Maaskofu nchini Colombia:Amri ya haki inayohakikisha ushiriki wa jamii!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baraza la Maaskofu nchini Colombia (CEC) lilielezea masikitiko yake makubwa kufuatia na kifo cha Seneta Miguel Uribe Turbay, kilichotokea Jumatatu tarehe 11 Agosti 2025 kutokana na shambulio la Juni 7 huko Bogotá. Katika taarifa rasmi, Maaskofu hao walionesha mshikamano wao na familia ya mbunge huyo wa zamani, waliyemkabidhi kwa Bwana wa faraja katika saa hii ya maombolezo. Ofisi ya Urais ya Uaskofu ilitoa mwito mkali kwa mamlaka kuwa: "Tunaziomba mamlaka husika na vyombo vya dola kuendeleza juhudi zao za kufafanua ukweli kuhusu mauaji haya, ili yaadhibiwe." Wakati huo huo, Maaskofu waliwataka Wakolombia "kutoruhusu matumaini kuibiwa na kulinda amani ambayo ni tunu za kitaifa, kwa kuzingatia kauli mbiu ya nembo: "Uhuru na Kanuni!" Katika maelezo yao walimza hiyo ni bora na inamaanisha: "Uhuru kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu, heshima kwa tofauti bila vurugu, na ulinzi wa maisha katika aina zake zote: Kanuni ya haki ambayo inahakikisha ushiriki wa kijamii, maelewano, na heshima kwa haki za raia.”
Kardinali Aparicio: huu si wakati wa kutugawanya bali kutuunganisha
Na kwa upande wa Kardinali Luis José Rueda Aparicio, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Bogota kupitia ujumbe kwa njia ya video, alionesha kuunga mkono huzuni ya familia ya Uribe Turbay na kusema kuwa: "Leo tunataka kuwaambia familia ya Uribe Turbay kwamba tunawakumbatia(...) Sasa tunamkabidhi kwa Mungu Baba, ili ampokee katika nyumba yake ya milele." Kardinali huyo alitoa wito wa umoja wa kitaifa kuwa: "Huu si wakati wa kutugawa. Huu ni wakati wa kuungana," na kusisitiza "kukataa vurugu zote."
Jumbe zote mbili zilikubaliana kwamba: "vurugu si njia ya maisha au maendeleo" na kusisitiza changamoto ya kujenga "usawa, haki, upatanisho na amani." Baraza la Maaskfu nchini Colombia(CEC ),ilihitimisha taarifa yake kwa maombi kwa ajili ya Colombia, likiomba kwamba: "maadui warudi kwenye urafiki, wapinzani waungane, na watu watafute umoja."