Maaskofu wa Korea wazindua upya Harakati ya Pro-Life huku kukiwa na mijadala ya utoaji mimba
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Askofu Moon Chang-woo wa Jeju, rais wa Kamati ya Familia na Maisha ya Baraza la Maaskofu wa Korea, alitangaza mipango ya kupanua kampeni ya “kuamsha hisia za utume na wito wa kulinda maisha kutoka mwanzo hadi mwisho wake wa asili” na “kupaza kilio cha kinabii.” Alisema mpango huo unalenga kurejesha "heshima isiyoweza kuepukika kwa maisha ya binadamu" kwa mjadala wa umma na hatua za kisiasa, kulingana na ripoti la Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari la Vatican Fides. Harakati hilo lililobuniwa katika ngazi ya kitaifa, linalenga kuratibu mipango mbalimbali ya kikanda, kama vile “Mpango wa Maisha Yanayozaliwa Kabla ya wakati(Njiti),” unaotoa matunzo na usaidizi kwa akina mama wanaohitaji na ambao unakuza “Utamaduni wa Maisha” kupitia shughuli za kitamaduni na utetezi. Tarehe 26 Agosti 2025, Askofu Moon, akifuatana na wawakilishi wa mashirika ya Kikatoliki ikiwa ni pamoja na Kamati ya Maadili ya Baraza la Maaskofu na Taasisi ya Utafiti wa Maadili ya Kikatoliki, walikutana na Kamati ya Afya ya Bunge kujadili marekebisho ya Sheria ya Afya ya Mama na Mtoto.
Onyo la maaskofu kuhusu kutoa mimba
Mswada huo, unaoungwa mkono na wanachama 11 wa Chama cha Kidemokrasia cha Korea, unalenga kushughulikia mapengo ya kisheria yaliyoachwa na uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba ya 2019 iliyotangaza utoaji wa mimba kuwa kinyume na katiba. Iwapo itapitishwa, Maaskofu walionya, marekebisho hayo yataruhusu utoaji mimba hata wakati kiini tete kinaweza kuwa nje ya tumbo la uzazi na kuondoa vizuizi vya utoaji mimba kwa hiari. Kanisa lilisema hatua kama hizo zitaruhusu "utoaji mimba bila vikwazo," na kunyima kiiumbe haki yake ya kuishi.
Kuna haja ya kutoa elimu
Padre Leo Oh Seok-jun, Katibu Mkuu wa Kamati ya Pro-Life ya Jimbo Kuu la Seoul, nchini Korea Kusini alisisitiza haja ya elimu kwa umma kuhusu suala hilo. "Kumekuwa na mijadala mingi juu ya suala hili hapo awali: Tunapinga uavyaji mimba, bila kujali umri wa ujauzito," alisema. Padre huyo alisema ni muhimu kueleza kwa uwazi na kwa kina suala hilo kwa umma “ili waamini na watu wote wenye mapenzi mema wasipoteze thamani kuu ya maisha, ambayo ni heshima ya maisha ya mwanadamu.” Mjadala huo pia umeendelea hadi maswala ya mwisho wa maisha, kwani Askofu Ku Yoo-bi, Askofu Msaidizi wa Seoul na rais wa Kamati ya Maadili ya Kibiolojia, alihutubia kuhusu euthanasia na kusaidia kujiua wakati wa Kongamano la tarehe 28 Agosti 2025 katika Bunge la Kitaifa.
Ubinadamu wa jamii unapimwa jinsi unavyowajali wagonjwa na wanyonge
"Ongezeko la mahitaji ya euthanasia na kusaidiwa kujiua leo ni kwa sababu ya kupoteza matumaini ya kupona," Askofu Ku alisema. "Wakati jamii yetu inasisitiza ufanisi na tija tu, kutunza wagonjwa kunatazamwa kama shughuli ya ubadhirifu na isiyo na maana, ambayo husababisha wagonjwa kusukumwa hadi vifo vyao." Alisisitiza kwamba ubinadamu wa jamii unapimwa kwa jinsi inavyowajali wagonjwa na wanyonge, akionya kwamba kupuuza au kutelekeza wagonjwa walio katika mazingira magumu kuelekea kifo kunaondoa jamii msingi wake wa maadili. Pia alionya dhidi ya kutunga kujiua kwa kusaidiwa kama kitendo cha huruma, na kuiita upotoshaji wa utunzaji wa kweli. Kwake yeye, kujiamulia kunaweza kutumika tu kwa walio hai na hakuwezi kuzidi haki ya msingi ya kuishi, kwani kifo hakiwezi kuchukuliwa kuwa haki.