杏MAP导航

Tafuta

Tafakari Dominika ya 18 ya Mwaka C wa Kanisa: “Ombeni, jitenge na tamaa… kwa maana uzima wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo.” (Lk 12:15) Tafakari Dominika ya 18 ya Mwaka C wa Kanisa: “Ombeni, jitenge na tamaa… kwa maana uzima wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo.” (Lk 12:15)  (AFP or licensors)

Tafakari Dominika 18 Mwaka C wa Kanisa: Jilindeni na Uchoyo!

Kutokana na kuvunjika kwa misingi ya haki, amani na utulivu, watu wengi wanaanza kujiwekea mikakati ya kuwa na uhakika wa usalama wa maisha yao. Changamoto kwa waamini ni kujiwekea hazina yao mbinguni, mahali ambako wanauhakika wa usalama na wahakikishe kwamba , wanatumia mali na utajiri waliokirimiwa na Mungu kwa ajili ya kudumisha haki, amani, upendo na mshikamano hasa kwa wahitaji zaidi, jambo ambalo litawatajirisha machoni pa Mungu.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo Dominika ya 18 MWAKA C, Ni siku njema, tulivu, tukufu, siku ya Bwana, Dominika, tunamshukuru Mungu kwa mema ya juma hili. Kristo anatuongoza kutumia mali kwa faida ya roho akisema “angalieni, jilindeni na choyo.” Kutokana na vitendo mbalimbali ambavyo vinaashiria kuvunjika kwa misingi ya haki, amani na utulivu, watu wengi kwa sasa wanaanza kujiwekea mikakati itakayowawezesha kuwa na uhakika wa usalama wa maisha yao. Changamoto kwa waamini kujiwekea hazina yao mbinguni, mahali ambako wanauhakika wa usalama wa hazina hiyo pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatumia mali na utajiri waliokirimiwa na Mungu kwa ajili ya kudumisha haki, amani, upendo na mshikamano hasa kwa wahitaji zaidi, jambo ambalo litawawezesha waamini hao kujitajirisha machoni pa Mungu. Masomo haya yanatuuliza swali la msingi sana, Tunajenga maisha yetu juu ya nini? Je, tumaini letu ni la milele au la muda mfupi? Katika dunia ya sasa, Wengi wanahangaikia mali, hadhi, mafanikio ya muda. Wengine wamekata tamaa kwa sababu ya magonjwa, umasikini, au kupoteza kazi. Na wengine wanaishi kana kwamba hawatakufa kamwe. Yesu leo anatufundisha: “Jizoezeni kuwa matajiri kwa Mungu.” Kwa kawaida familia nyingi huwa katika amani na maelewano, hali hii huwa hadi lini? amani na utulivu hudumu hadi siku ya kugawana mirathi. Mbele ya fedha na mali akili hubadilika na rangi zote halisi huonekana. Katika fedha na mali tunajipatia upofu. undugu, ujamaa na urafiki wetu huingia doa, chuki hutawala na magomvi kutamalaki. Katika mazingira haya zaidi ni “maslahi” binafsi, kunyauka kwa ukarimu na zaidi sana kushamiri kwa ubinafsi na uchoyo.

Waamini jiwekeeni hazina mbinguni
Waamini jiwekeeni hazina mbinguni   (AFP or licensors)

Kwa msaada wa wenzetu wenye hekima tunaweza pata mwafaka lakini chuki ya ndani na kinyongo hubaki kwa miaka mingi wanafamilia/ukoo wakibaki bila salamu wala jambo... Kristo anatuasa, ‘jilindeni na choyo maana uzima wa mtu haumo katika uwingi wa vitu alivyo navyo,’na Muhubiri katika somo I (1:2; 2:21-23) akikazia kwamba yote “ni ubatili tena ubatili mtupu”. Mhubiri anasema: “Ubata mtupu… yote ni hewa.” Anahoji maana ya kazi, mali na bidii ambayo huishia kwa huzuni na mashaka. Yesu anatoa mfano wa tajiri mpumbavu aliyejenga maghala makubwa lakini akafa usiku huo huo. Mungu akasema: “Mpumbavu! Leo hii roho yako itachukuliwa…” Mwinjili Luka anasimulia kwamba Yesu aliombwa kusuluhisha mgogoro wa urithi, akakataa, “mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?” kwa nini hakutaka kujihusisha na jambo hili? Je, ni kutokujali shida za watu? hapana, alitamani kuingia katika mzizi wa tatizo na kulizungumzia kwa uzito wake. Kiini cha mgogoro kilikuwa uchoyo na ubinafsi na ndio kisa anaanza kwa kuonya “angalieni...” Hiyo ni tahadhari, sawa na kusema “jihadhari na majambazi, jitunze chuki, kisasi, kujilimbikizia mali, na uonevu kwa wasio na mamlaka vinazuilika, zingatia hapo unapopapenda pana tatizo, kuwa makini dunia leo ni ya moto... angalieni jilindeni na choyo”. Hili linafafanuliwa kwa mfano wa mkulima tajiri mwenye mavuno mengi shambani, anaanza kufanya hesabu, “nifanyeje maana store yangu ni ndogo, nitaibomoa na kujenga kubwa halafu nitaiambia nafsi yangu, kula, kunywa na ufurahi…” Zaburi 33:10 inasema “Mungu hupangua mipango ya mataifa na kuyabatili mawazo yao,” katikati ya mipango mikakati hii, usiku huu huu wanataka roho yako... hakika ni ubatili, basi jilindeni na choyo.

Mfano wa Tajiri Mpumbavu: Jiwekeeni hazina mbinguni
Mfano wa Tajiri Mpumbavu: Jiwekeeni hazina mbinguni

UFAFANUZI: Mhubiri aliona utajiri na kazi kama mwendo wa upepo unaofuatwa lakini haukamatwi. Anatufundisha kuwa bila Mungu, hata mafanikio makubwa hayawezi kutupa amani ya kweli. Katika muktadha wa maisha ya leo: Hali ya uchumi inayoyumba, rushwa, mashindano ya kijamii yote yanatuonyesha kuwa mali pekee haina uwezo wa kuleta tumaini la kweli. Papa Leo XIV anasema “Tumaini la kweli si mali unayokusanya, bali ni huruma unayotoa.” Nampenda mkulima huyu tajiri... ni mtu makini anayeona mbali, ana bahati njema, hajamuibia mtu, anajua ni lini afanye kazi na lini atulie, kupumzika na kustarehe, akili njema. Hata hivyo Mungu hampi nafasi ya kutulia na kufurahia matunda ya kukusanya kwake mali, tatizo ni nini? amekosea wapi? Tatizo ni moja tu… sio mali, sio store kubwa ila ni moyo uliojaa choyo, ubinafsi na kupungukiwa ukarimu na upendo. Moyo, roho, akili, utashi na nafsi nzima ya bwana huyu vilijaa mavuno tu basi. Katika mtu huyu hakuwemo mkewe, watoto wake, jirani, rafiki wala jamaa zake, hakuwamo hata Mungu, kilichoujaza moyo wake ni ngano tu, basi. Baada ya mavuno mali ndio ilikuwa baba yake, mama yake, mke wake, mtoto wake naam, mali ilikuwa kila kitu kwake. Mali ilikuwa kwake mungu wa kuabudiwa na kusujudiwa, naye aliacha kuwa mtu akafanana na mashine yenye kuzalisha tu mali, akafanana na kitabu cha mapato na matumizi, ndio, kijitabu cha risiti basi, amepoteza mwelekeo wa maisha na utu wake hanao tena. Ndio maana Yesu anaasa, jilindeni na choyo, uzima wa mtu haumo katika wingi wa mali alizonazo na Muhubiri anacheka akisema, “yote ni ubatili, tena ni ubatili mtupu.”

Vijana wekezeni kwenye mambo ya kiroho
Vijana wekezeni kwenye mambo ya kiroho   (@Vatican Media)

Mtume Paulo anatuambia “Mlivyofufuliwa pamoja na Kristo, tafuteni yaliyo juu. Tunaitwa kuishi kwa maadili mapya kusamehe, kutunza utu wa wengine, kuepuka tamaa za kidunia. Katika maisha ya kila siku, Ni rahisi sana kufungwa na ‘utambulisho wa kimwili’ kazi, elimu, mitandao. Paulo anatuita tujitoe kwa upya – mtu mpya anayeishi kwa Kristo. Jubilei ya Matumaini 2025 inahimiza kufufua utu wa ndani, kwa kutubu, kusamehe, na kuanza upya. Yesu anasimulia juu ya tajiri aliyefanikiwa sana, lakini akashindwa kuishi kwa hekima. Alijijengea maghala makubwa, akajivunia mali yake, lakini hakutambua kuwa usiku huo atakufa. Ujumbe wa Yesu, Mali si tatizo, bali mtazamo wetu kuhusu mali. Watu wengi ni matajiri wa mali, lakini maskini kwa Mungu Katika muktadha wa sasa: Tunajiuliza: Ni akiba gani ninaweka kwa Mungu? Je, maisha yangu ni ya kutoa au ya kujikusanyia? Papa Leo XIV anahimiza “Kanisa lenye moyo wa kutoa,” si kujikusanyia. Anasema “Tumaini linaishi pale ambapo moyo wa mwanadamu unajifunza kushiriki na wengine.” Lakini kutafuta mali na kuweka akiba ni dhambi? Hapana. Kristo hajakataza mali mahali popote ila daima anaasa hatari ya kupoteza nafsi zetu katika mali na kumuacha Mungu. Tazama, kati yote aliyowaza mtu huyu yanayotawala ni “mimi, yangu, zangu, vyangu.” William Barclay anasema “yangu” ni kiwakilishi katili, ishara ya choyo na ubinafsi. Mali itupe hali njema ya maisha na kuwa daraja ya kutuvusha ng’ambo ya pili, mbinguni kwa Baba. tuombe neema ya ukarimu tukiwashirikishana tunayojaliwa pasi na mastahili yetu.

Wkezeni katika haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi
Wkezeni katika haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi   (@Vatican Media)

Uchoyo ni tabia ya kutokutoa kitu kwa mwingine kama msaada au zawadi, unyimi, mkono wa birika. Inaweza pia kuwa ulafi wa vitu au kufanya moyo kuwa mgumu mbele ya mwingine, ni kufumba mkono mbele ya mhitaji (Kumb 15:7-8). Biblia inatumia choyo kwa namna mbili, mosi ni moyo wa kujitafutia vitu au mali, choyo hii husababisha kudhulumu, kupunja na kufunika haki za wengine. Pili ni choyo katika kutumia vitu vilivyopo, hapa ubahiri hutawala mmoja akizuia kabisa vitu visitoke kwenda kwa mwingine kama zawadi au msaada, ‘jilindeni na choyo, kwani yote ni ubatili tena ni ubatili mtupu.’ Swali la changamoto lingekuwa ‘mioyo yetu imejaa nini?’ Kwa mfano ukiona baba na mama wanavaa vizuri ilhali watoto wao ndio hivyo tena ujue ni uchoyo tu na si kingine. Aidha, ukiona baba anapata fedha na hajali hali njema ya familia badala yake ananywea pombe, anahonga au hata haijulikani anafanyia nini na ana madeni yasiyojulikana basi tambua kilichopo hapo ni uchoyo... Kama mama anapenda fedha za familia zitumike kununua kila toleo la vitenge, au anataka mshahara wa baba utumike kujengea na kufanya mambo ya familia wakati yeye mshahara wake anajua mwenyewe anavyoutumia, mama huyu ni mchoyo. Kwenye shule ya boarding nguruwe au ng’ombe anachinjwa walimu na wapishi wanafaidi minofu wakati wanafunzi wanaambulia mifupa na mafuta tu ujue hapo kuna uathirika wa uchoyo.

Jiwekeeni hazi mbinguni
Jiwekeeni hazi mbinguni   (@Vatican Media)

Katika mazingira hayo ni nani basi anastahili kuitwa “mkristo?” Kristo alikuwa mkarimu, hakujenga ghala kubwa ya kuhifadhia nafaka wala hakuwa na akaunti kubwa Bank, aliwakaribisha na kuwahudumia kwa kauli, kwa kitu na kwa vitendo wakoma, vipofu, wagonjwa na wadhambi. Padre asiye mkarimu, kiongozi H/walei asiye mkarimu, mwanachama wa chama cha kitume/sala asiye mkarimu asiyeweza kuchukuliana na wenye dhiki, fukara, ombaomba au wadhambi wowote wale wanaodharauliwa na watu japo kwa kauli na lugha nzuri huyo asijiite “mkristo.” Uchoyo ni unajisi, ni ngumu kuwa mchoyo na kuuona ufalme wa mbinguni, Mt. Paulo katika somo II (Kol 3:1-5,9-11) anatuomba tutafute yaliyo juu Kristo aliko na namna mojawapo ya kutenda hilo ni kujilinda na choyo na kuwa wakarimu kama Mungu katika Kristo alivyo... Mwito wa Jubilei ya Matumaini 2025 Katika mwaka huu maalum wa neema, tumealikwa, Kuweka tumaini letu kwa Mungu si kwa maghala ya dunia. Kujivua utu wa kale – chuki, tamaa, majivuno. Kuwa watu wa kushiriki mali, huruma, na matumaini kwa wengine. Leo Yesu anatufundisha kuwa: Tajiri wa kweli si yule mwenye maghala makubwa, bali yule anayejiaminisha mbele ya Mungu, mwenye moyo wa huruma, ukarimu, sala, na toba. Katika Jubilei ya Matumaini, tumeitwa kuwa mashahidi wa tumaini si kwa maneno tu, bali kwa maisha yenye kuelekeza mbinguni. “Ombeni, jitenge na tamaa… kwa maana uzima wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo.” (Lk 12:15), Tuchague leo kuwa matajiri wa Mungu – tusafishe moyo, tushiriki, na tuishi kwa matumaini. Amina.

Liturujia D 18 Mwaka C
02 Agosti 2025, 10:07