Maaskofu Katoliki wa Afrika(SECAM)wajadili maono ya kichungaji ya 2025-2050!
Na Paul Samasumo – Kigali.
Zaidi ya Maaskofu 250 wa Kikatoliki wanaowakilisha mabaraza mbalimbali ya Maaskofu barani Afrika wanahudhuria Mkutano Mkuu wa 20 wa SECAM. Siku ya Kwanza ilianza kwa Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Kukuza Maendeleo Fungamani ya Kibinadamu kuanzia 2016 hadi 2021, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Cape Coast nchini Ghana, na kuanzia tarehe 4 Aprili 2022 alikuwa Kansela wa Chuo cha Kipapa cha Sayansi na Chuo cha Kipapa cha Sayansi ya Jamii, nyadhifa alizoshika hadi tarehe 21 Aprili 2025. Kwa njia hiyo misa ilikuwa katika Parokia ya Regina Pacis huko Kigali. Na ikijulikana kwa ukarimu wake mchangamfu, Parokia ya Katoliki ya Regina Pacis inahudumia jumuiya mbalimbali na kutoa Misa katika lugha ya Kinyarwanda, Kiingereza na Kifaransa.
Kwa nini SECAM?
Wakati wa kikao cha kusikilizana kilichofanyika katika Ukumbi maarufu wa Mikutano huko Kigali, Maaskofu walikumbushwa kuhusu madhumuni ya SECAM. Kikao hicho kililenga kuthibitisha ni kwa nini Shirikisho la mabaraza ya Maaskofu lipo na kuwafahamisha ‘maaskofu vijana’ na sababu ya kuwa SECAM. Mada hiyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Cape Coast, nchini Ghana, Gabriel Charles Palmer-Buckle. Kwa njia hiyo Askofu Mkuu Palmer-Buckle alitoa mada yake kupitia tafakari ya historia ya SECAM, akishirikisha takwimu, nukuu kutoka katika vikao vya awali, na hati husika za Kanisa. Mwishoni, Maaskofu walikubaliana kwamba, kadiri ulimwengu unavyobadilika kwa kasi, ndivyo wanavyohudumiwa vyema zaidi kwa kushirikiana ili kukabiliana na changamoto za pamoja za kichungaji zinazolikabili Kanisa Barani Afrika.
Afrika katika Njia panda
Kanisa na serikali ya Rwanda hazijaacha juhudi zozote kuhakikisha Mjadala wa SECAM unafanikiwa. Waziri Mkuu wa Rwanda, Dk. Justin Nsengiyumva, alihutubia katika siku ya kwanza. Aliwapongeza Maaskofu kwa kuichagua nchi ya Rwanda kuwa nchi mwenyeji na kulipongeza Kanisa la Afrika kwa kuwa mshirika wa kutegemewa wa serikali nyingi—hasa katika huduma za kijamii, elimu na afya.
Waziri Mkuu huyo alisema kuwa,"Afrika iko katika njia panda. Majeraha ya siku za nyuma bado yanapona, na shinikizo mpya za kimataifa zinaibuka. Lakini ndani ya changamoto hizi kuna fursa ya pekee ya kufanywa upya. Kanisa Barani Afrika, kama sauti ya dhamiri, lina jukumu muhimu katika kuhamasisha uongozi wa kimaadili, kukuza utu, na kuimarisha dira ya maadili ya mataifa yetu," alisema.
Kardinali Ambongo - Kristo anatembea na Afrika
Akifungua kikao hicho, Rais wa SECAM, Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Kinshasa, alitoa wito wa kusitishwa kwa migogoro ya kivita inayoendelea barani humo. Kardinali huyo wa Kinshasa aliongeza hivi: “Mada ya Mkutano huu ni ‘Kristo, Chanzo cha Tumaini, Upatanisho, na Amani’ ambayo inagusa sana nafsi ya bara letu.” Katika ulimwengu uliovunjwa na vita, umaskini, kulazimishwa kuhama makazi yao, na matatizo ya kimazingira, tunaelekeza macho yetu kwa Kristo, ambaye ndiye chanzo hai cha uponyaji na kufanywa upya.”
Kardinali aliongeza: “Yeye ndiye anayetembea na Afrika katika majeraha yake, ambaye anapatanisha mioyo iliyogawanyika, na ambaye hutoa matumaini pale ambapo kukata tamaa kunatishia. Kama wanafunzi, tumeitwa kuwa mafundi wa amani, manabii wa matumaini, na vyombo vya upatanisho. Hii si tu imani ya kitheolojia bali ni dharura ya kichungaji. Kanisa Barani Afrika lazima liwe ishara na sakramenti ya umoja, haki na amani ya kudumu."
Vilevile, Askofu mkuu Arnaldo Sanchez Catalan, Balozi wa Vatican nchini Rwanda, alihimiza kuendelea kwa mipango ya amani kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hasa kuhusu mzozo wa mashariki mwa Congo. “Kuna matumaini makubwa ya amani ya kweli na ya kudumu. Majaribio mengi yamefanywa huko nyuma,” alisema. “Tunaomba kwamba wakati huu, mazungumzo ya amani na makubaliano yatafanyika na kuleta amani ya kudumu.”
Pia katika Mkutano wa Mjadala wa SECAM alikuwa ni Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kuhamaisha Maendeleo ya Kibinadamu. Alipendekeza njia za kivitendo ambazo Kanisa Barani Afrika lingeweza kushirikiana na Baraza la Kipapa hilo. Wawakilishi kutoka mabara mengine, Asia, Amerika Kusini, Amerika Kaskazini, na Ulaya pia walizungumza kwenye mkusanyiko huo na kutoa jumbe mbali mbali za mshikamano. Mashirika mengi ya kidini kutoka duniani kote yanashiriki, na hivyo kufanya mkutano huo kuwa uliojaa idadi na shughuli mbali mbali.