Kard.Pizzaballa:Damu ya kila asiye na hatia katika Gaza na duniani kote haijasahaulika
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kardinali Pierbatttista Pizzaballa, Patriaki wa Kilatini wa Yerusalemu aliadhimisha Misa ya Kupalizwa Mbinguni Bikira Maria katika Monasteri ya Wabenediktini ya Abu Ghosh, tarehe 15 Agosti 2025. Akianza mahubiri yake, Kardinali alisema “Ndugu wapendwa, Bwana awape amani! Leo tunaadhimisha matukio mawili muhimu: Sherehe ya Kupalizwa kwa Bikira Maria Mbinguni na Maandhimisho ya kuanzishwa, kwa Shirika la Watawa Waomblate wa Mtakatifu Franciska Romana kunako 1425, ambapo kunako tarehe 15 Agosti 1433, walipewa ruhusa ya kuishi maisha ya Kitawa na Papa Eugene IV. Kardinali Pizzaballa aliomba ruhusa kufafanua kwa upya kile ambacho wanakiishi katika nuru ya Neno la Mungu ambalo lilisikika. Akianza kunuu usomaji kutoka kitabu cha Ufunuo alisema kuwa “ni kifungu ambacho kimetusindikiza mara kadhaa katika miezi hii yenye uchungu na kimetupatia kitu cha kutafakari. Hakika, ni katika kipindi hiki ambapo tunahisi hitaji kubwa la maneno ya kweli na yenye maana kwetu sisi wenyewe. Ni maumivu ya wakati huu hasa, ambayo hayaturuhusu kutoa hotuba juu ya amani ambazo zimetiliwa chumvi na zisizoeleweka, na kwa hivyo sio za kuaminika, wala kujizuia kwenye uchambuzi au malalamiko mengi. Badala yake, ni juu ya kusimama kama waamini ndani ya hali hii, ambayo haitaisha hivi karibuni.”
Joka Kuu ni kielelezo cha wazo ya nguvu za uovu
Kardinali Pizzaballa aliendelea kusema kuwa: “Joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na vilemba kumi ni kielelezo cha wazi kabisa cha nguvu za uovu duniani, za Shetani, ambaye ana vichwa vingi na vilemba vingi sawa na vile vile, ishara ya mamlaka, na ambaye huvuta theluthi moja ya nyota za mbinguni kuja duniani (Ufu, 12:4 ), yaani, kwa nguvu ya ajabu ya uharibifu usio wa kawaida. Inanishangaza kwamba ni wazi kutokana na kifungu hiki, joka, yaani Shetani, hataacha kamwe kujidhihilisha na ghadhabu katika ulimwengu, hasa “dhidi ya wale wanaozishika amri za Mungu na kumshuhudia Yesu” (12:17). Kwa kusisitiza zaidi alisema Sote tunataka uovu ushindwe haraka iwezekanavyo, utoweke katika maisha yetu.” Patriaki aidha akusema “Ili kufafanua kifungu kutoka katika Injili, tungependa kung’oa magugu kutoka shamba la ngano (rej. Mt 13:30), kutoka kwenye maisha ya ulimwengu. Lakini sivyo ilivyo. Tunajua hili, lakini lazima tuendelee kujifunza kuishi na ufahamu wenye maumivu kwamba nguvu ya uovu itaendelea kuwepo katika maisha ya ulimwengu na katika maisha yetu wenyewe. Hatutaweza kushinda nguvu kubwa ya joka hili kwa nguvu zetu za kibinadamu pekee. Ni fumbo, ingawa ni ngumu na ngumu jinsi ilivyo, ambalo ni sehemu ya ukweli wetu wa kidunia. Sio kukata tama, kinyume chake, ni ufahamu wa mienendo ya maisha duniani, bila kutoroka yeyote, lakini pia bila hofu, bila kushiriki uovu huo, lakini pia bila kuificha.”
Nguvu ya joka haiwezi kushinda uzazi wa Mama
Kardinali Pizzaballa aliongeza kusema “ Lakini sherehe ya leo hii pia inatuambia kwamba kuna mtu ambaye uovu hauna nguvu mbele yake. Nguvu ya joka haiwezi kushinda mbele ya uzazi, Mama anayezaa, ambaye hutoa uhai. Joka haliwezi kushinda mbegu ya uzima, tunda la upendo. Kifungu hicho kinaongeza kwamba mwanamke, mfano wa Kanisa, baada ya kumzaa mtoto wa kiume ambaye ataongoza mataifa kwa uthabiti (12:5), amepata kimbilio jangwani(12:6). Mungu atamwandaa jangwani. Katika Biblia, jangwa si mahali pa kutokuwepo, bali ni mahali ambapo Mungu huwatunza.” Kwa kutazama hali ya vurugu iliyoko huko Nchi Takatifu aliongeza kusema “Katika uzoefu wetu wa sasa, ambao ni mgumu na washida sana, Mungu anaendelea kututunza, akituonya juu ya yote dhidi ya nguvu ya uovu, dhidi ya mamlaka ya ulimwengu ambayo kweli inaonekana kutawala ulimwenguni na katika wakati huu. Sote tunataka hali hii ya vita na matokeo yake kwa maisha ya jamii zetu ikome haraka iwezekanavyo, na ni lazima tufanye kila tuwezalo ili hili litokee, lakini tusidanganyike. Mwisho wa vita bado haungemaanisha mwisho wa uhasama na maumivu watakayosababishiwa.”
Uovu unaonekana kutawala mioyo ya watu
Patriaki aliendelea kusema kuwa: “Bado kutakuwa na hamu ya kulipiza kisasi na hasira katika mioyo ya watu wengi. Uovu unaoonekana kutawala mioyo ya watu wengi hautaacha kufanya kazi, lakini daima utakuwa kazini, ningesema hata kwa ubunifu na tutapambana na matokeo ya vita hivi kwa maisha ya watu kwa muda mrefu ujao. Inaonekana kwamba Nchi yetu Takatifu, ambayo ina ufunuo na udhihilisho wa juu zaidi wa Mungu, pia ni mahali pa udhihirisho wa juu zaidi wa nguvu za Shetani. Na labda ni kwa sababu ni mahali ambapo moyo wa historia ya wokovu unapatikana, pia ni mahali ambapo “Adui wa Kale” anajaribu kudhihirisha zaidi kuliko mahali pengine popote.” Kardinali aliuliza swali: “Je basi, ni nini kifanyike? Kifungu hiki hiki kinatuambia: katika ulimwengu huu wenye vurugu, unaotawaliwa na maovu mengi, sisi, Kanisa, jumuiya ya waamini, sote tunaitwa “kumzaa mtoto wa kiume”, yaani kupanda mbegu ya uzima ulimwenguni. Katika mazingira haya yenye sifa ya kifo na uharibifu, tunatakiwa kuendelea kuwa na imani na kuunganisha nguvu na watu wengi hapa ambao bado wana ujasiri wa kutaka yaliyo mema, na pamoja nao kuunda mazingira ya uponyaji na maisha. Uovu utaendelea kujidhihilisha, lakini tutakuwa mahali, uwepo ambao joka haliwezi kuushinda: yaani ni mbegu ya uzima. Tutaishi jangwani, sio mjini.”
Damu iliyotiririka ni ya ukombozi
“Kwa hiyo hatutakuwa kitovu cha maisha ulimwenguni”, alisisitiza Patriaki kwamba, "Hatutafuata maana ambayo inaambatana na maisha mengi ya wenye nguvu. Pengine tutakuwa wachache, lakini daima kutofautina, kamwe bila kupatana, na labda kwa sababu hiyo hiyo tutakuwa uwepo wa kutatanisha. Bado tutakuwa mahali ambapo Mungu hututunza, kimbilio linalolindwa na Mungu. Bora zaidi, tumeitwa kuwa kimbilio la wale wanaotaka kuhifadhi mbegu ya uzima, katika aina zake zote. Ndiyo, na ni kweli tunajua kwamba baadaye joka litashindwa. Lakini tunajua kwamba ni lazima tuvumilie sasa kwa sababu tunajua kwamba joka litaendelea kuwwepo katika historia. Na damu inayosababishwa na uovu huu wote, damu “wale wazishikao amri za Mungu na kumshuhudia Yesu” (12:17), na ile ya watu wengine wote wasio na hatia, si hapa tu katika Nchi Takatifu, huko Gaza kama ilivyo katika kila sehemu nyingine ya ulimwengu, haitasahaulika.” Kardinali Pizzaballa alikazia kusema “Haitatupwa kwenye kona fulani ya historia. Badala yake, tunaamini kwamba damu hii hutiririka china ya madhabahu, ikichanganywa na damu ya Mwana-Kondoo, ikiunganishwa na kazi ya ukombozi ambayo sisi sote ni sehemu yake. Hapo ndipo tunapopaswa kusimama. Hapo ndipo mahali petu, kimbilio letu jangwani. Maisha ya Kikristo kwa ufupi, ni maisha ambayo hugeuza viwango vya ulimwengu juu chini.”
Mtakatifu Franciska Romana
Kwa kutoa mfano, Kardinali Pizzaballa alisema: “Tanaona hili pia kwa watakatifu wengi wanaume na wanawake; watakatifu wa zamani na sasa. Mtakatifu Franciska Romana, ambaye siku zote alitaka kujiweka wakfu kwa Mungu, badala yake maisha yake yaligeuka. Alilazimishwa kuolewa kinyume na mapenzi yake. Kisha akazaa watoto kadhaa, lakini hatua kwa hatua walichukuliwa kutoka kwake. Hakuwa na maelewano mazuri na familia ya kifalme aliyokuwa nayo, kwa sababu alitapanya pesa zao kwa maskini”. Kwa kifupi,- Patriaki aliongeza kusema “alilazimika kuvumilia magumu mengi sana. Ilikuwa pia vile katika kesi yake ikiwa Shetani alitaka kuzuia hamu yake ya kuishi kwa ajili ya Mungu. Shetani anajua jinsi ya kutengeneza vikwazo. Lakini hawezi kamwe kushinda kabisa. Kiukweli, hata Franciska Romana, ambaye licha ya mateso siku zote alibaki mwaminifu kwa shauku yake ya kujitolea kwa Mungu, aliweza kujiweka wakfu kwa Mungu mnamo tarehe 15 Agosti, miaka 600 miaka iliyopita. Alikuwa mwanamke ambaye, alikamilisha kazi ya Mungu licha ya vikwazo vingi ambavyo mara kwa mara vilizuia mipango ya maisha yake. “Mungu anapoingia kwenye historia, anageuza maisha ya watu. Kama inavyoimbwa wimbo mkuu wa Injili: Aliye juu amenyenyekezwa, aliye chini ameinuliwa. Yeye Aliye juu hutiwa unyenyekevu, yeye aliye chini hutukuzwa. Yeye aliye tajiri anakuwa maskini na aliye maskini kadhalika anakuwa tajiri. Bwana mwenyewe kwanza hubadilisha hali yake mwenyewe. Kwa umwilisho, anakuwa mwanadamu. Yeye, ambaye ni Mungu, anakuwa mwanadamu. Na anageuza kila hali anayokutana nayo njiani, na anafanya hivi hadi Pasaka, wakati hata utawala wa kifo unageuzwa. Mungu hufanya kazi na watu wote kwa njia hii. Anaingia na kuwaangusha. "
Tulibatizwa na kukumbolewa na damu ya Kristo
Patriaki kwa njia hiyo, alisisitiza kuwa tunapoadhimisha ushiriki wake kamili, kwa mwili na roho, katika ushindi wa Kristo, pia ni mfano wa hatima yetu kama watoto wa Mungu, tuliobatizwa na kukombolewa kwa damu ya Kristo. Yeye, aliyebarikiwa kwa sababu aliamini, aliona kwamba mwisho unatangaza mwanzo. Nguvu ya mauti ya joka haitakuwa na neno la mwisho juu ya maisha na historia. Kama Maria, sisi pia tunaweza sasa kuimba kwa imani na matumaini: “Ewe mauti, uko wapi ushindi wako? Ewe mauti, uko wapi uchungu wako?”(rej. 1Kor 15:55 ). Kwa hiyo tunapoondoka kwenye meza ya Ekaristi, leo hii nasi tunachukua pamoja uhakika wa ushindi wa Kristo juu ya mauti, imani kwamba maisha yetu, hata iwe yanageuzwa kiasi gani na matukio ya leo hii ya kusikitisha, hata hivyo ni mahali ambapo joka halitashinda, kwa kuwa ni maisha yaliyomwagika damu ya Mwanakondoo, katika upendo usio na mwisho wa Mungu. Bikira Mtakatifu atuombee, ili mbegu hii ya uzima, mfano wa uzima wa milele unaotungoja, izaliwe ndani yetu na kukaa ndani yetu daima. Amina.” Alihitimisha.