杏MAP导航

Tafuta

Patriaki Bartolomeo:pamoja kama wakristo tunashuhudia kuwa hakuna amani pasipo haki

Mahojiano na Patriaki wa Kiekumeni wa Constantinople na vyombo vya habari vya Vatican:"Katika Ukraine,vita vya kidugu,kashfa kwa Ulimwengu wa Kikristo,hasa ulimwengu wa Kiorthodox."

Andrea Tornielli

 “Kama Wakristo, tunahitaji kutoa sauti zetu, kwa umoja, kama vile ndugu zetu wamefanya,” na “lazima pia tuoneshe nia thabiti ya haki, kwa sababu bila haki hakuna amani.” Patriaki wa Kiekumene wa Konstantinopoli, Bartholomayo, katika Mkutano wa Urafiki kati ya Watu huko Rimini kuzungumza kuhusu mkutano wa Mtaguso wa Nicea, alihojiwa na vyombo vya habari vya Vatican. Alizungumza kuhusu tarehe ya kawaida ya Pasaka kwa Wakristo na ushuhuda wao katika Ulimwengu uliokumbwa na vita. Amemkumbuka Baba Mtakatifu Francisko na kuzungumzia Papa Leo XIV, huku akisisitiza kwamba, safari ya kwanza ya Askofu mpya wa Roma itakuwa nchini Uturuki, kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa Nicea.

Tunaadhimisha kumbukumbu ya miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea, tukio muhimu katika historia ya Wakristo wote na kwa umoja wa Kanisa. Je, Mtaguso huo inatuletea ujumbe gani leo?

Mtaguso wa Nicea ulikuwa hatua muhimu katika historia nzima ya Ukristo. Kulingana na ahadi za Kristo, Roho Mtakatifu amesema na anaendelea kutenda katika historia ya mwanadamu. Mababa wa Nicea, waliobaki imara katika msingi wa Maandiko Matakatifu, walifafanua kile ambacho Kanisa la Kikristo lilikuwa likitangaza kwa karne tatu kupitia ishara za ubatizo, likiratibu ukweli uliotangazwa katika kanuni. Mtaguso unawaamsha tena Wakristo wa Makanisa ya wakati wetu kwa ukweli kwamba Kristo ndiye kweli Logos, ambaye alifanyika mwili, mwanga kutoka kwa mwanga, Mungu wa kweli kutoka kwa Mungu wa kweli, Homoousios, wa kitu kimoja na Baba. Kwani kama Yesu Kristo asingekuwa Mungu, pamoja na Roho Mtakatifu, Utatu wa kweli na usiogawanyika, basi historia ya Kikristo ingekuwa tu falsafa nzuri ya kimaadili na si historia ya wokovu. Kutokana na hili hufuata matendo yetu yote, leo na kesho.

Huko Nicea, tarehe ya Pasaka ilijadiliwa na makubaliano yakatafutwa. Baada ya karne na karne, kwa nini bado haiwezekani kwa Wakristo kuiadhimisha siku ile ile, Jumapili ile ile?

Huko Nicea, iliamuliwa kwamba ilikuwa muhimu kutoa ushahidi wa ufufuko wa Kristo siku hiyo hiyo, kila mahali katika Ulimwengu uliojulikana wakati huo. Kwa bahati mbaya, hali mbalimbali za kihistoria zimekaidi dalili za Mtaguso. Sio kwetu kuhukumu kile kilichotokea, lakini hata leo tunaelewa kwamba ili kuaminika kama Wakristo, ni lazima kusherehekea ufufuko wa Mwokozi siku hiyo hiyo. Pamoja na hayati Papa Francisko, tuliteua tume kuchunguza tatizo hilo. Tulianza mazungumzo. Hata hivyo, kuna hisia tofauti kati ya Makanisa, na kwa hiyo kazi yetu pia ni kuepuka migawanyiko mipya. Kwa Kanisa la Kiorthodox, kile kilichoanzishwa na Baraza moja la kiekumene kinaweza kubadilishwa tu  na Baraza lingine la kiekumene. Hata hivyo, sote tuko tayari kumsikiliza Roho, ambaye, tunaamini, ametuonesha mwaka huu jinsi ilivyo muhimu kuunganisha tarehe ya Pasaka.

Mwaka huu, kiukweli, Wakristo wote waliweza kusherehekea Pasaka siku moja. Pasaka pia ilikuwa siku ya kuonekana hadharani kwa mara ya mwisho kwa Papa Francisko, ya kukumbatiwa kwake kwa mwisho na waamini. Je, una kumbukumbu gani kuhusu Francis, na unadhani alichangia vipi katika mazungumzo ya kiekumene?

Papa Francisko, wa wa hiri ya kumbukumbu, hakuwa Askofu wa Roma tu, kama alivyosema juu yake mwenyewe. Alikuwa pia kaka ambaye tuliunganishwa naye kwa uelewa wa pamoja wa matatizo makubwa ya mwanadamu wa wakati wetu na shauku kubwa ya umoja wa ulimwengu wa Kikristo. Tangu siku ya kuchaguliwa kwake, tulihisi hamu ya kuwapo wakati wa kuwekwa wakfu  kwake: ilikuwa ni mara ya kwanza katika historia kwa Patriaki wa Kiekumene. Tulipambania pamoja kwa ajili ya amani kati ya watu, kwa mazungumzo na imani kuu, mazungumzo ya kidini, kwa ajili ya haki ya pamoja, kwa ajili ya mazingira ya asili, kwa ajili ya mdogo wa dunia. Tumekutana mara nyingi sana, na kila moja ya mikutano yetu imekuwa mkutano kati ya ndugu wanaopendana. Mungu atamlipa kwa yale aliyoyashuhudia kwa maisha yake na kazi yake (Requiescat in pace)- Apumzike kwa amani

Tangu tarehe 8 Mei, tumekuwa na Papa mpya, Leo XIV...

Tayari nimekutana naye mara mbili ...

Kwa hakika, nilitaka kukuuliza jinsi mikutano hii ya kwanza ilivyokuwa na ni nini kilikugusa kuhusu hatua hizi za kwanza katika utume wake kama Askofu wa Roma na Mchungaji wa Kanisa.

Tumevutiwa sana na sura ya Papa mpya, ambaye, ingawa anafanya kazi tofauti na Papa Francisko, tangu mwanzo ameonesha imani yake thabiti ya kuendelea kufuata nyayo za mtangulizi wake. Pia tunahisi uhusiano mkubwa naye, na hasa tunafurahi kwamba ziara  yake ya kwanza nje ya nchi itakuwa kwa Patriaki wa Kiekumene, hadi Uturuki, nyumbani kwetu, na Nicea, ambapo kwa pamoja tutashuhudia imani yetu thabiti ya kuendeleza mazungumzo ya kiekumene na kujitolea kwa Makanisa yetu katika kukabiliana na changamoto za kimataifa. Tunamngoja kwa hamu kubwa.

Baba Mtakatifu, dunia inakumbwa na vita. Kuna mzozo huko Ukraine, jeraha chungu kwa Makanisa pia. Kuna mkasa huko Gaza, ambapo watu wanakufa kwa njaa. Kuna vita vingine ambavyo haviongelewi. Je, tunaweza kufanya nini ili kukuza utamaduni wa udugu na amani?

Kwa bahati mbaya, kuna vita vingi duniani, mara nyingi mbali na tahadhari ya vyombo vya habari vya kimataifa. Na kisha kuna Ukraine, vita vya kidugu, kashfa kwa Ulimwengu wa Kikristo, hasa Ulimwengu wa Kiorthodox. Kuna Gaza na Mashariki ya Kati nzima, ambapo maslahi yaliyo mbali na mahitaji ya wakazi wao husukuma kutoelekea kwenye amani ya haki, bali kuendeleza vita vya kutisha na visivyo vya kibinadamu. Tukiwa Wakristo, tunahitaji kufanya sauti zetu zisikike, tuungane, kama vile ndugu zetu, Patriaki wa Kiothodox ya Kigiriki wa Yerusalemu, Theophilus, na Patriaki wa Kilatini, Kardinali Pizzaballa, walivyofanya. Ni lazima pia tushuhudie nia thabiti ya haki, kwa sababu bila haki hakuna amani. Lakini kama Wakristo, pia tunayo silaha isiyoweza kushindwa: sala. Na hatupaswi kamwe kusahau hili.

 Asante, Baba Mtakatifu, na asante pia kwa kushiriki katika Mkutano huu wa Udugu wa Watu, fursa nyingine ya amani.

 

Nilikubali mwaliko huo kwa furaha na niko hapa Rimini kutoa ushuhuda wangu wa unyenyekevu. Kesho nitarudi Istanbul, kwenye makao makuu yangu.

27 Agosti 2025, 10:05