杏MAP导航

Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 19 ya Mwaka C wa Kanisa: Kesheni, Salini na tekelezeni dhamana na nyajibu zenu. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 19 ya Mwaka C wa Kanisa: Kesheni, Salini na tekelezeni dhamana na nyajibu zenu.   (Vatican Media)

Tafakari Dominika 19 ya Mwaka C wa Kanisa: Imani na Matumaini

Masomo ya dominika ya 19 ya Mwaka C wa Kanisa yamejikita katika kuimarisha imani ya wanaoelekea kukata tamaa, na waliokata tamaa kuwainua kwa kuwatia moyo kwa kuwa imani ni msingi na chanzo cha matumaini ya kweli na mwanzo wa uzima wa milele. Imani inatuonjesha furaha na heri ya mbinguni tungali bado tuko duniani, furaha ambayo Mungu Baba ametuahidia kwa Agano aliloliweka kwa njia ya Mwanae Bwana wetu Yesu Kristo. Imani na Matumaini!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 19 ya Mwaka C wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika ya 19 ya Mwaka C wa Kanisa yamejikita katika kuimarisha imani ya wanaoelekea kukata tamaa, na waliokata tamaa kuwainua kwa kuwatia moyo kwa kuwa imani ni msingi na chanzo cha matumaini ya kweli na mwanzo wa uzima wa milele. Imani inatuonjesha furaha na heri ya mbinguni tungali bado tuko duniani, furaha ambayo Mungu Baba ametuahidia kwa Agano aliloliweka kwa njia ya Mwanae Bwana wetu Yesu Kristo. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii unasema hivi; “Ee Bwana, ulitafakari Agano, usisahau milele uhai wa watu wako walioonewa. Ee Mungu, usimame, ujitetee mwenyewe, usiisahau sauti ya watesi wako” (Zab. 74 :20, 19, 22, 23). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, sisi tunathubutu kukuita Baba. Ututhibitishie moyoni mwetu neema ya kuwa wana wako, tupate kustahili kuingia katika urithi uliotuahidia.”

Waamini Dumuni katika Imani yenu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.
Waamini Dumuni katika Imani yenu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.   (Vatican Media)

Somo la kwanza ni la kitabu cha Hekima ya Sulemani (Hek 18:6-9). Kitabu hiki kiliandikwa kwa ajili ya Wayahudi walioishi nje ya Palestina – Diaspora –, na kiliandikwa kwa lugha ya Kigiriki na sio Kiaramaiki. Ni kwa sababu hii Wayahudi wa Palestina walikikataa kitabu hiki na kusema kuwa sio kitakatifu. Lakini lengo kuu la kitabu hiki ni kuwakumbusha vijana historia ya babu zao, na mambo makuu aliowatendea Mungu, ili kamwe wasimuasi na kufuata imani ya miungu ya watu wa mataifa mengine ya kipagani, iliyokuwako katika mazingira waliyoishi. Ni katika muktadha huu, ujumbe msingi katika somo hili unawakumbusha uaminifu wa Mungu kwa ahadi zake, kutayarishwa kwa babu zao kwa safari ya ukombozi kutoka utumwani Misri kwa mapigo mengi kwa Wamisiri, ikiwa ni pamoja na kuuawa kwa wazaliwa wao wa kwanza wa wanyama na watu, na mwanzo wa Pasaka yao wahayudi, walipomla mwanakondoo waliyemchinja na Mungu kuwaweka huru kutoka utumwani. Hivyo anawaasa wasifuate na kuiga njia potofu za dhambi za watu wa mataifa ya kipagani. Anawakumbusha kuwa Hekima ya kweli ni kufuata njia ya Mungu kwa uaminifu, kwa kuzishika ahadi zake, na kuwa maisha hayaishii hapa duniani kama watu wengine wanavyofikiri. Hivyo wasiionee aibu imani yao, ambayo imejaa historia ya utukufu. Zaidi sana Hekima ambayo Mungu anawapa watu wake, ni bora na kubwa kuliko hekima ya wanadamu wasomi wa dunia hii. Sisi nasi kwa imani tunapaswa daima kuwa tayari kwa saa ya kifo chetu na kwa ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa utimilifu wa ukombozi wetu kwa furaha, tukiwa tayari mda wote. Ni katika muktadha huu wimbo wa katikati unasema hivi; “Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi wake. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, wazingojeao fadhili zake. Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, na kuwahuisha wakati wa njaa. Nafsi zetu zinamngoja Bwana, Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu. Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe” (Zab. 32:1, 12, 18-19, 20-22).

Tangazeni na kuishuhudia imani yenu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake
Tangazeni na kuishuhudia imani yenu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake   (EPA)

Somo la pili ni la Waraka kwa Waebrania (Ebr 11:1-2, 8-19). Waraka huu waliandikiwa Wayahudi walioongokea ukristo waliokaa na kuishi nje ya Yerusalemu. Katika mazingira waliyoishi walikutwa na madhila na mateso mengi kwa kutengwa na Wayahudi wasio wakristo kwa kuonekana kuwa ni wasaliti wa imani yao ya kiyahudi – imani ya babu zao. Hali hii iliwafanya waukumbuke mji wao wa Yerusalemu na Hekalu lake, wakatamani kurudi. Sehemu ya somo hili, inawaimarisha na kuwatia moyo, wadumu katika imani yao kwa Kristo mfufuka kwa ajili ya uzima wa milele, wakifuata mfano wa babu zao wa imani Ibarahimu, Isaka na Yakobo. Kwani kwa imani Ibrahimu alikaa ugenini katika nchi ya ahadi. Kwa imani Sara alipata mtoto uzeeni akiwa na miaka 90, na Ibrahimu akiwa na miaka 100 (Mwa 17:17), na ni kwa imani Ibrahimu alikubali kumtoa sadaka mwanae wa pekee, akiamini kuwa Mungu ana uwezo wa kuwafufua waliokufa. Ndiyo maana tunamuita baba wa Imani. Ni katika muktadha huu anawaasa watambue kuwa Imani kwa Kristo ni ya thamani zaidi, kwani ni katika Yeye, Agano la Kale limitimilizwa, na Ukuhani wa Kristo ni mkuu kuliko ule wa makuhani wa Agano la Kale, na Sadaka ya Kristo ni bora zaidi kuliko ile waliyotolea makuhani wa Agano la Kale. Hivyo wadumu katika Imani hii, wasirudi kamwe katika imani ya zamani. Nasi tudumu katika hii imani kwa Yesu Kristo, tuliyoipokea kwa njia ya mitume, ndiyo hakika yetu ya maisha ya uzima wa milele mbinguni. Kwa maana; “Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Ebr. 11:1.)

Waamini tangazeni na kushuhudia Imani yenu kwa Kristo Yesu
Waamini tangazeni na kushuhudia Imani yenu kwa Kristo Yesu   (REUTERS)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk 12:32-48). Ujumbe mahususi katika sehemu hii ya Injili ni huu; tukiyavumilia mateso na mahangaiko yatokanayo na imani yetu, tukasisima imara mpaka mwisho, tutapokea tuzo ya maisha ya milele mbinguni, kuonana uso kwa uso na Mungu Baba. Katika kufikisha ujumbe huu, Mwinjili Luka ameweka pamoja misemo mbalimbali na mifano mitatu aliyoitoa Yesu katika mafundisho yake. Mfano wa kwanza ni wa mwenye nyumba anayerudi harusini usiku wa manane na kuwakuta watumishi wake wakimsubiri, naye kwa furaha anawahudumia. Mfano wa pili ni wa mwizi anayevamia kwa kuvizia ili asionekane, kusisitiza kuwa Mungu anapomtuma mjumbe wake, dada yetu kifo, hakuna anayejua. Na mfano wa tatu ni wa mtumwa mwema na mwaminifu, kusisitiza kuwa tayari mda wote. Lengo kuu la mifano hii ni kuwatia moyo na kuwafariji waamini waliokata tamaa kwa kukawia kuja kwa mara ya pili kwa Kristo Yesu kama alivyowaahidi, wakawa wanamsubiri kwa shauku kubwa aje awachukue na kuwapeleka mbinguni. Lakini mda ulizidi kupita, mateso na madhulumu yakipamba moto, wengi walipoteza mali zao, wengine kufungwa magerezani na wengine kuuawa. Hali hii ilipelekea wengine kukata tamaa na kuona kuwa ujio wa pili wa Yesu ni fundisho la uongo. Luka anawatoa shaka wachache waliobaki imara katika imani akiwaambia; “Msiogope enyi kundi dogo”, licha ya madhulumu na mateso mnayopata sasa, furahini, simameni imara, msikate tamaa, maana wale wanaowatesa hawawezi kuichukua furaha yenu ya uzima wa milele, mkisimama imara katika imani yenu mpaka mwisho.

Msiogope eny kundi godo!
Msiogope eny kundi godo!   (ANSA)

Nasi tukidumu imara katika Imani yetu mpaka mwisho, hakika tutastahilishwa kuingia katika uzima wa milele. Imani kwa Kristo Yesu ndiyo njia ya uhakika ya kufika mbinguni, kwani inatusaidia kujua jinsi tunavyopaswa kuishi maisha yetu, kuielewa na kuitikia miito yetu ikiwa ni pamoja na wito wa upadre, utawa, na ndoa, na namna ya kuendesha kazi na shughuli zetu na jinsi ya kuipenda, kuitunza na kuiheshimu miili yetu. Imani inatusaidia kujua namna tunavyopaswa kusali, kwa maana tunasali kadiri ya imani na tunaamini kadiri tunavyosali. Sala ni chazo cha imani na sala inaonyesha imani ya mtu. Imani ni sababu ya matumaini yetu. Imani yatusaidia kujua malengo ya maisha yetu na kutupatia mwelekeo na jinsi tunavyopaswa kuishi kwa sasa, na kutupatia maelezo ya matumaini kwa mambo ambayo hatuyaelewi kwa akili zetu hasa uwepo wa matatizo, magonjwa, mateso, na kifo, ikituelekeza kwenye uzima wa milele. Basi tudumu katika imani yetu kwa Mungu mmoja katika nafsi tatu aliyejifunua kwetu kama Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu, Imani ya Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, Imani inayotupa tumaini la kweli la maisha ya milele Mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali; “Ee Bwana, uwe radhi kuzipokea dhabihu za Kanisa lako. Umetupatia kwa huruma dhabihu hizi ili tukutolee; na kwa enzi yako unazifanya kuwa fumbo la wokovu wetu”. Na katika sala baada ya Komunyo anapohitimisha maadhimisho haya anasali hivi; “Ee Bwana, sakramenti yako tuliyopokea ituokoe na kututhibitisha katika nuru ya kweli yako”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D 19
08 Agosti 2025, 11:45