UISG,Agosti 14 ni siku ya kufunga na sala kwa ajili ya amani
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kuanzia Gaza, Sudan, Ukraine, Haiti, DRC, Syria, Myanmar, Congo DRC, na kwingineko dunania. Ni majeraha ya ulimwengu ambayo yapo na yanaonekana kwa wote! Ni nyuso zilizo alama ya maumivu, nyumba kuharibiwa, jamii kusambaratika. Wanaolipa gharama ya juu mara nyingi ni wanawake na watoto. Hii ndiyo sababu Umoja wa Kimataifa wa Mama wakuu wa Mashirika ya kitawa (UISG), umezindua wito mzito kwamba: "mnamo tarehe 14 Agosti 2025, katika mkesha wa sherehe ya Kupalizwa kwa Bikira Maria Mbinguni, itafanyika Siku ya kimataifa kwa ajili ya kufunga na maombi kwa ajili ya amani. Katika muktadha huo, Jumuiya zote za kitawa na yeyote mwenye mapenzi mema anayetaka kujiunga anaalikwa kufanya hivyo."
Hatuwezi kusubiri, amani lazima ijengwe
Katika taarifa iliyotolewa na Sr Roxanne Schares SSND – Makamu rais wa UISG na Sr Thérèse Raad, sdc – Afisa mawasiliano wa UISG wanawatangazia kuwa: "Kama wanawake wa amani waliopo pembezoni mwa dunia na kuzama katika mateso ya binadamu, tunahisi udharura wa kupaza sauti zetu, kuunganisha mioyo, kuomba, na kutenda." Na ili lipate kufanyika, ishara tatu za dhati zinapaswa kutekelezwa: "Ombeni pamoja na kutafakari Neno la Mungu, katika mwanga wa vita na migogoro ya sasa; Wito wa haki na upatanisho, ukizihimiza mamlaka za kiraia na kikanisa kufuata njia za amani, upokonyaji silaha, na ulinzi wa haki za binadamu; Kutenda kwa mshikamano thabiti, kusaidia wale wanaoteseka kupitia mitandao ya ukaribisho na misaada ya kibinadamu.
Kuungana katika sala na ushuhuda
Kwa kuongezea watawa hawa wanasisitiza wito kwamba: "Hatuwezi kusubiri. Amani inajengwa. Na inajengwa pamoja.” Katika ulimwengu ulioangaziwa na vurugu aidha, UISG "inaendelea kuamini kwamba nuru ya Injili, haki, na udugu bado inaweza kung'aa. Pamoja na Maria, Mama wa Matumaini," masista hawa "wanaungana katika sala na ushuhuda."