wakiishia kwa “miungu na manabii wa uwongo, wachawi na imani za kishirikina. Ukuu wa kweli unasimikwa katika unyenyekevu na huduma, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, mfano bora wa kuigwa kwa wafuasi wanaojitaabisha kutumikia.
Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, ana haya ya kusema: MALEZI YA NDOA NA FAMILIA: Naomba nianze na swali. Hivi ni kwa nini leo tunalalamika hatuwaoni waume zetu kwenye Jumuiya? Jumuiya wanaohudhuria ni nani? Baba? Mama? Vijana? Watoto? Mume wako, na kwa mabinti zangu – Baba yako anaonekana nyumbani ama haonekani? Umewahi kujiuliza ni kwa nini haonekani nyumbani (ikiwa kweli haonekani) lakini ana muda na washikaji? Umewahi kutafakari huyo mtoto wako wa kiume unayeemlea leo ama utakaemzaa kesho ungependa awe nani, aishi maisha gani, matamanio gani, uwajibikaji wake, uadilifu wake, weledi wake ama atofautiane namna gani na uhalisia wa sasa? Je, ungependa binti unayemlea leo afuate nyayo zako? Kwa nini? Na kijana wa kiume Je? Afanane na baba yake?
KWA NINI Leo tunazungumzia sana: Msongo wa Mawazo! Afya ya akili! Magomvi kwenye maisha ya ndoa na familia? Talaka n.k. Nini maana ya familia kadiri ya machimbuko. Familia ni taasisi ya msingi ya jamii iliyowekwa na Mungu. Inaundwa na ndoa na inaundwa na watu wanaohusiana kwa ndoa, kwa damu au kuasili(adoption). Familia ni taasisi ya msingi ya jamii ya wanadamu. (Mwanzo 2:20-25; Mwanzo 4:1; Kutoka 20:5-6; Yoshua 7:10,15,24-25; 2 Wafalme 13:23.) Familia ni tabernakulo ya uhai wa mwanadamu ni mahali ambapo watoto wanarithishwa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Familia ni shule ya malezi na makuzi bora; ni mahali pa kujifunza kusamehe na kusamehewa, kupenda na kupendwa. Familia ni kitalu cha haki, amani na upatanisho wa kweli; mahali ambapo watu wanajifunza kutaabikiana na kusumbukiana kwa hali na mali. Familia ni mahali muafaka pa kujifunza maisha ya Kisakramenti, Tafakari na Neno la Mungu na kuhakikisha kwamba, kweli imani inamwilishwa katika matendo. Familia ni kikolezo cha uinjilishaji kwani kwa kujiinjilisha yenyewe inashiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji. Wazazi ni mashuhuda wa kwanza wa Injili ya Kristo Yesu.
MALEZI NI NINI: Ni mfumo wa majiundo, anaopewa mtu (mtoto/kijana) katika hatua mbali mbali ili kumjenga kiutu, kimaadili (kitabia), kiroho, kiakili na kimwili, lishe bora, ulinzi nk. Upendo wa Kikristo ni sadaka (ni kujitoa), kama vile Yesu alivyoonyesha kwa kufa msalabani, wazazi na watoto wanaitwa kutoa sadaka (dhabihu) kwa ajili ya kila mmoja wao. Familia ndio mahali pa kwanza ambapo watoto wanaweza kujua juu ya upendo, urafiki na msamaha. Wazazi wanaweza kuwawekea watoto mfano mzuri wa jinsi ya kuishi maisha ya Kikristo. Hayo ndiyo tuyaitayo MALEZI. Malezi yanaanza pale mimba inapotungwa, kwa sababu ukaribu hapa mtoto akiwa kijana ama mtu mzima hakuna namna ya kumbadilisha. Anakuwa mzigo kwa: mama, familia, jamii na Taifa.
Muhtasari wa Mahubiri ya Papa Leo IV Kuhusu Malezi ya Familia: Familia kama msingi wa malezi: Familia ni mahali ambapo watoto hupokea tunu za kiroho, kiutu, kimaadili na kitamaduni. Ni shule ya kusamehe, kupenda, kushirikiana na kujenga haki, amani na upatanisho. Wajibu wa wazazi: Wazazi ni mashuhuda wa kwanza wa Injili kwa watoto wao, wanapaswa kuwafundisha maisha ya sala, tafakari na imani inayomwilishwa katika matendo mema, adili na matakatifu. Kujenga mshikamano: Watoto wafundishwe kujenga madaraja ya urafiki na mshikamano bila kujali tofauti zao, na kuwa wajenzi wa amani na maridhiano. Changamoto za malezi ya kisasa: Shughuli nyingi za wazazi na watoto zinapunguza muda wa mawasiliano ya familia; kuna haja ya kusawazisha maisha ya kiroho na kijamii. Aina nne za malezi: Malezi ya kimabavu: Adhabu kali huzaa watoto wasiojiamini. Malezi ya mamlaka/demokrasia: Huwasaidia watoto kuwa na furaha, uthabiti na mafanikio. Malezi huru: Wazazi huingilia tu panapojitokeza tatizo kubwa, huchukua nafasi ya rafiki kuliko mzazi, na hukosa uthabiti wa kuongoza. Malezi huria: Ukosefu wa ufuatiliaji na miongozo hudumaza ufaulu, nidhamu na furaha ya watoto. Lengo kuu: Malezi bora yanapaswa kuwaendeleza watoto kiroho, kiutu, kijamii na kimatamaduni, wakikua wakiwa watu wenye maadili na imani thabiti. Watafiti na wanasaikolojia wanasema, kuna uhusiano mkubwa sana baina ya maisha tuliyopitia utotoni na tabia ama mwonekano wetu wa sasa. Mtoto akipitia uzoefu mbaya utotoni: unyanyasaji, ama ukatili akiwa mtoto – asipopata usaidizi wa kisaikolojia sehemu kubwa ya maisha yake atayaishi hayo (tabia). Sista Rosemary Nyirumbe alituambia wakati akitoa wasilisho la nyanyaso na vipigo vilivyopitiliza kwa watoto kuwa alipigwa sana wakati anakua na akaapa kulipiza anapokuwa mtu mzima. Kwa neema ya Mungu alisaidika katika majiundo ya utawa na badala ya kulipiza kisasi, amejenga upendo wa kuwahudumia wanaopitia changamoto hizi.
Tunawalea vipi Watoto leo? Usisubiri upate mtoto ndipo ujifunze Kulea. La hasha, unajifunza kabla na unaendelea kujifunza Kadiri unavyokabiliana na changamoto za njiani. Soma vitabu vingi uwezavyo! Dadisi, na angalia tafiti za wabobezi. Haimaanishi utakuwa mkamilifu lakini utaboresha na kukabiliana na changamoto mapema na kwa urahisi zaidi. ZINGATIA NA WEKEZA katika: Imani; Uthabiti unaojengwa wakati wa majiundo ya ubongo na nafsi -Resilience built during soul development (hapa wazazi/walezi tunahusika. Kuwa na rafiki wa kukimbilia na kujimwaga mbele yake “Having even One person to run to” Mafungamano na Mahusiano mazuri na ndugu wa familia “Family coherence” Kutambua hatma ya maisha - Having known purpose in life (wazazi wana deni kubwa sana hapa. Kujitambua n.k. Kuepuka upweke hasi! Tofautisha upweke na kuwa pweke! Waweza onekana kana kwamba umezungukwa na watu wengie lakini ukawa mpweke Tufanyeje! Tunatokaje? Turejee wito wetu wa malezi na kuwekeza kwa vitendo na sio kwa maneno. Tukiwa na nia thabiti tutaweza kukabiliana kikamilifu na changamoto mamboleo katika maisha, malezi na makuzi ya watoto wetu. Tupige hatua ndogo ndogo kufanya marekebisho tulipoanguka “Small steps.” Hatuwezi kubadili kila kitu kwa wakati mmoja. Hapa mara nyingi tunategemea mabadiliko makubwa mno kwa Watoto wetu kiasi kwamba wanapopiga hatua kidogo tu, hatuoni ili tuwapongeze na kuwapa moyo wa kupiga hatua inayofuata. Matazamio yaliyo nje na uwezo wa mtoto kwa wakati huo, yanawakatisha tamaa wote wawili - mzazi na mtoto.
HIVYO FUNGUA MACHO KUONA NA KUPONGEZA KILA KITENDO CHANYA ANACHOFANYA MTOTO. Hii inampa moyo kwamba anaweza, kuwa unaona juhudi yake, kwamba una interest naye na matendo yake, kuwa unampenda unapompongeza kwa hatua kidogo tu! “Role modeling! Watoto wetu na vijana hawaguswi na kuambiwa, ila wanaguswa sana na kuona. Kila mzazi awe kila anachotaka kuona kwa mtoto wake. Mama Teresa wa Calcutta aliwahi kusema (Anza wewe kubadilika kuwa kile unachokitamani” Be the change you want to see.” Na hapa tunasema, “Be the change you want to see in your child.” Usimwambie mtoto asali wakati wewe husali! Baba ajiulize – huyu binti yangu wa kike ndie anaweza kuwa aina ya mke ambae ningemtamani, likewise Mama kwa mtoto wa kiume. “In the flip side.” Mtoto wa kiume kwa mama na mtoto wa kike kwa baba. Nina rafiki ambae kwa hakika kazi yake inamfanya anakuwa “busy” sana – anachofanya anapotoka kazini ni kwenda moja kwa moja nyumbani. Atacheza na watoto, atahakikisha ameketi nao mezani kula na wakishasali anaendelea na ratiba binafsi ikiwa ni pamoja na kuona “washikaji kijiweni.” Je, Mume wako anaona fahari kurejea nyumbani kufurahi na Watoto wake? Ama akirejea anajua matusi yatamfanya asitoke, kumbe ni bora abaki mtaani, nyumbani anarejea kulala? Nani kakudanganya baba na mama yako hawakukerana? Unadhani kwa nini walilea watoto wao pamoja?
Tunalihitaji Kanisa kuwekeza katika mazingira wezeshi; Mazingira ya Kanisa ni pamoja na viongozi wetu wa kiroho kuwa karibu na wazazi, ili kubaini changamoto zao za malezi, kuwapa mwanga wa nini kifanyike, ili na viongozi wetu wasaidie kwa kutoa ujumbe ule ule kwa watoto na vijana wetu wanapofundisha - mahubiri, semina na makongamano ya watoto na vijana. Faida yake ni kwamba mtoto atasikia ujumbe ule ule, toka nyumbani, kwa mwalimu na kanisani. Hapa ni dhairi ujumbe huo utakuwa na uzito Zaidi na ni rahisi kwa mtoto kuzingatia na kuufanyia kazi. Hapo tutaona mabadiliko chanya na ya kweli kwa Watoto wetu. “Consistency is key here.” Wazazi pia nyumbani wasipishane kwa ujumbe wanaoutoa kwa watoto wao! Baba na mama wawe kitu kimoja na kutoa ujumbe ule ule, na waoneshe na kushuhudia tunu wanazozitamani kwa watoto wao! Serikali kuwekeza sera wezeshi: Serikali kikatiba na kisheria ni mlezi mkuu. Inapaswa kuwa karibu sana na wazazi na walezi katika kazi hii muhimu ya malezi. Watoto wanaolelewa ndiyo raia na iongozi wa serikali; hivyo wakiharibika serikali ndiyo ya kwanza kupoteza – hakuna serikali inayoweza kuendelea ikiwa asilimia kubwa wa watu wake ni hohehahe au ni mazuzu! Hivyo tunaisihi seriali ishirikiane na wadau wote wa malezi na kuwapa msaada wanohitaji katika kazi ya malezi! Wadau hawa ni wazazi, waalimu na viongozi wa dini, maana hawa ndio walezi wakuu wa Taifa!
NINI WAJIBU WA MZAZI/MLEZI: Kumjua mtoto wako (Know Your Child – KYC) ni muhimu kuliko hata kumjua mteja wa kibiashara; inajumuisha jina, tarehe ya kuzaliwa, marafiki wa karibu, chakula na michezo anapenda, maeneo ya likizo, shughuli baada ya shule, na dawa zinazoweza kumdhuru. Watoto hawafanani, hivyo malezi yanapaswa kubadilishwa kulingana na tabia na mahitaji ya kila mtoto mmoja mmoja. Changamoto za watoto hutofautiana kwa umri; mfano, miaka 3 na 13 zina changamoto tofauti, ikiwemo kushuka kwa utendaji wa kielimu wakati wa kubalehe. Licha ya wazazi wengi kudai familia ni kipaumbele, wachache huwekeza muda, elimu, fedha, na rasilimali nyingine kwa watoto wao ipasavyo. Ukuaji mkubwa wa ubongo hutokea kati ya miaka 0–5, ambapo karibu 90% ya ukubwa wa ubongo wa mtu mzima hufikiwa; kipindi hiki ni muhimu kwa kujenga uhusiano wa neva kupitia uzoefu na mafunzo. Miaka 6–12 ni kipindi ambacho ubongo unaendelea kukua hasa katika lugha, ujuzi, na udhibiti wa hisia; malezi bora yanaweza kusaidia kuondoa mazoea yasiyo na manufaa. Tambua, una ushwishi mkubwa wa tabia na mwenendo wa mtoto wako kati ya umri sifuri hadi miaka 12 (0-12) (kabla ya balehe).
Hiki ni kipindi ambacho mtoto anamwamini mzazi asilimia 100? Baada ya hapa kinachoendelea ni 50:50 – atakusikiliza, atabalance na marafiki ataamua la kufuata! Ni muda anahitaji muda wake mwenyewe. Kitabu cha “The Whole Brain Child” kinashauri wazazi kusaidia watoto kutumia pande zote mbili za ubongo (kulia – hisia, kushoto – mantiki) kwa usawa. Epuka kutumia upande mmoja wa ubongo pekee; mzazi anatakiwa kuungana na mtoto kihisia kwanza (“connect”) kisha kumwelekeza (“redirect”.) Mfano: Mtoto akilia baada ya kuvunja kitu, mzazi amfariji kwanza kisha amwelekeze jinsi ya kuepuka kosa hilo tena. “Connect Before You Correct.” Wazazi wanapaswa kutuliza mtoto kihisia kabla ya kutoa ushauri au kurekebisha tabia. Ubongo wa kulia hujifunza kupitia vitendo zaidi kuliko maneno; kuonesha huruma, kugusa, na kutumia lugha ya vitendo husaidia zaidi. Tabia nzuri au mbaya hujengeka mapema, hasa kati ya miaka 0–8; hivyo wazazi wanapaswa kuzingatia malezi chanya mapema iwezekanavyo!
ATHARI ZA TALAKA KWA WATOTO: Ni ukweli usiopingika kuwa, maisha ya mtoto baada ya wazazi kutalikiana ni sana na kuwa amefiwa na mzazi mmoja. Lengo si kuzuia talaka bali kusaidia watu kufikiria kwa makini kabla ya kujaribu talaka, na njia mojawapo ni kuhakikisha maamuzi ya kuingia kwenye ndoa ni sahihi. Ndoa inahitaji heshima, kujiheshimu na nidhamu; kuoa au kuolewa na mtu asiye na maadili kunachangia kuvunjika kwa ndoa. Wengi huingia kwenye ndoa kwa sababu za kifedha au fursa binafsi, bila kuzingatia uhusiano wa kweli, na huishia talaka. Takwimu za 2022 Dar es Salaam zilionesha ndoa 300 kuvunjika, na mjadala uliibua hoja kuhusu ustawi wa watoto baada ya talaka. Hekima ya ndoa: Ndoa inaweza kuwa mbaya zaidi kabla ya kuwa bora; changamoto ni sehemu ya safari ya ndoa. Watafiti wamasema, ndoa nyingi huvunjia katika hatua ya mwisho kabisa ya kuelekea ubora! “Ukweli mchungu.” Falsafa ya Marcus Aurelius: msamaha, uaminifu na kuvumilia marafiki waliokosea huimarisha mahusiano. Wanaopenda wenzao huwapenda pamoja na mapungufu yao; usiharakishe kuondoka ukidhani hali ni bora kwingine. Utafiti wa Judith Wallerstein: Watu hufikiria mara nyingi kuhusu talaka bila kutekeleza, lakini madhara ya talaka yakitokea ni makubwa, hasa kwa watoto. Talaka husababisha mgawanyiko wa kifedha, kuvunjika kwa mafungamano na uhusiano wa kifamilia, na mara nyingi huchangia matatizo ya kijamii na kihisia kwa watoto; marafiki watagawanyika n.k. Sababu kuu za talaka: ukosefu wa uaminifu, ukosefu wa mawasiliano, matatizo ya kifedha, matumizi ya dawa za kulevya, na ukatili wa kijinsia. Tafiti zinaonesha ndoa za muda mrefu zinaathiriwa na historia ya familia, uzoefu wa utotoni, na mtazamo wa ndoa uliopatikana kwa wazazi. Ushauri Makini: tafuta suluhu na msaada wa kiroho na kitaalamu kabla ya kuamua kuvunja ndoa.