Malawi:Kongamono la I la Ekaristi kitaifa:Ekaristi,chanzo na kilele cha mahujaji wa matumaini
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kutafakari na kusali kuhusu umuhimu wa Sakramenti Kuu katika maisha ya mahujaji wa Matumaini katika Mwaka huu wa Jubilei 2025, ndiyo yalikuwa madhumuni ya Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Ekaristi Takatifu, lililofanyika mjini Lilongwe nchini Malawi kuanzia tarehe 5 hadi 10 Agosti 2025 kwa kwa kushirikisha majimbo katoliki yote 8 ya nchi inayohesabiwa kuwa na wakatoliki karibu milioni 3 yenye wakazi milioni 19. Katika Kongamano hilo lililoongozwa na Kauli mbiu: “Ekaristi: chanzo na kilele cha mahujaji wa matumani, kama sehemu ya Jubilei tunayoendelea nayo, lilipata hata baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV, kupitia Katibu Mkuu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin aliyeshiriki.
Wakati wa Ufunguzi wa Kongamano la kwanza uliofunguliwa na Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Balozi wa Vatican nchini Malawi na Zambia, Askofu mkuu Gian Luca Perici, na kuhudhuriwa pamoja na Katibu wa Vatican Kardinali Pietro Parolin, ambaye alitoa salamu zake kutoka kwa baba Mtakatifu Leo XIV. Balozi wa Vatican nchini Malawi, alibanisha kuwa: "Jambo muhimu zaidi sio kile tunachofanya na Ekaristi, lakini kile tunachofanya kwa Ekaristi.” Maneno yake yaliungwa mkono Askofu Mkuu wa Jimbo la Lilongwe George Desmond Tambala ambaye alisisitiza kwamba, “kiini cha Ekaristi katika maisha ya Mkristo si chaguo au chaguo la mtu binafsi, bali ni agizo la moja kwa moja kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe.”
Tamko la mwisho la lengo kuu, ambalo lilitokana na ripoti sita zilizowasilishwa kwenye Kongamano hilo, liliakisi vipaumbele vifuatavyo: kusambaza tafakari na matunda ya Kongamano kwa waamini wote katika kila ngazi ya Kanisa, kukuza ibada ya kina zaidi kwa Sakramenti Takatifu, na kuhimiza tafakari na katekesi inayoendelea kuhusu fumbo la Sakramenti Takatifu. Wakati wa Kongamano hilo, wajumbe pia waliamua kuandaa orodha ya maazimio, ikiwa ni pamoja na maandalizi makini ya sherehe za kiliturujia, kwa kuanzia na nyimbo zinazopaswa kuwasaidia waamini kushiriki kikamilifu katika Liturujia, na huduma ya kichungaji kwa wabatizwa ambao hawawezi kupokea sakramenti, ili waweze kupatana na kurudi katika ushiriki kamili wa Kisakramenti.
Fursa ya ukimya
Usichukue fursa ya ukimya wa Yesu katika Ekaristi kufikiri kwamba tunaweza kumvunjia heshima kwa kukiuka kanuni za kiliturujia. Hili lilikuwa onyo kutoka kwa Monsinyo Thomas Luke Msusa, Askofu Mkuu wa Blantyre, katika mahubiri yake wakati wa Misa ya kufunga Kongamano la Kitaifa la Ekaristi Takatifu la Malawi, lililoadhimishwa katika Kanisa kuu la Lilongwe, mji mkuu, Dominika tarehe 10 Agosti 2025. Kwa mujibu wa Tovuti ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki (AMECEA,) liliripoti kuwa, Askofu Mkuu Msusa alilaani matumizi ya simu wakati wa Misa, hata kwa kupiga soga.“Ikiwa tunaamini kwamba Yesu Kristo yupo katika sakramenti ya Ekaristi, tunapaswa kuonesha imani hii kwa jinsi tunavyoomba. Tuna simu za mkononi zinazorekodi, hata kama sisi si waandishi wa habari. Badala yake, lazima tusikilize na kusali." Askofu alirejea histotoria kibiblia ya mwito wa Mungu kwa Musa kwenye Mlima Horebu, akiwahimiza waamini kudumisha heshima wakati wa liturujia. “Musa alipotambua kwamba alikuwa amesimama mbele ya Mungu, alivua viatu vyake mara moja na kupiga magoti, akionesha heshima ya Mungu,” Kadhalika askofu Mkuu aliwaalika waamini hao kukaribia sakramenti ya upatanisho kwa uzito.
Ifuatayo ni orodha ya maazimio saba ya Kongamano la Ekaristi mwishoni mwa tukio hilo:
1) Kukuza heshima kwa Sakramenti Takatifu kama uwepo wa kweli na halisi wa Kristo.
2) Mapadre, kama wahudumu wa kawaida wa Ekaristi, wanapaswa kukuza heshima kwa Ekaristi.
3) Ibada na Baraka katika parokia zisichukuliwe kuwa ibada ya faragha kwa makundi fulani, bali ni wajibu kwa Wakristo wote katika kila parokia.
4) Namna ya Kuabudu, kama inavyotolewa katika vitabu vipya vya nyimbo katika lugha za Chichewa na Chitumbuka, inapaswa kujulikana kwa waamini wote.
5) Sherehe za kiliturujia zinapaswa kutayarishwa vya kutosha, na kwaya zisaidie kutaniko ili kushiriki kikamilifu katika liturujia kwa kuchagua nyimbo zinazojulikana sana na waamini.
6) Inapendekezwa sana kwamba Ekaristi ipokelewe kwa ulimi.
7) Wachungaji wote wanapaswa kuweka kipaumbele katika kueneza mafundisho ya Sakramenti Takatifu na kutoa huduma ya kichungaji kwa Wakristo wanaozuiwa kupokea sakramenti hizo, ili wapate upatanisho na kurudi katika ushiriki kamili wa sakramenti.