Tanzania,Ask.Mwijage: kila familia inayo wajibu wa kulinda Imani Katoliki bila kuyumbishwa!
Na Patrick P. Tibanga-Radio Mbiu – Kagera.
Wazazi na walezi wametakiwa kutunza uzao, kuwafundisha watoto wao sala na Imani na kuwaandaa watoto wao katika kuitetea Imani na kuliombea amani taifa la Tanzania. Rai hiyo imetolewa tarehe 10 Agosti 2025 na Mhashamu Jovitus Mwijage, Askofu Jimbo Katoliki Bukoba, Tanzania wakati wa homilia yake, kwa waamini wa Kigango cha Mtakatifu Petro Mtume- Mabira, Parokia ya Rukindo, Jimbo Katoliki Bukoba, alipokuwa katika ziara yake ya kichungaji katika Parokia hiyo.
Askofu Mwijage alisema kuwa, kila familia inayo wajibu wa kulinda Imani Katoliki na kamwe wasikubali kudanganyika na madhehebu yanayo chipukia, na kuwasihi wazazi kulinda Kanisa lao na vizazi vijavyo kwa gharama yoyote kwa kuwa na Imani thabiti na kuilinda kupitia matendo mema. “Sehemu zote nilipokwenda katika mataifa ya magharibi ninakuta hakuna silaha ya kulinda Kanisa ambalo ni watoto, wamejenga makanisa mazuri sana, kitu walichokosea walikataa uzao, hawakuwa na majeshi ya kulinda Kanisa, na Makanisa sasa hivi yananunuliwa na wahamiaji kutoka nchi za mashariki ya kati, na hilo ni tatizo kubwa linalokumba makanisa ya Ulaya na Amerika, kwa hiyo ninawaomba wakina baba na mama, familia tilieni maanani hilo kutunza makanisa, baada ya muda mchache Mungu atatuita kama hakuna majeshi ya watoto ya kulinda na kutunza makanisa, itakuwa kazi bure.” Alisema Askofu Mwijage katika mahubiri yake. Askofu Mwijage alidha aliwataka waamini kuanzisha vyama vya kitume na kuwahimiza watoto kushiriki katika vyama hivyo huku akisisitiza watoto kuwa “ni hazina bora ya Kanisa, pamoja na kutenga muda wa kuabudu Ekaristi Takatifu, kupokea sakramenti ya kitubio na kupeleka mahangaiko yao kwa Yesu wa Ekaristi kila wanapopata nafasi.”
Kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajiwa nchini Tanzania hivi karibuni, Askofu Mwijage aliwataka waamini “kuombea haki na Amani nchi Tanzania nakuwasihi viongozi wa Serikali kuhubiri haki na Amani, ili kutenda haki kwa wananchi wake ndio Amani itapatikani” na kuongeza kuwa “ taifa haliwezi kuwa na Amani bila haki kutendeka kwa wananchi wake.”
"Tuombe viongozi wetu, waweze kufahamu watu wanalia hakuna haki, wanaombea haki na amani, wawe tayari kutunza haki ndipo amani itapatikana, neno haki hawataki kulisikia, sisitiza kwanza pawepo haki ndipo amani itapatikana, wengi wanapotosha kwa kusema amani bila ya haki, wengi linawasumbua hawataki kusikia neno haki, sisitiza kwanza pawepo haki ndipo Amani itafuata," alisisitiza Askofu Mwijage katika homilia yake.
Katika ziara hiyo Askofu Mwijage alifanikiwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kanisa la Kigango cha Ihunga na kuzindua Kanisa la Kigango cha Mtakatifu Petro Mtume Mabira, kisha alihitimisha ziara yake kwa kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waimarishwa 2511 wa Parokia hiyo.