杏MAP导航

Tafuta

2023.05.22 Ad Limina Visit dei Vescovi Tanzaniani 2023 La Santa Messa dell’Ascensione del Signore rappresenta il momento in cui Gesù si stacca dalla Terra e dai suoi discepoli, lasciando la Sua forma umana per salire al Cielo.

Tanzania: Novena, Sala, Toba na Mfungo Wa Kuombea Haki na Amani

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi OFMCap., ameagiza kwamba katika Parokia zote na Asasi zote katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam ifanyike Novena ya kuomba Haki na Amani kuanzia tarehe 15 Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho hadi tarehe 23 Agosti 2025. Askofu Mkuu Ruwa'ichi ameelekeza kwamba, Novena hiyo iambatane na kuabudu Ekaristi Takatifu, Kusali Rozari Takatifu na kusali sala ya Kuiombea Tanzania kama iliyotolewa na TEC.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa mwanga na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, akiwa ameungana na Maaskofu wenzake, Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 akatangaza rasmi kwamba, Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili ni sehemu ya Mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki. Bikira Maria tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Baba Mtakatifu Benedikto XVI anatukumbusha kwamba, maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria yanakwenda sanjari na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Bikira Maria, Mama wa Mungu kwa upendeleo na neema ya Mungu akabahatika kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na hivyo kushirikishwa kwa namna ya pekee kabisa katika Fumbo la Pasaka na utukufu wa Kristo Yesu. Hili ni Fumbo linaloonesha historia ya ubinadamu, matumaini ya watu wa Mungu na Kanisa katika ujumla wake.

Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho
Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho   (© Catherine Leblanc - byzance-photos.fr)

Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho, anaendelea kuliombea Kanisa ambalo bado liko safarini, ili liweze kupata neema ya uzima wa milele. Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya Kimama anaendelea kuwasindikiza watoto wa Kanisa ambao wako bondeni huku kwenye machozi, ili siku moja, waweze kufika mbinguni na kufurahia maisha na uzima wa milele. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni inakita mizizi yake katika imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni kielelezo cha ushindi wa nguvu ya upendo wa Mungu kwa waja wake.

Kuanzia tarehe 15 hadi 24 ni Siku za Novena, Kusali, Kufunga na Toba
Kuanzia tarehe 15 hadi 24 ni Siku za Novena, Kusali, Kufunga na Toba

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi OFMCap., wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania tarehe 07.07.2025 katika Sherehe za Upadrisho katika Viwanja vya Msimbazi Center, alitoa maelekezo kuhusu utaratibu wa Novena ya kuliombea Taifa la Tanzania Haki na Amani. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi OFMCap., ameagiza kwamba katika Parokia zote na Asasi zote katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam ifanyike Novena ya siku tisa (9) kuomba Haki na Amani kuanzia tarehe 15 Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho hadi tarehe 23 Agosti 2025. Askofu Mkuu Ruwa'ichi ameelekeza kwamba, Novena hiyo iambatane na kuabudu Ekaristi Takatifu, Kusali Rozari Takatifu na kusali sala ya Kuiombea Tanzania kama iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC). Aidha, katika siku ya kilele cha Novena hiyo, yaani Jumamosi tarehe 23 Agosti 2025, ambayo ni kwa ajili kuombea Haki na Amani, waamini wote wanaalikwa kufuata ratiba iliyotolewa na Idara ya Kichungaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambayo inaelezea namna ya kufanya sala na mfungo huo ambao utaanza hiyo tarehe 23 Agosti kwa adhimisho la Ekaristi Takatifu, ikifuatiwa na kuabudu Ekaristi Takatifu ikiambatana na vipindi mbalimbali vya sala, mafundisho, na ukimya, na kuhitimishwa Dominika tarehe 24 Agosti kwa adhimisho la Misa Takatifu kama inavyoelekezwa katika maelekezo yaliyotoka TEC. Hapa inapendekezwa kwamba katika Parokia zote Misa hii ya hitimisho la kesha iwe Misa ya kwanza. Nyongeza: Sala mbalimbali ambazo zimeelekezwa/ zimependekezwa katika ratiba hii iliyotolewa na TEC, inaweza pia kutumika katika kusali Novena iliyoelekezwa na Askofu mkuu.

Jimbo kuu la Dar Es Salaam Novemba ya Kuombea Haki na Amani Tanzania
Jimbo kuu la Dar Es Salaam Novemba ya Kuombea Haki na Amani Tanzania

SALA YA KUIOMBEA TANZANIA: Ee Mungu Mwenyezi wa milele, Baba wa mataifa yote na wa watu wote, utuangalie kwa macho ya huruma sisi watu wako wa Tanzania, ambao nasi sasa twahesabika kati ya mataifa ya dunia. Kwa baraka yako uhuru wetu huu usipokonywe, na utuwezeshe kuishi maisha mema zaidi kadiri iwastahilivyo waana wa Mungu. Tunakuomba nchi yetu iwe ya amani, waliopotea wapatikane na waliotekwa wapate uhuru wao, walioumizwa wapone, na waliouawa wapate uzima wa milele na uovu ukome katika nchi yetu. Tunakuomba ubadilishe nyoyo za watenda maovu na washirika wao katika uovu ili zikuelekee wewe, kwani sisi tulio wanyonge hatuna uwezo wa kuzibadilisha nyoyo ovu. Uendelee kututawala na kutuongoza. Daima nchi hii iongozwe na viongozi ambao ni chaguo lako. Waangazie watawala hao, sheria wanazotunga kwa kutufaidia kwa mambo mema ya hapa duniani zipatane na Wewe uliyetuumba kwa ajili yako. Wajalie watu wetu wote paji lako la Imani. Tukiwa Mahujaji wa Matumaini, tuthibitishe tusishindwe kupambana na maovu yawezayo kutufikia kutoka nje au ndani, tupe hekima ya kutafuta ukweli katika mambo yote, na kuishi kwa uaminifu katika amri zako. Ee Mwenyezi Mungu, uongozi wa kweli unatoka kwako, tunakuomba ujalie wale watakaosimamia na kuiishi Demokrasia ya kweli, Haki na Amani katika nchi yetu ili haki ituletee Amani ya kudumu. Washa nyoyo zetu na mapendo yako ya kimungu yatakayotuwezesha kushinda utengano, ushindani, na chuki ya ukabila au utaifa, na tuunganishe wote katika muungano wa kidugu utakaotuwezesha, kwa msaada wa neema yako, kutufanya tuwe umoja katika Wewe Baba wa wote. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina. Bikira Maria Mtakatifu Mkingiwa dhambi ya asili. Utuombee. Atukuzwe Baba.... Amina.

Haki na Amani Tanzania
09 Agosti 2025, 14:16