杏MAP导航

Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 18 ya Mwaka C wa Kanisa: Waamini jiwekeeni hazina ya kweli mbinguni. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 18 ya Mwaka C wa Kanisa: Waamini jiwekeeni hazina ya kweli mbinguni.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 18 ya Mwaka C Kanisa: Jiwekee Hazina ya Kweli Mbinguni

Mama Kanisa anatualika “Kujiwekea hazina ya kweli mbinguni.” Mwanadamu katika maisha yake ya hapa duniani anajishughulisha katika kutafuta mambo mengi: afya njema, mali, utajiri, maendeleo, usalama, sifa, heshima, familia, marafiki na mambo mengine mengi. Mambo yote haya yanakoma pale mwanadamu anapofikia ukomo wa maisha yake ya hapa duniani, kwa kifo chake. Kumbe tunapoyatafuta mambo ya ulimwengu huu yanayopita, tunapaswa kumtafuta Mungu!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 18 ya Mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 18 ya Mwaka C wa Kanisa inatualika, “Kujiwekea hazina ya kweli mbinguni” Mwanadamu katika maisha yake ya hapa duniani anajishughulisha katika kutafuta mambo mengi, afya njema, mali, fedha, utajiri, maendeleo, usalama, sifa, heshima, familia, marafiki na mambo mengine mengi. Mambo yote haya yanakoma pale mwanadamu anapofikia ukomo wa maisha yake ya hapa duniani, kwa kifo chake. Kumbe tunapoyatafuta mambo ya ulimwengu huu yanayopita, tunapaswa kumtafuta Mungu aishiye milele. Ndivyo anavyotufundisha Mhubiri katika somo la kwanza (Mhu 1:2; 2:21-23).  Kristo katika somo la Injili Takatifu (Lk 12:13-21), Yesu anawafundisha makutano na anatufundisha nasi sote kwamba, uhai wetu haupo katika wingi wa mali au vitu tulivyo navyo, ambavyo tunavihangaikia usiku na mchana kwa nguvu na jitihada nyingi, bali upo katika kuutafuta uzima wa milele, yaani kumtafuta Kristo, kuishi na Kristo na kufa katika Kristo. Mtume Paulo katika somo la pili (Kol 3:1-5,9-11) anahitimisha kwa kutukumbusha thamani ya maisha yetu, kwamba, kwa kubatizwa, tulikufa na kufufuliwa pamoja na Kristo na hivyo hatupaswi kuhangaikia tu kuyatafuta na kuyafuata mambo ya ulimwengu huu, bali kuyatafuta yaliyo juu mbinguni Kristo alipo.  Maisha haya ni maandalizi ya ulipo uraia wetu wa kudumu yaani mbinguni.

Waamini wanaalikwa kuwekeza katika mambo ya mbinguni
Waamini wanaalikwa kuwekeza katika mambo ya mbinguni   (@Vatican Media)

Somo la Kwanza: Ni kutoka katika kitabu cha Mhubiri 1:2; 2:21-23. Kitabu cha Mhubiri (Ecclesiastes/ Quoheleth), ni moja kati ya vitabu vitano vya Hekima katika Agano la Kale. Mwandishi wa kitabu hiki ni Mfalme Sulemani, Mwana wa Daudi aliyekuwa Mfalme wa Israeli, wataalamu wa Maandiko Matakatifu wakituambia pengine ni katika uzee wake aliandika kitabu hiki (Mhu 1:2, 12-18; 2:1-11). Mwandishi wa kitabu hiki anazungumzia hasa juu ya maisha kwa mtazamo wa hekima ya kidunia na kutafakari juu ya mambo ya ulimwengu. Mhubiri anapingana na mtazamo wa kale wa kiulimwengu juu ya hekima, ambapo watu waliamini kwamba, mafanikio ya kweli yapo katika kutafuta hekima ya kibinadamu (yaani maarifa, akili au busara ya kidunia.) Hekima hii waliamini kwamba ilipelekea kuleta maana halisi ya maisha, yaani furaha ya kweli, amani, haki, utulivu wa nafsi, maisha marefu, heshima, faraja, familia kubwa nk, ambazo hizi zilikua ni ishara za nje kwamba mtu huyu amebarikiwa na Mungu (signs of secure existence). Na aliyekosa haya alionekana kama amelaaniwa na Mungu. Mhubiri sio kwamba anaikataa kabisa hekima ya kibinadamu, ila anatoa changamoto katika uelewa huu wa kale. Anatuambia kuwa mwanadamu mambo yote anayoyatafuta ambayo katika ujumla wake ndio ishara ya hekima ya kweli, yanakoma pale anapokufa, na yafuatayo baada ya hapo hayajui tena. Je, mhubiri anatukatisha tamaa? Ni kwamba mambo yote tunayoyahangaikia hapa duniani hayana maana? Je, kwa kuwa tunajua kwamba sote tutakufa, tusihangaike katika kutafuta kuboresha maisha yetu ya sasa na ya vizazi vijavyo?

Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya uadilifu na utakatifu wa maisha
Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya uadilifu na utakatifu wa maisha   (@Vatican Media)

La hasha. Mhubiri anatupa moyo, kwamba, katika hayo yote tunapaswa kutambua nafasi ya Mungu, kumtegemea yeye na kuitafuta Hekima ya kweli itokayo kwake. Tukitambua ufupi wa maisha yetu na kwamba yote tuliyo nayo yametoka kwa Mungu na ni ya kupita tu, tutatambua hitaji la kuwa na Mungu asiyepita kamwe. Ndugu mpendwa, unapotafuta maisha ya dunia hii, kumbuka kumtafuta Yesu, kuishi na Yesu na kufa katika Yesu, hiyo ndio maana ya maisha, kwa kuwa utaishi milele.Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo manne ya kujifunza. Kwanza: Hekima ya kibinadamu haiwezi kuelewa mipango ya Mungu. Mhubiri anatufundisha juu ya hekima ya kibinadamu namna isivyo suluhisho la mambo yote yahusuyo maisha ya mwanadamu kama ilivyokuwa katika uelewa wa kale. Anatukumbusha kuwa katika maisha haya, hata wenye hekima, ufahamu, mali, utajiri, nguvu, ushawishi, vyeo nk, hawawezi kamwe kuelewa mipango ya Mungu, na kwamba maarifa ya mwanadamu yana mipaka. Ndugu mpendwa, hekima ya hapa duniani siyo suluhisho la hatma ya maisha yetu. Tunaweza kufanya mambo mengi sana, tunaweza kupambana kwa nguvu nyingi na muda mrefu kwa ajili ya kujijenga katika ulimwengu huu, tukapata elimu kubwa, tukafanya kazi zetu kwa bidii na maarifa, tukatafuta majina mazuri, vyeo na madaraka, tukajijengea historia nzuri, CV inayovutia machoni pa watu, tukafanikiwa kuwa na familia kubwa, yenye mafanikio. Lakini pia tunaweza kujilaumu mara nyingi kwa vile tulivyo, tukalaumu kwa nini pengine hatujafanikiwa kutimiza malengo yetu maishani, hatujafanikisha mipango yetu mbalimbali nk.

Ujana pia ni utajiri na amana ya maisha
Ujana pia ni utajiri na amana ya maisha   (@Vatican Media)

Tunapofanya haya yote, tufahamu hakika ya kuwa hiyo ni mipango yetu. Je, vipi kuhusu mipango ya Mungu? Nimemshirikisha Mungu katika hayo yote? Je mpango wa Mungu ni upi katika kutafuta haya yote ninayohangaikia katika ulimwengu huu? Je, ninapambana kutafuta maendeleo yangu na kufanikisha mipango yangu ilihali ninawaumiza wengine, sitendi haki, nadhulumu, napora haki ya wengine, nawakandamiza wengine, nawadharau na kuwaona kama wamelaaniwa na Mungu, na kujisifia juu ya mali, maendeleo na mafanikio yangu? Mipango yetu si mipango ya Mungu. Mshirikishe Mungu katika kila jambo unalotenda, katika kila mpango wa maisha yako, tenda haki, kuwa mwema, hurumia, jali, saidia wengine. Mshukuru Mungu kwa kila linalotokea katika maisha yako.  Tusali pamoja na mzaburi katika Zaburi ya 139:1-3, Ee Mungu wangu umenichunguza, ukanifahamu nilivyo mimi, wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu, ulifahamu wazo langu tokea mbali, umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, umeelewa njia zangu zote. Pili: Hekima ya kidunia haitoi uhakika wa furaha wala mafanikio. Mhubiri anatoa mtazamo wa tofauti kabisa juu ya Hekima ya kibinadamu. Anasema mambo yote ni ubatili mtupu. Anaendelea kusema,“Katika wingi wa hekima kuna msiba mwingi, na yeye aongezaye maarifa huongeza huzuni” (Mhu 1:18). Kadiri mtu anavyojua zaidi ndivyo huzuni na kuchanganyikiwa huongezeka. Kwa kuwa siku zake zote ni masikitiko, na kazi yake ni ya huzuni, naam hata usiku moyoni mwake hamna raha.

Tafakari kuhusu tajiri mpumbavu
Tafakari kuhusu tajiri mpumbavu   (©Dan74 - stock.adobe.com)

Ndugu mpendwa, mara nyingi tunawaza kupambana kutafuta maisha na hiyo ni ndoto ya kila mmoja kwamba, nipige hatua kubwa kimaendeleo, nipate utajiri, nifanikiwe katika maisha. Ni kiu na shauku ya kila mmoja. Mhubiri anatuambia ya kuwa, hayo yote bila Mungu ni chanzo cha huzuni, hofu na kuchanganyikiwa kwa kuwa tutawaza tu juu ya mwisho wa mambo hayo yote kwa mtazamo na jicho la kidunia. Ila kama tutawaza yote kwa jicho la Kimungu, hapo tutaona maana ya maisha haya na hatutakua na hofu na mashaka yoyote. Tutashukuru pale Mungu atakapotubariki na kutuinua na kutambua kuwa kuwa sio sisi bali ni Mungu. Tutashukuru hata asipotubariki leo kwa kuwa tutatambua kuwa Mungu anafahamu hatma yangu, anaona mapambano yangu, anaona jitihada yangu, anafahamu kesho ya maisha yangu na hivyo sina hofu nikiwa naye. Nje tunaweza kuonekana dhaifu lakini ndani ya mioyo yetu tukawa na furaha isiyo kifani kwa kuwa tumekabidhi maisha yetu yote kwake yeye atutiaye nguvu.

Mungu ndiye asili ya afya njema, wema na utajiri wetu
Mungu ndiye asili ya afya njema, wema na utajiri wetu   (AFP or licensors)

Tatu: Hekima ya kidunia si kinga dhidi ya kifo wala utupu wa maisha. Mhubiri anatukumbusha kuwa mwisho wetu sote ni kifo, anasema,“Kama ilivyo kwa mpumbavu, ndivyo itakavyokuwa kwa mimi pia, yaani kwake mwenye hekima, kwamba sote tutakufa. Hata nikasema moyoni mwangu, hali hii ni ubatili pia” (Mhu 2:15). Katika historia ya Falsafa, alikuwepo Mfalme maarufu sana ulimwenguni aliyeitwa Alexander Mkuu (356-323 BC). Huyu alikua mfalme wa Macedonia huko Ugiriki na alifanikiwa kutengeneza himaya kubwa kuwahi kutokea katika historia na kueneza kwa kasi utamaduni wa kigiriki uliwenguni kwa wakati huo. Mfalme huyu katika miaka yake 32 tu aliyoishi, alifanikiwa kuwa maarufu sana kwa kupata utajiri mkubwa na kuyashinda mataifa mengi na kuyaweka chini ya utawala wake. Licha ya hayo yote, kabla ya kifo chake, akiwa na umri wa miaka hiyo 32 tu, aliomba mambo matatu makubwa yafanyike siku ya mazishi yake. Kwanza aliomba mikono yake ibaki ikining’inia nje ya jeneza ili kuonesha kwamba alikuja duniani mikono mitupu na ataondoka mikono mitupu na hawezi kuchukua chochote hapa duniani. Pili aliomba daktari wake ndiye abebe jeneza lake ili kuonesha kuwa hata madaktari wakuu hawawezi kuzuia kifo na maisha yapo mikononi mwa Mungu. Tatu aliomba barabara atakayopitishwa itandazwe dhahabu, fedha na vito vya thamani ili kuonesha kuwa mali zote alizozipata duniani hazina maana yoyote mbele ya kifo. Tukitambua kuwa sote tutakufa, tutakuwa wanyenyekevu na kutambua nafasi ya Mungu na nafasi ya wengine. Tulikuja duniani mikono mitupu na hivyo hivyo tutayaacha maisha haya ya hapa duniani. Jitahidi kuwa chanzo cha furaha, amani, tabasamu, upendo na matumaini kwa wengine. Fungua mikono yako, saidia wenye shida hata kwa kidogo ulicho nacho, fungua macho yako, ona mahangaiko na misalaba ya wengine, fungua moyo wako, hisi maumivu wanayopita wengine, nyanyua miguu yako, tembelea wangonjwa, wazee, yatima. Hiyo ndiyo hazina tunaweza kujiwekea mbinguni kupitia zawadi hii ya maisha Mungu aliyotupatia.

Tajiri alimsahau Mungu, aliwasahau majirani na kujiangalia peke yake
Tajiri alimsahau Mungu, aliwasahau majirani na kujiangalia peke yake   (@Vatican Media)

Nne: Maisha hayana maana bila Mungu. Mhubiri anatupa moyo kwamba, ili mambo yote tunayofanya yawe na maana, twapaswa kumpa Mungu nafasi ya kwanza kama nilivyotangulia kusema hapo mwanzo. Mhubiri anatofautisha hekima na kidunia na ile ya Kimungu kwamba, mwenye kuitafuta hekima ya Kimungu atatambua nafasi ya Mungu. Anatuambia katika sura ya mwisho kabisa ya kitabu hiki kwamba, “Mwisho wa maneno yote, umesikia haya: Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, maana ndiyo impasavyo kila mtu (Mhu 12:13.) Ndugu mpendwa, mhubiri alikua na vitu vyote lakini aliona vyote ni ubatili na havina maana. Nabii Yeremia anatuambia amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amyfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Mungu. Kuna hatari kubwa sana ya kuelekeza mioyo, nguvu, akili na roho katika mambo ya dunia hii pekee. Huenda katika mali, katika umaarufu, katika, utajiri, katika tamaa, pengine tukaweka matumaini yetu kwa watu, au kwa vitu na kusahau nafasi ya Mungu. Haya yote hayawezi kutuletea uzima wa roho zetu bali kama tumemwacha Mungu aliye chanzo na sababu ya kuwepo kwetu hapa duniani.

Tajiri aliwekeza kwenye vitu na kusahau utu wa binadamu
Tajiri aliwekeza kwenye vitu na kusahau utu wa binadamu   (AFP or licensors)

Somo la Injili: Ni Injili ya Luka Lk 12:13-21. Kristo Yesu katika somo la Injili Takatifu (Lk 12:13-21) anawafundisha makutano nasi sote kwamba, uhai wetu kumbe haupo katika wingi wa mali au vitu tulivyo navyo. Anatufundisha kuwa maana halisi ya maisha ni jitihada ya kumfikia Mungu. Katika tamaduni ya wayahudi, Walimu yaani Rabbi, waliombwa mara kwa mara kusuluhisha migogoro iliyokua inatokea kati ya ndugu katika jamii. Waliamua kesi hizi kwa kutumia sheria ya Musa, yaani Torati. Katika mambo yaliyohusu mgawanyo wa urithi katika familia iliyokuwa na wana wawili, yalipatikana katika vitabu vya Kum 21:15-17, Hesabu 27:1-11; 36:7-9 ambapo 2/3 ya mali alipewa mwana mkubwa na 1/3 ya mali alipewa yule mdogo. Ikiwa familia ilikua na wana wengi basi yule wa kwanza alipokea mara mbili ya yule mdogo na hapo aliwekwa kama msimamizi wa familia katika nafasi ya Baba. Katika somo la Injili ya leo, anakuja mtu mmoja katika mkutano, mwenye moja kati ya kesi tajwa hapo juu. Huenda aliyekua mwana mkubwa alichelewesha sehemu ya mali aliyopaswa kupewa mwana mdogo, au pengine mwana mdogo alilalamika kwa vile kaka yake alivyopata mara mbili ya urithi ambao yeye alipata. Yesu anakataa kuwa msuluhishi juu ya swala hilo kwa kuwa, yeye alikuja kutuletea Habari Njema, na kuwaleta watu karibu zaidi na Mungu, kwa kushirikishana upendo. Anatumia tukio hili kutufundisha kuwa, mambo yote hayo tunayoshikamana nayo na kuyang’ang’ania hayana maana sana katika kuupata uzima wa milele, tusipotambua nafasi ya Mungu.

Inalipa kuwekeza imani kwa vijana
Inalipa kuwekeza imani kwa vijana   (AFP or licensors)

Katika somo hili la Injili dominika ya leo tuna fundisho moja kubwa na mafundisho matatu ndani yake. Kwanza: Kristo anatufundisha kutafuta utajiri katika mambo yenye maana kwa Mungu (richness in what matters to God). Katika somo la Injili, Kristo anamjibu mtu yule katika makutano aliyekuja kulalamika juu ya urithi wake kwa kutoa mfano wa Tajiri mpumbavu. Kwa nini Kristo anamwita tajiri huyu ni mpumbavu? Katika tamaduni za wayahudi, kazi njema zilijumuisha kusali, kufunga na kutoa sadaka kwa ajili ya kusaidia maskini. Mwenyezi Mungu alimbariki tajiri huyu kwa mavuno mengi, lakini tajiri huyu akasahau kuwa ni Mungu alimbariki, kwamba ni Mungu alimpatia yote yale na kwamba alipaswa kumrudishia Mungu Shukrani kwa kusali, kushukuru na kutoa kwa ajili ya maskini ambao hawakua na chochote. Kinyume chake anaamua kukumbatia anasa, kula, kunywa na kufurahi. Alisahau mambo matatu. Kwanza: Mungu ndiye mmiliki wa kila kitu alichokuwa nacho; Tajiri huyu anasahau kuwa Mungu ndiye mmiliki wa kila kitu alichokua nacho, mali, mavuno, na utajiri wote na hata maisha yake pia. Alikuwa tu mtumishi aliyekabidhiwa hayo kwa niaba ya Mungu na alipaswa kuwa mwaminifu kwa aliyempatia hayo yote. Alijiwaza yeye mwenyewe. Anasema wazi kuwa mazao yake yamezaa sana na hana mahali pa kuweka zaidi kwa kuwa ghala zake zote zilikwisha jaa. Anawaza kuvunja ghala zake ili ajenge kubwa zaidi. Ndugu mpendwa, hali hii ya tajiri huyu yanihusu mimi na wewe. Mungu ametupa nguvu, afya, akili, maarifa, utajiri, karama, vipaji na baraka mbalimbali kadiri apendavyo, na kwa kiasi alichopenda kutupatia kila mmoja wetu. Je, ninakumbuka kumshukuru kila mara kwa neema na baraka zake nyingi ambazo amenijalia? Nakumbuka kumtolea Mungu Shukrani kwa matoleo na zaka kwa neema na baraka hizo nyingi?  Tajiri huyu alimsahau Mungu, alisahau kushukuru. Ndugu mpendwa, mafanikio yako, karama, vipaji, visikufunge macho ukasahau nafasi ya Mungu.

Hakikisha kwamba Moyo wako una nafasi kwa matendo ya huruma
Hakikisha kwamba Moyo wako una nafasi kwa matendo ya huruma   (MATTEO CIAMBELLI)

Pili: Aliwasahau wengine (He forgot others). Tajiri huyu mpumbavu alijaza ghala zake na hakua na nafasi ya kuweka kitu chochote tena. Alikua na vingi lakini hakua tayari kutoa kwa ajili ya wengine, akaona ni vyema avunje ghala ili aendelee kulimbikiza kwa ajili yake peke yake.  Ndugu mpendwa, Ghala yako ndio baraka na neema mbalimbali Mungu alizokujalia, ndio afya njema Mungu aliyokupa, ndio utajiri Mungu aliokupa, ndio mali Mungu alizokupatia. Je, katika wingi wa baraka hizo unawakumbuka wengine? Wakati ninapowaza kununua nguo mpya ilihali nina nguo sijazivaa mwaka mzima ndani ya masanduku yangu, wapo wengine wenye nguo moja tu. Wakati ninapowaza kumwaga chakula kwa kuwa nimeshiba mimi na familia yangu, wapo wengine wanaolala bila kula, wapo wanaokufa kwa njaa na utapiamlo. Je, ninagawa baraka za Mungu kwa wengine? Ghala yangu ya yako yaweza pia kuwa ni moyo wangu. Huenda moyo wangu hauna nafasi yoyote kwa ajili ya wengine, umejaa, hauna nafasi kwa ajili ya Mungu, hauna nafasi kwa ajili ya maskini, wagonjwa, wajane, yatima, hauna nafasi kwa ajili ya wenye njaa, wenye msongo wa Mawazo nk. Huenda nina chakula cha kutosha hata sijui nipekeleke wapi, huenda nina mavazi mengi mpaka sijui nipeleke wapi. Mtakatifu Mama Teresa wa Kalcuta anasema, “Sio wote tunaweza kufanya mambo makubwa kwa ajili ya wengine, bali sote tunaweza kufanya mambo madogo tu ila kwa upendo mkubwa.“ Fungua macho, ona wenye shida, Saidia kwa upendo, wekeza na utapata baraka za Mungu. Sali sala ya ya mwandishi wa kitabu cha mithali 30:8-9 anayesema, “Uniondolee ubatili na uongo, usinipe umaskini wala utajiri. Unilishe chakula kilicho kadiri yangu, nisije nikashiba na kukukana, nikasema, Bwana ni nani? Wala nisiwe maskini sana nikaiba na kulitaja bure jina la Mungu wangu.”

Wkezeni katika ukimya, tafakari na kufunga
Wkezeni katika ukimya, tafakari na kufunga   (ANSA)

Tatu: Alisahau kuwa mambo yote tutayaacha hapa duniani (He forgot that he was going to die soon or later). Tajiri huyu alivutiwa na kudanganywa na mali na utajiri wake na kuwaza kujilimbikizia zaidi na zaidi kana kwamba ataishi milele. Alisahau ya kuwa kuna siku atakufa na kwamba hatachukua chochote kile pamoja naye. Alipanga mambo yake bila kumshirikisha Mungu na kusahau ya kuwa hataishi milele. Maisha yetu ni mali ya Mungu na muda wowote anaweza kutuita kwake, muda na saa ambayo hauijui. Hivo viuno vyetu vyapaswa kuwa vimefungwa na taa zetu daima ziwe zinawaka, tukija muda wowote Bwana arusi atakuja. Ndugu mpendwa, katika maisha yetu tunapaswa daima kutambua uhalisia huu wa maisha ya kwamba, maisha yetu yapo mikononi mwa Mungu na hatujui ni muda gani atatuita. Kila mmoja apaswa kujiuliza kila siku, nimejiandaaje kuiacha dunia hii? Je, nikifa leo, itakua ndiyo mwisho wa maisha yangu au utakua ndio Mwanzo wa maisha mapya ya umilele pamoja na Mungu aliyenipenda, akaniumba na kunikomboa? Tuandae kesho yetu leo ambayo ipo mikononi mwa Mungu. Mwanamuziki maarufu nchini Marekani Merlyn Sellars katika wimbo wake uitwao, “One day at a time” aliimba, “Yesterday is gone sweet Jesus, and tomorrow may never be mine. Lord, help me today, show me the way, one day at a time” Jana imepita, Ee Yesu mpenzi, na kesho inaweza isiwe yangu. Bwana nisaidie leo, nioneshe njia, siku moja tu kwa wakati” Ishi kwa upendo leo, saidia wengine leo, ijali familia yako leo, jali wengine leo, samehe leo, hurumia leo, tenda haki leo, simamia ukweli leo, jenga urafiki na Mungu leo. Wakati ndio sasa, saa ya wokovu ndio sasa. Weka kesho yako mikononi mwa Mungu. Bwana wewe wajua yote, wewe wajua kuwa nakupenda. Nijalie mwisho mwema.

Kristo Yesu apewe kipaumbele cha kwanza
Kristo Yesu apewe kipaumbele cha kwanza   (@Vatican Media)

Somo la pili: Ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai Kol 3:1-5,9-11. Mtume Paulo katika somo la pili (Kol 3:1-5,9-11) anahitimisha kwa kutukumbusha thamani ya maisha yetu kama Watoto wa Mungu, kwamba, kwa kubatizwa, tulikufa na kufufuliwa pamoja na Kristo na tukapata uzima mpya. Hivyo hatupaswi kuishi tena maisha ya kale, maisha ya dhambi, bali kuishi maisha ya uzima mpya. Tunapaswa kuvua utu wa kale na kuvaa utu mpya, kuachana na anasa, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, Mawazo mabaya na kutamani, kwani huko ni kumwacha Mungu wa kweli na kuabudu mambo hayo. Katika kuishi kwetu, tunapohangaika kuyatafuta mambo ya ulimwengu huu, tunapaswa kutambua kuwa sisi sio wa ulimwengu huu, na hivyo wajibu wetu wa kwanza ni kumtafuta Kristo ambaye alikwisha tuandalia makao yetu ya kudumu mbinguni. Mambo yote ya ulimwengu huu hayadumu milele lakini Kristo anaishi milele. Tukimtafuta na kuishi naye tutatawala naye milele yote. Tunapaswa kuondoa tofauti zote kati yetu kuwa kuwa sote tulikombolewa na mkombozi wetu ni mmoja. Hitimisho. Tumwombe Mungu katika Dominika ya 18 ya Mwaka C wa Kanisa atusaidie tusikie sauti yake anaposema nasi, tusifanye migumu mioyo yetu. Pia tumwombe Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo aijalie nuru macho ya mioyo yetu ili tujue tumaini la mwito wake lilivyo. Amina.

Tafakari D 18 Mwaka C
Ushuhuda wa Fr Alistide
02 Agosti 2025, 11:54