杏MAP导航

Tafuta

Kila tarehe 28 ya kila Mwaka ni kumbukizi ya Baba wa Kanisa Mtakatifu Agostino Kila tarehe 28 ya kila Mwaka ni kumbukizi ya Baba wa Kanisa Mtakatifu Agostino 

Mt.Agostino Mwalimu wa Kanisa:"Nilichelewa kukupenda&ukaponya upofu wangu"

Mtakatifu Agostino wa Hippo,Padre,Askofu na Mwalimu wa Kanisa ambaye katika maisha yake amefanya mengi.Anakumbukwa katika uongofu wake na urithi wa barua nyingi na vitabu vyenye ushuhuda wa upendo kwa Bwana.Yeye anathibitisha:"Si binadamu anayemtafuta Mungu,bali Mungu ndiye anaye mhurumia mwanadamu mdhambi na kwamba usadiki ili uwelewe,halafu uelewe ili usadiki."

Angella Rwezaula - Vatican.

Kila tarehe 28 Agosti ya kila mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha siku kuu ya Mtakatifu Agostino, Padre, Askofu na  Mwalimu wa Kanisa. Mtakatifu Agostino wa Hippo alizaliwa huko Thagaste, mji huo leo hii unaitwa Souk Ahras nchini Algeria, kunako tarehe 13 Novemba mwaka 354  na mauti yakamfikia kunako tarehe 28 Agosti, 430. Agostino alikuwa mtawa, Mtaalimungu, Padre  na hatimaye kuwa Askofu Mkuu wa Hippo. Wakati wote wa ujana alifuata anasa za dunia na uzushi, bila kujali machozi ya Mama yake Monica ambaye alitamani kuona mwanae anabadilika.  Agostino alipata elimu yake nzuri ya lugha na Falsafa na ya ufasaha wa kuhubiri huko Thagaste, Madaura na hata katika Chuo Kikuu cha Karthago (karibu na Tunis,   ingawa hakuwa daima mwanafunzi mzuri, mbali na kuwa na akili ya kipekee. Hata hivyo alimudu kikamilifu Kilatini, lakini si sana Kigiriki ambapo Baba yake Patrick alifurahia uwezo wake mpana wa masomo.

"Nguvu mbili zinazouungoza kwenye ujuzi"

Akiwa huko Karthago, mwaka 373 alisoma kitabu cha maadili cha Sisero ambacho kilibadilisha hisia zake,  kwa maana hiyo ataandika kuwa:“matumaini yote ya bure yakawa hayana maana kwangu, nikatamani hekima isiyokufa kwa ari isiyosemeka moyoni mwangu. Lakini kwa kuamini ukweli haupatikani pasipo Yesu, ambaye hatajwi katika kitabu hicho, Agostino, alianza kusoma Biblia, ila hakupenda tafsiri ya Kilatini wala yaliyomo, akiyaona tofauti na mtindo wa falsafa inayotafuta ukweli. Kutokana na hilo alisogea mbali na dini iliyoonekana kutotia maanani hoja za akili yake ambayo pamoja na imani ndizo: “nguvu mbili zinazotuongoza kwenye ujuzi.” Ataandika baadaye  kwenye maungamno akitoa pia kauli mbili za msingi kuhusu kulenga ukweli kwamba: “Usadiki ili uelewe” halafu “uelewe ili usadiki”.

Kujitafutai dini ya kuridhisha hamu yake ya kujua ukweli na karibu na Yesu

Mtakatifu Agostino hapo, kusudi asiishi bila Mungu, alijitafutia dini ya kuridhisha hamu yake ya kujua ukweli na ya kuwa karibu na Yesu, akajiunga kwa karibu miaka 10 na harakati iitwayo  “Umani”. Hii ni dini  iliyodai kufuata akili na kufafanua sababu ya mabaya kuwepo duniani kutokana na chanzo cha pili cha ulimwengu kilicho kinyume cha Mungu, huku ikikataa Agano la Kale ili kufuata Ukristo wa kiroho. Agostino alipenda pia maadili ya dini hiyo kwa sababu yalikuwa yanawadai sana baadhi ya waamini tu, yakiwaacha wengine wote wasijali zaidi. Hatimaye Wamani hao  walikuwa wanasaidiana kupanda mbegu zao katika jamii. Lakini alipokutana na Askofu wao Fausto, alikosa imani nao kwa kuona yeye alivyoshindwa kujibu maswali yake aliyokuwa nayo.

Uwongofu na ubatizo

Uongofu wake ulitimia kunako tarehe 15 Agosti 386, akiwa na umri wa miaka 32, aliacha kufundisha na hata kuishi na mama mtoto, huku akaenda kwa muda huko  Cassiciaco karibu na ziwa la Como nchini Italia lakini akiwa na Monika, mwanae  Adeodatus aliyemzaa na mwanamke aliyekuwa anakaa pamoja huko Algeria, na marafiki wachache, baadaye atarudi Milano na kubatizwa na Ambrosi (Mtakatifu) pamoja na mwanae na rafiki yake Alipio usiku wa Pasaka mnamo  mwaka 387. Baada ya kubatizwa hatimaye na kunuia kuishi kitawa Thagaste, huko  Afrika, bali  akiwa njiani, huko Ostia, katika Bandari ya Roma, Mama  yake Monica akafa. Ndoto yake ilikuwa kujitosa katika maisha ya sala na masomo pamoja na marafiki wake. Lakini hiyo ilidumu miaka mitatu tu.

Padre na Askofu 

Kwa kifupi mwaka 391 bila kutarajia alipewa daraja ya Upadre huko Hippo, mahali alipoanzisha monasteri, huku akigawa muda wake kati ya sala, masomo na mahubiri, halafu mwaka 395 akachaguliwa kuwa Askofu  msaidizi wa mji huo na mwaka 397 akawa Askofu wa jimbo hilo. Agostino ilimbidi akubali matakwa ya Mungu kwake, kwamba ajitoe kwa wengine na kuwashirikisha ujuzi wake ili kuishi kweli kwa ajili ya Kristo.  “Kuhubiri mfululizo, kujadili, kusisitiza, kujenga, kuwa tayari kwa yeyote ni jukumu kubwa sana, ni mzigo mzito, ni juhudi ya ajabu.”Ilikuwa kama uwongofu wake wa pili. Hapo alitegemeza maskini na watoto yatima, alisimamia malezi ya wakleri, akiwadai waishi pamoja, huku akaeneza Monasteri za kiume na za kike. Alifanya adhimisho la Ekaristi kuwa kiini cha maisha ya Jumuiya zake. Mahubiri yake mengi yanaonesha alivyojua kujadiliana na umati akitumia maneno rahisi na ya kawaida na hata ucheshi katika kulinganisha Neno la Mungu na mazingira yao. Kwa tabia yake karimu na pendevu, hisia zake, uvumilivu na utayari wa kusamehe alifanya hata maadui kadhaa kuwa marafiki. Maisha yake ya Kiroho yaliyoongoza uandishi wa kanuni yake kwa watawa yamefuatwa na mashirika mengi ya kiume na ya kike hadi leo hii,

Kwa miaka 35 mpaka kifo chake, mbali na kutimiza majukumu yake mengi, aliendelea kueleza na kutetea imani sahihi ya Kikristo kwa mahubiri, maandishi na vitabu vingi sana (hata vya mitindo mipya) dhidi ya aina zote za uzushi za wakati ule kama vile: Wamani, Wadonati, Wapelaji na Waario. Hivyo tangu alipokuwa hai, hakuongoza Kanisa la Afrika Kaskazini tu, bali alitegemeza imani kila mahali. Kwa njia hiyo Agostino amekuwa mwalimu muhimu sana katika Ukristo, hasa wa Magharibi (yaani Kanisa Katoliki na katika Uprotestanti uliotokea katika Kanisa hilo. Kwa mfano Martin Luther alimtaja kuwa Baba yake wa kiroho pamoja na Mtume Paulo.) Agostino alijimwilisha tunu za Kikristo na kutokeza utajiri wake wa dhati, huku  akibuni mawazo na mifumo ya kulisha vizazi vijavyo. Hata nakala za vitabu vyake ni nyingi sana, zikithibitisha jinsi gani vilipendwa na kuenea. Hivyo Basi Agostino  aliathiri sana ustaarabu wa Magharibi unaozidi kuenea leo duniani kote. Mawazo yote yaliyomtangulia yanakutana katika maandishi yake na kuwa chemchemi ya mafundisho kwa nyakati zilizofuata.

Miaka ya mwisho

Tarehe 26 Septemba mwaka 426 alikusanya waamini ili kuwatambulisha Padre  Eraklio aliyemchagua kama Mwandamizi wake, ili naye aweze kutumia miaka yake ya mwisho katika kusoma kwa dhati zaidi Maandiko Matakatifu. Watu walimkubalia kwa shangwe. Miaka minne iliyofuata Agostino alifanya kazi kubwa kwa kumaliza vitabu mbalimbali na kuanza kuandika vingine. Kati ya vile vya wakati huo kuna “Retractationes”(yaani “Kupitia Upya” vile vilivyotangulia), ambamo tunaona unyoofu wake wa kuwa tayari kurekebisha baadhi ya mafundisho aliyowahi kuyatoa. Hivyo mpaka mwisho Agostino alionyesha alivyolenga ukweli kuliko yote. Pia miaka hiyo alijadiliana na wazushi hadharani na kurudisha amani iliyohatarishwa na makabila ya kusini yakifaidika na matatizo kati ya Kaisari na Jemadari wake Bonifas. Agostini alimwandikia mpatanishi kuwa: “Ni utukufu mkubwa zaidi kuzuia vita vyenyewe kwa neno moja, kuliko kuangamiza watu kwa upanga, na vilevile kusababisha au kudumisha amani kwa amani kuliko kwa vita. Kwa sababu wanaopigana, ikiwa ni watu wema, bila shaka wanalenga amani, ila kupitia damu. Kumbe kazi yako ni kuzuia umwagaji damu.”Hata hivyo, tumaini lilitoweka Bonifas alipoalika kwa hasira wakana Mungu wa Kijerumani walioitwa Wavandali kutoka Hispania ili wavamie Afrika.

Kifo cha Mtakatifu Agostino

Agostino aliaga dunia akiwa Hippo tarehe 28 Agosti 430, wakati Wavandali walipokaribia kuteka mji wake baada ya kuuzingira miezi mitatu, huku wakibomoa makanisa na nyumba za vijijini na kuua au kukimbiza wakazi, wakiwemo watawa. Baadhi waliteswa na kuchinjwa, wengine walibakwa au kufanywa watumwa. Mbele ya maovu hayo yaliyokomesha ustaarabu wa Kirumi, Agostino alizidi kutafakari fumbo la Maongozi ya Mungu ili kujifariji na kuwatuliza wengine kama alivyofanya miaka 20 ya nyuma, Roma ilipotekwa kwa mara ya kwanza na Wagoti. Aliona ustaarabu huo ulikuwa umechakaa, kumbe Kristo tu hazeeki kamwe na ni wa kutegemewa. Ndiye kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki katika Afrika Kaskazini mwanzoni mwa karne ya 5. Kutokana na maisha, mafundisho na maandiko yake bora, tangu zamani anaheshimiwa kama Mtakatifu na Baba wa Kanisa. Na kunako Mwaka 1298,  Papa Bonifasi VIII alimuongezea sifa ya kuwa mwalimu wa Kanisa.

Dhambi na Neema

Mtakatifu Agostino anakumbukwa sana katika suala la ‘dhambi na neema’: Katika suala la neema na dhambi ni Agostino aliyefundisha kwamba ubinadamu umerithi dhambi ya asili kutoka kwa Adamu. Uhuru wa asili umepotezwa na dhambi hiyo, na hali hii imerithiwa na watu wote baadaye. Lakini kwa neema yake Mungu hufunua upendo wake kwao. Alisisitiza kwamba si binadamu anayemtafuta Mungu, bali Mungu ndiye anayemhurumia mwanadamu mwenye dhambi. Utakaso unaopatikana kwa imani unasababisha ondoleo kamili la dhambi zote kabisa. Halafu mwamini anazidi kufanywa mpya kwa mchakato utakaokamilishwa na ufufuko wa siku ya mwisho. Mchakato huo wote ni kazi ya neema ya Mungu: bila hiyo, binadamu hawezi kuongoka, kukwepa dhambi na kufikia utimilifu wa wokovu. Hayo yote ni zawadi tu ya Mungu, kama vilivyo pia udumifu na stahili za mtu. Sisitizo hilo la kwamba neema ni dezo, lilimuongoza Augustino kufundisha juu ya uteule, neema ambayo hakuna anayeweza kuikataa na ambayo inafikisha kwa hakika mbinguni. Kwa nini Mungu hawapi wote neema hiyo ni fumbo ambalo tuliinamie tu, kwa sababu hatuwezi kabisa kulielewa. Kwa vyovyote haiwezekani kumlaumu Mungu kwa ajili hiyo, eti si haki. Mawazo hayo yalikuja kukaziwa zaidi tena na watu kama Martin Luther, Yohane Kalvini na Janseni, namna iliyokataliwa na Kanisa Katoliki.

Sala za Mtakatifu Agostino ni za kusisimua

Sala zake Mtakatifu Agostino zimekuwa ni mwanga mkuu kwa kila mmoja mwenye kujikita katika hija ya Bwana, kumtafuta bila kuchika kwa sababu yeye anaandika: Wewe Bwana ni mkuu na unastahili kabisa sifa. Uweza wake ni mkuu na hekima yako haina mipaka. Mtu anataka kukusifu, yeye aliye sehemu ndogo ya viumbe vyako vyote, yeye anayetembea akielekea kifo, ushahidi wa dhambi yake, wa kwamba wewe unapinga wenye kiburi. Hata hivyo mtu, sehemu ndogo ya viumbe vyako vyote, anataka kukusifu. Wewe unamchochea aonje furaha ya kukusifu, kwa kuwa umetuumba kwa ajili yako, na moyo wetu hautulii mpaka ustarehe ndani mwako. Ee upendo wenye kuwaka daima usiweze kuzimika kamwe, Mungu wangu uniwashe moto! Unijalie mimi, mimi pia, Bwana wangu mpenzi, nikujue, nikupende na kukufurahia.

Nisipoweza kufanya hayo kikamilifu katika maisha haya, unijalie walau kusonga mbele kila siku hata niweze kufikia kuyafanya kwa ukamilifu. Acha nikufahamu zaidi na zaidi hata ukamilifu. Acha nikupende kila siku zaidi na zaidi hata ukamilifu; furaha yangu iwe kubwa kwa yenyewe, na kamili ndani yako. Wewe ni nini kwangu? Uniwie huruma, niweze kusema. Mimi ni nini kwako, hata uniagize nikupende, halafu nisipokutii unanikasirikia na kunitishia maafa makubwa? Je, kutokupenda si balaa kubwa tayari? Lo, kwa huruma yako, Bwana Mungu wangu, uniambie wewe ni nini kwangu. “Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako”. Sema hivyo, nami nitasikiliza. Tazama, moyo wangu unakusikiliza, Bwana; uuweke tayari ukaniambie, “Mimi ni wokovu wako”. Nitafuata sauti ya neno lako hilo hata nikufikie. Usinifiche uso wako: nife nisije kufa, bali niuone uso wako.

Unijalie nifanye unachoagiza, halafu uniagize unachotaka: Nimechelewa kukupenda, Uzuri wa kale na mpya daima; nimechelewa kukupenda. Tazama, wewe ulikuwa ndani mwangu, nami nilikuwa nje na kukutafuta huko. Mimi, mbaya, nilikuwa ninaparamia vitu vizuri ulivyoviumba. Wewe ulikuwa nami, lakini mimi sikuwa nawe. Vilikuwa vikinishika mbali nawe viumbe vile ambavyo kama visingekuwa ndani yako hata kuwepo visingekuwepo. Uliniita, ukanipigia kelele, ukashinda uziwi wangu. Uliniangaza, ukanimulikia kama umeme angani, hatimaye ukaponya upofu wangu. Ulinipulizia harufu yako nami nikainusa, na sasa nakuonea shauku. Nimekuonja na sasa nakuonea njaa na kiu. Umenigusa nami sasa nawaka tamaa ya kupata amani yako. Sasa nakupenda wewe tu, nakufuata wewe tu, nakutafuta wewe tu, niko tayari kukutumikia wewe tu, kwa kuwa wewe tu unatawala kwa haki, natamani kuwa chini ya uwezo wako. Naomba kitu hiki tu kutokana na hisani yako kuu: kwamba unigeuzie kabisa kwako, usiruhusu chochote kunizuia nisielekee kwako.

Historia yake na maandiko yake ni ya kusisimua sana  na kuvutia kuendelea kumtafuta Bwana kila wakati, kwa utambuzi wa kuwa sisi sote ni wadhambi, na kukumbuka ushuhuda wake kwamba hatutaweza kabisa kutulia hadi tunapumzika ndani mwake Yeye...!

Kumkukumbu ya Mt.Agostino

 

28 Agosti 2025, 08:56