Tafakari Dominika 19 Mwaka C wa Kanisa: Kesha, Imani na Uaminifu!
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 19 ya mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya 19 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa inatualika; “Kukesha kwa imani na uaminifu katika kumngoja Bwana.” Maisha ya Mwanadamu hapa duniani ni safari kuelekea Mbinguni, ulipo utimilifu wa lengo la kuwepo kwetu hapa duniani, yaani kumjua Mungu, kumpenda, kumtumikia ili mwisho turudi kwake. Katika Dominika iliyopita, Kristo alitutahadharisha juu ya hatari ya kujisahau katika maisha haya, na kushindwa kuwekeza hazina yetu mbinguni. Katika Dominika hii ya 19 ywa Mwaka C wa Kanisa Kristo anatukumbusha kuwa, maisha haya ni mafupi na ni ya muda tu, hivyo tunapaswa kujiandaa kila wakati kwa kuwa muda na wakati tusioujua tutaiacha dunia hii na hapo tutapaswa kutoa Hesabu ya maisha yetu. Tukitambua hilo tutakesha kwa Imani na uaminifu mkubwa katika kutimiza yale yote ambayo Mwenyezi Mungu ametuagiza kuyafanya kwa niaba yake kwa ajili ya wengine, yaani nyajibu zetu za kila siku kila mmoja kadiri ya wito ambao Mungu amemwita kumtumikia.
Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Hekima ya Sulemani 18:6-9. Kitabu cha Hekima ya Sulemani ni moja kati ya vitabu vitano vya Hekima katika Agano la Kale. Mwandishi wa kitabu hiki aliandika kwa Wayahudi waliokuwa uhamishoni huko Misri (diaspora Jews) mnamo katika karne ya 1 BC. Wakiwa uhamishoni, Wayahudi walipitia changamoto nyingi, kubwa wakati huu ikiwa ni tamaduni mpya kutoka kwa Wagiriki ambazo nyingi ziliwafanya wengi kuacha tunu muhimu za Imani yao kwa Mungu mmoja, Torati, sabato na sheria nyingine mbalimbali za dini yao ya Kiyahudi. Katika kujibu changamoto walizokuwa wanapitia, Mwandishi wa kitabu hiki anawapa moyo kwamba, Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake. Anawakumbusha jinsi Mungu alivyowakumbuka Baba zao walipokuwa utumwani Misri, akatimiza ahadi ya ukombozi aliyonena na Ibrahimu (Kutoka 11 na 12). Anawakumbusha namna Baba zao walipokesha usiku ule waliposubiria utimilifu wa ahadi ya Mungu kwao ya ukombozi kutoka utumwani. Walianza kusherehekea utimilifu wa ahadi ya Mungu kwa imani na furaha kubwa wakiamini kwa kuwa Mungu alishaahidi kuwakomboa watu wake.
Katika Somo la kwanza katika dominika ya leo tuna mafundisho mawili ya kujifunza. Kwanza: Imani thabiti kabla ya kuona matokeo. Somo la kwanza, mwandishi wa kitabu hiki cha hekima anaeleza namna Waisraeli walivyosherehekea usiku wa Pasaka kabla ya kutoka kwao utumwani Misri, wakiamini Neno la Mungu kupitia kiongozi wao Musa. Kwa Imani kuu walisherehekea na kuamini na kisha Mungu akatenda kile alichonena nao kwa kuwatimizia ukombozi wao kutoka utumwani Misri. Hivyo mwandishi anawapa moyo wayahudi ambao wakati huu walikua huko uhamishoni misri, katikati ya changamoto mbalimbali walizokuwa wanazipitia kwa wakati huo kwamba, Mungu ni mwaminifu na hawakupaswa kamwe kupoteza Imani na matumaini yao kwa Mungu. Ndugu mpendwa, mimi na wewe katika safari yetu ya maisha, tunapita katika nyakati zenye changamoto mbalimbali. Katika nyakati na changamoto zote hizo tunasali na kumwomba Mungu, tunayakabidhi yote mikononi mwa Mungu. Lakini ni hulka ya mwanadamu kutegeemea majibu ya haraka ya sala, maombi na juu ya hali mbalimbali tunazopitia katika maisha. Pengine, tunaona kama Mungu anachelewa kujibu sala zetu, na hapo tunaweza hata kushawishika kutafuta suluhisho mahali pengine. Somo hili la Hekima ya Sulemani linatufundisha kushikilia ahadi za Mungu hata kabla hatujaona uthibitisho wake. Hii ndio maana ya Imani kama tulivyosoma katika waraka kwa waebrania 11:1, “Kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.” Tusikate tamaa na wala tusipoteze matumaini. Sala zako, dua na maombi yako, Mwenyezi Mungu anasikia na kwa kuwa ni mwaminifu, atatenda kwa wakati wake. Mtakatifu Augustino wa Hippo anatufundisha kuwa, “Sala haimbadilishi Mungu, bali inatubadilisha sisi ili tuweze kupokea kila ambacho Mungu ameandaa kwa ajili yetu.”
Pili: Uhalisia wa hukumu ya mwisho na wito wa kukesha. Taifa la Israeli wakiwa utumwani Misri walishuhudia namna Mwenyezi Mungu alivyowakomboa watu wake na kuwaangamiza walikuwa waovu na watesi wao yaani Wamisri na hivyo walikesha. Mwandisho wa kitabu cha Hekima ya Sulemani anatupa fundisho kutoka katika somo hili juu ya uhalisia wa hukumu ya mwisho, kama tunavyokiri katika kanuni ya Imani yatu kwamba, Kristo atakuja tena kuwahukumu wazima na wafu. Wenye haki wataurithi ufalme ulioandaliwa kwa ajili yao tangu kuumbwa ulimwengu na wale waovu watapoteza neema ya kuupata uzima wa milele. Ndugu mpendwa, maisha yetu ya hapa duniani ni safari kuelekea mbinguni ulipo utimilifu wa ukombozi wetu. Kumbe maisha yetu hayaishii tu hapa duniani kwa kifo chetu bali kuna hukumu ya mwisho na maisha baada ya maisha haya. Kumbe tunapoishi ni muda wa kufanya uchaguzi, ni muda wa kujiandaa, ni muda wa kukesha na kujiweka tayari, viuno vyetu viwe vimefungwa na taa zetu ziwe zinawaka, nasi tuwe kama watu wanaomngoja Bwana. Maisha ya hapa duniani yatusaidie kujiandaa kuuendea uzima wa milele.
Tatu: Ushirika katika kusubiri Ujio wa Bwana. Taifa la Israeli walisherehekea Pasaka pamoja, wakisubiri katika umoja utimilifu wa ukombozi wao, wakiimba na kutolea sadaka. Ni mfano wa watumishi waaminifu waliosubiria na kushirikiana kwa pamoja mpaka Bwana atakaporudi tena kama anavyotufundisha Kristo katika somo la Injili Takatifu. Ndugu mpendwa, imani ya kweli hukua ndani ya jumuiya, kuanzia katika familia, katika jumuiya ndogondogo na katika Parokia zetu. Sisi sote tupo safarini. Tunajiandaaje kuhakikisha kuwa hatumwachi hata mmoja wetu nyuma sisi kama mahujaji wa matumaini? Imani katika familia yangu ipoje? Huenda mimi ninajitahidi katika imani ilihali watoto wangu, mke wangu, ndugu na jamaa zangu wamerudi nyuma kabisa kiimani, au hata wengine wameikana imani. Tunapaswa sote katika umoja wetu kutembea pamoja. Kushirikiana sote katika changamoto zetu mbalimbali ambazo tunakutana nazo, kwa imani na matumaini, lakini pia kumkaribisha Yesu atembee nasi ili tusimwache yeyote nyuma.
Somo la Injili: Ni Injili ya Luka Lk 12:32-48. Kristo katika somo la Injili Takatifu domimika iliyopita, Dominika ya 18 ya Mwaka C (Lk 12:32-48) aliwafundisha makutano nasi sote kwamba, uhai wetu, yaani hazina yetu ya kweli, haupo katika wingi wa mali au vitu tulivyo navyo. Alitufundisha kuwa maana halisi ya maisha ni jitihada ya kumfikia Mungu na kuupata uzima wa milele. Somo la Injili ya leo limegawanyika katika sehemu kuu nne. Sehemu ya kwanza (Lk 12:32-34), Kristo anatuhakikisha utimilifu wa Ahadi ya uzima wa milele na anatukumbusha juu ya kutokujishikamanisha sana na mambo ya ulimwengu huu (reassurance of the Kingdom and an invitation to detachment.) Sehemu ya pili (Lk 12:35-40) Kristo anatoa fundisho juu ya watumishi waaminifu (Parable of the Watchful Servants), waliotambua umuhimu wa kukesha na kujiandaa wakimngoja Bwana wao, taa zako zikiwa zinawaka na viuno vyao vikiwa vimefungwa. Ni wajibu wa kujiweka tayari kwa ujio wa Kristo muda na saa ambayo hakuna hata mmoja wetu anayeijua. Sehemu ya tatu (Lk 12:41-44) Kristo anafundisha juu ya wakili mwaminifu (The Faithful Steward) ambaye alitimiza kwa uaminifu yote aliyokabidhiwa kuyafanya na Bwana wake kwa ajili ya watu, na huyo Bwana wake alipokuja muda na saa asiyojua na akamkuta ametenda aliyostahili, atamweka juu ya mali yake yote. Mwaliko wa kuwa waaminifu kwa nyajibu tulizopewa na Mungu kwa ajili ya watu wake.
Sehemu ya nne (Lk 12:45-48) Kristo Yesu anatoa fundisho juu ya wakili aliyeshindwa kuwa mwaminifu (The Unfaithful Servant) kwa yale aliyokabidhiwa na Bwana wake kwa ajili ya watu. Ni mwaliko kwetu kutumia vyema nafasi tunazokabidhiwa na Mungu kwa ajili ya watu, kwa kutenda haki, kusema ukweli, kutodhulumu wanyonge, kutokandamiza wengine, kuwa na huruma nk. Kwa kuyanya hayo yote tutastahilishwa kuurithi ufalme ulioandaliwa kwa ajili yetu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Katika somo hili la Injili dominika ya 19 ya Mwaka C wa Kanisa tuna mafundisho sita ya kujifunza. Kwanza: Mwenyezi Mungu amekwishatuahidia uzima wa milele, kwa wale walio wadogo (The Kingdom is already the Father’s delight to give). Katika sehemu ya kwanza ya somo la Injili Takatifu, Bwana wetu Yesu Kristo anawaambia makutano kuwa, “Msiogope enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme” Kristo anawaita makutano “Kundi dogo” akionesha namna Baba wa mbinguni anavyowajali na kuwalinda wale ambao katika mtazamo wa kidunia wanaonekana wadogo na dhaifu. Licha ya kuonekana wadogo na dhaifu, hao ndio wakubwa katika ufalme wa Mbinguni na watafurahia kuingia katika furaha ya uzima wa milele. Ndungu mpendwa, Kristo anatukumbusha kuwa Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake. Ahadi alizonena na Ibrahimu na uzao wake amezitimiza kwetu kwa ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo, na atazitimiza kwao wote walio tayari kwa unyenyekevu kupokea Habari Njema ya ufalme wa Mbinguni. Ni mwaliko kwetu kuwa wanyenyekevu na kutambua udogo na udhaifu wetu mbele za Mwenyezi Mungu, kuwa kama Watoto wadogo ambao tumaini lao lote li kwa wazazi wao, nasi tuweke Imani na matumaini yetu yote kwa Mungu Baba yetu, Mungu anayejua mahitaji yetu yote, anayejua hatma ya maisha yetu. Tumwombe atukumbushe daima kutambua kuwa anatupenda na ametuandalia tayari zawadi ya ufalme wa mbinguni.
Pili: Mwaliko wa kutojishikamanisha ya mambo ya ulimwengu huu (An invitation to detachment). Katika sehemu hii ya kwanza ya Injili Takatifu, Kristo Yesu anawafundisha makutano umuhimu wa kutojishikamanisha na mambo ya ulimwengu huu. Anasema, “Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa na akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haiwezi kuharibu. Kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo itakapokuwapo mioyo yenu” Kristo anatuhakikishia kuwa Mbinguni ndipo mahali pekee palipo salama kuweka hazina yetu. Hakuna usalama katika kujishikamanisha na mambo ya ulimwengu huu kwa kuwa yote yatapita. Ndugu mpendwa, tunaishi katika ulimwengu ulijaa kila aina ya hofu juu ya hatma ya maisha yetu ya baadaye. Mara nyingi tunajiuliza maswali mengi, kwamba kesho yangu itakuwaje? Biashara zangu zitakuwaje? Ndoto na malengo yangu tayatimia? Je, miradi yangu itazaa matunda, je nafasi ya vyeo vyangu nitaendelea kuwa navyo? Mali zangu itakuwaje, je zipo salama? Pamoja na maswali mengine mengi ambayo yanahusu tu hatma ya maisha. Katika hayo yote tunapaswa kujiuliza swali moja la Msingi kwamba, mwisho wa mambo yote haya ninayoyahangaikia ni nini? Ndicho alichotufundisha Mhubiri katika Dominika iliyopita kwamba, yote ni ubatili, kwa kuwa tutakufa na tutayaacha hapa duniani. Kristo anatualika kujitahidi kutojishikamanisha na mambo ya ulimwengu huu bali hayo yote yatusaidie katika kuwekeza ilipo hazina yetu ya kweli yaani katika uzima wa milele. Kwa kufanya hivyo tutakua macho kila mara, na Kristo atakapokuja atatutkuta tupo tayari. Mali, majumba, magari, vyeo, fedha, zote tutaziacha. Ila roho tutabaki nayo milele, andaa roho yako, ili tuwe mahali salama baada ya maisha haya ya kupita.
Tatu: Tunaalikwa kukesha na kuwa macho kila wakati (Watchful Servants). Katika sehemu ya pili ya somo la Injili, Kristo anatualika kuwa macho, kukesha kama watumishi waaminifu wanaomngoja Bwana. Anasema, “Viuno vyenu viwe vimefungwa na taa zenu ziwe zinawaka, nanyi iweni kama watu wanaomngojea Bwana wao, atakapokuja na kuibisha wamfungulie mara” Ni mwaliko kwa wa kuwa macho, kusubiria saa ya wokovu vile kama wana wa Israeli walipokua macho kukesha wakisubiri kutoka utumwani Misri, au kama watumwa wanavyokesha wakisubiri Bwana wako atakaporudi ili wamfungulie mara, saa na muda ambao hawaujui. Ndugu mpendwa, Kristo anatualika sisi sote kukesha na kuwa macho kiroho tukisubiri kwa matumaini saa ya wokovu wetu. Kukesha katika maisha yetu ya kiimani ni kuwa tayari kiroho kwa kuishi kila siku kana kwamba Kristo anakuja kesho. Tukiishi namna hiyo basi tutatambua wajibu wetu wa kumpenda Mungu, wajibu wetu wa kuwapenda watu wote, bila masharti, bila kikomo, tutatambua wajibu wetu wa kusamehe, kuhurumia wengine na kutokua sababu ya kuumiza wengine kwa sababu ya uwezo, nguvu, Madaraka, mali, ushawishi, vyeo nk. Kukesha sio swala la kubashiri (paranoia) kwamba huenda ni leo au ni kesho, bali ni swala la kuishi maisha sasa na wakati huu. Hatuna muda wa kuahirisha, kesho haipo mikononi mwangu, na hivyo kila sekunde ya maisha yetu ni ya muhimu sana katika wokovu wetu. Kuna watu waliowahi kusema, nitakuja kesho na wala hawakufika, walisema nitamsamehe ndugu yangu kesho wala hakufikia, nitasaidia wenye shida kesho, wala kesho haikufika, nitashiriki misa kesho, nitaungama kesho, nitafanya Matendo ya huruma kesho, kesho si yangu wala si yako. Ishi vyema leo, tengeneza hatma ya maisha yako sasa hivi, mtafute Mungu leo maadamu anapatikana. Taa yako inawaka? Roho yangu ipo hai kwa njia ya Neno la Mungu lililo taa ya maisha yangu? Ninapokea sakramenti za kanisa?
Nne: Uaminifu katika kutekeleza mapenzi ya Mungu (faithful Stewards). Katika Sehemu ya tatu ya Injili (Lk 12:41-44) Kristo anafundisha juu ya wakili mwaminifu (The Faithful Steward) ambaye alitimiza kwa uaminifu yote aliyokabidhiwa kuyafanya na Bwana wake kwa ajili ya watu, na huyo Bwana wake alipokuja muda na saa asiyojua na akamkuta ametenda aliyostahili, atamweka juu ya mali yake yote. Mwaliko wa kuwa waaminifu kwa nyajibu tulizopewa na Mungu kwa ajili ya watu wake. Kristo alitoa fundisho hili akimjibu Petro aliyeuliza kama mafundisho hayo yaliwahusu wao tu au yaliwahusu watu wote. Fundisho hili linatuhusu wote tulio wafuasi wa Kristo. Ndugu mpendwa, kila mmoja wetu ni mtumishi aliyekabidhiwa wajibu na Kristo mwenyewe kwa ajili ya watu wake, kila mmoja Kadiri ya wito ambao Mungu amemwitia. Mtumishi mwaminifu aliyenenwa katika somo la Injili alitambua kuwa alipaswa kutimiza kwa uaminifu majukumu aliyokabidhiwa na Bwana wake. Je, ninatimiza vipi wajibu wangu niliokabidhiwa na Kristo kwa ajili ya watu? Kama Padre ninatimiza kwa uaminifu, majitolea, upendo na sadaka wajibu wangu kama mchungaji wa kundi la Mungu? Kama Baba wa familia, mama wa familia, kiongozi katika ngazi yoyote katika jamii, wapaswa kujihoji kila siku maswali haya. Tukitimiza nyajibu zetu kwa uaminifu basi atakapokuja atatuweka juu ya vitu vyake vyote, yaani tutarithi uzima wa milele pamoja naye. Nafasi ni sasa. Tumikia kwa uaminifu.
Tano: Ukosefu wa uaminifu katika ufuasi wetu utatufanya tuukose uzima wa milele (warning against Unfaithfulness and unaccountability). Katika sehemu ya mwisho ya Injili Kristo anatoa fundisho juu ya wakili aliyeshindwa kuwa mwaminifu (The Unfaithful Servant) kwa yale aliyokabidhiwa na Bwana wake kwa ajili ya watu. Wakili huyu alipoona Bwana wake anakawia kurudi akawapiga wajoli wake, wanaume na wanawake, akila na kunywa na kulewa, Bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. Kristo anatukumbusha kutokujisahau katika maisha yetu ya ufuasi. Ndugu mpendwa, mara kadhaa tunaweza kujisahau kwa sababu ya kiburi cha uhai, na kama nivyotangulia kusema, kiburi cha Madaraka, mafanikio, kiburi cha nguvu na vyeo na tukajisahau kutimiza yale tuliyopaswa kutenda kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya wengine. Mtumishi huyu alisahau kwamba alipaswa kuja kutoa Hesabu ya yote aliyokabidhiwa kufanya kwa niaba ya Bwana wake. Kumbe nasi pia tukitambua kuwa mwisho wa maisha yetu ya hapa duniani tutadaiwa Hesabu ya mambo yote tuliyokabidhiwa kwa ajili ya kundi la Mungu. Mtumishi huyu aliona kwamba alikua na muda bado mrefu wa kuweka mambo yake sawa kabla ya bwana wake kurejea. Ndugu mpendwa tunaloweza kufanya leo kama nilivyotangulia kusema tusingoje kesho. Tenda yote unayoweza kufanya leo, ungali bado na muda na wakati. Uhai huu si mali yetu, hapa duniani tupo katika nyumba ya kupanga, tupo safari na hatujui tutakufa lini. Weka mambo sawa. Shirikisha baraka alizokupa Mungu pamoja na wengine.
Sita: Aliyepewa vingi, kwake vitatakwa vingi pia. Mwisho Kristo anamalizia kwa kusema, “Na kila aliyepewa vingi, kwake vitatakwa vingi, naye waliyemwekea amana vitu vingi kwake huyo watataka na zaidi” Kristo alimaanisha hapa kuwa aliyepewa vingi ni yule aliyejaliwa karama, fursa, maarifa au nafasi ambazo Mungu ameweka mikononi mwetu. Ni kwa hao, vitatakwa vingi hali kadhalika, yaani watawajibika zaidi. Ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu ametuamini katika mambo mengi. Ametupa afya njema ya mwili na roho, ametupa nguvu za kufanya kazi, ametupa rasilimali mbambali, ametupa neema na baraka zake nyingi katika maisha yetu. Ametupia hivi vyote sisi tuvitunze na kuvifanyia kazi kwa niaba yake yeye mwenye mali, tukirehea mfano talanta katika Injili ya Mathayo 25:14-30. Je, ninazitumiaje neema na baraka hizi alizonijalia Mungu? Huenda nimeshindwa kuleta faida kadiri ya wingi wa karama alizonijali Mungu au kwa uzembe, au kwa ubinafsi, kutokujali, au kwa kutokuwajibika ipasavyo, au kwa ubinafsi na uchoyo, au kwa wivu na chuki nikashindwa kuwa mtu wa faida. Kristo atakaporudi atanidai kulingana na alichonipa. Tutumie vyema Zawadi hizi alizotukabidhi Mungu kwa niaba yake, tuwe waaminifu kweli ili kwa njia ya utumishi uliotukuka kwa yale aliyotukabidhi Mungu, yatustahilishe kuupata uzima wa milele.
Somo la Pili: Ni kutoka katika Waraka kwa Waebrania 11:1-2,8-19. Mwandishi wa waraka kwa waebrania aliandika waraka huu kuwa wakristo waebrania walikuwa wanapita changamoto kubwa katika imani yao, wakiishi katikati ya wale ambao walikua si Wakristo. Licha ya changamoto ambazo walikua wakizipitia, mwandishi anasihi kutokukata tamaa bali wawe na imani thabiti kwa mambo ya mbele aliyoahidi Mungu kama mababu waliotupa mfano bora wa kushika imani thabiti maishani mwao. Anatupa fundisho nini maana ya imani, kwamba ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo na ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Kumbe, nasi katika maisha yetu tunaposubiria utimilifu wa ukombozi wetu kwa ujio wa pili wa Bwana wetu Yesu Kristo, tunapaswa kuwa na imani thabiti. Hatupaswi kupoteza lengo msingi la maisha yetu. Tunaalikwa kukesha na kujiweka tayari ili Kristo atakapokuja atukute tupo tayari. Hitimisho: Katika dominika ya leo tumshukuru Mungi ambaye ni mwaminifu kwa ahadi zake kwetu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo alitimiza ahadi yake ya ukombozi wetu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti, akatuchagua kuwa urithi wake. Tuombe neema ya kutembea na Yesu katika safari yetu hapa duniani, kwa kukesha na kujiweka tayari kwa imani na uaminifu tukimngojea Bwana.